-->
UTANGULIZI.
Uhuru wa kujumuika unawapa wafanyakazi
uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Vilevile unawapa
wafanyakazi haki ya kushiriki katika shughuli za vyama vyao kwa uhuru bila hofu
ya kubaguliwa au kunyanyaswa au kupoteza haki yoyote.
Hata hivyo, uhuru wa kuunda na kujiunga
na vyama vya wafanyakazi una mipaka yake. Uhuru huu umewekewa mipaka kwa
wafanyakazi wa kada zifuatazo:-
a)
Mahakimu
– hawa wanaweza kuunda na kujiunga na Chama cha Maafisa wa Mahakama pekee.
b)
Waendesha
Mashitaka – hawa wanaweza kuunda na kujiunga na chama cha Waendesha Mashitaka
au Watendaji wengine wa Mahakama pekee.
c)
Wafanyakazi
wa kada ya Meneja Mwandamizi ambaye kwa nafasi yake ana mamlaka ya kutengeneza
sera kwa niaba ya muajiri na ana mamlaka ya kuingia majadiliano na Chama cha
Wafanyakazi, haruhusiwi kujiunga na Chama cha Wafanyakazi wasio Mameneja
Wandamizi.
Pia uhuru wa kuunda na kujiunga na
vyama vya wafanyakazi unatoa kinga ya mfanyakazi kutobaguliwa na mtu yeyote kwa
sababu ya kuwa mwanachama wa chama cha wafanyakazi au kujihusisha na shughuli
halali za chama.
HAKI
ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
1.
Kuwa
na Katiba yake bila kuingiliwa na dola, chama cha siasa au muajiri.
2.
Kupanga
na kuendesha mambo yake ya ndani na shughuli halali bila kuingiliwa.
3.
Kujiunga
na kuunda shirikisho na kushiriki shughuli za shirikisho hilo.
4.
Kujiunga
na mashirikisho ya kimataifa, kuchangia na kupokea misaada ya kifedha kutoka
kwa vyama au mashirikisho hayo.
UTARATIBU
WA KUUNDA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini na.6 ya mwaka 2004, Chama cha Wafanyakazi kinaweza kuanzishwa
na wafanyakazi wasiopungua 20. Wafanyakazi hao wanapaswa kuitisha kikao cha
kuanzisha Chama, ambapo watajiorodhesha na kutia saini zao katika rejista ya
mahudhurio. Watamteua Katibu wa kikao ambaye atatayarisha muhtasari wa kikao
wenye azimio la kuanzisha chama.
MAMBO
YA KUZINGATIA WAKATI WA KUANZISHA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
1.
Chama
kiwe ni chama halisi cha Wafanyakazi (Bona fide Trade Union).
2.
Kisiwe
chama kwa madhumuni ya kupata au kutengeneza faida (Association not for Gain).
3.
Kiwe
ni chama huru, kwa maana kwamba kisianzishwe na muajiri au waajiri au serikali.
4.
Kianzishwe
na wafanyakazi wasiopungua 20.
5.
Kiwe
na katiba na kanuni zinazozingatia kifungu cha 47 cha Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini na.6 ya 2004.
6.
Kiwe
na jina lisilofanana na jina la chama kingine, kuzuia mkanganyiko au
kuwapotosha watu.
7.
Kiwe
na makao yake makuu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
UTARATIBU
WA KUSAJILI CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Chama cha Wafanyakazi kinapaswa
kusajiliwa ndani ya miezi sita (6) kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwake. Maombi
ya usajili yatafanyika kwa kujaza fomu maalum ambayo itajazwa kikamilifu na
kusainiwa na katibu wa kikao kilichoanzisha chama hicho.
Fomu hiyo ya maombi inapaswa kuambatana
na nakala zilizothibitishwa za rejista ya mahudhurio, na nakala
zilizothibitishwa za katiba na kanuni, na kuziwasilisha kwa msajili wa Vyama
vya Wafanyakazi na waajiri.
MAJUKUMU
YA CHAMA KILICHOSAJILIWA.
Chama kilichosajiliwa kinapaswa
kuwasilisha kwa msajili kila ifikapo tarehe 31 Machi au kila mwaka taarifa
zifuatazo:-
a)
Taarifa
ya fedha zilizokaguliwa kwa kipindi cha fedha kinachoishia tarehe 31 Desemba ya
mwaka uliopita.
b)
Orodha
ya wanachama inayoonesha jumla ya wanachama kwa kipindi kinachoishia tarehe 31
Desemba ya mwaka uliopita.
c)
Majina
ya viongozi walioteuliwa au kuchaguliwa na anuani zao ndani ya siku 30 tangu
uteuzi au uchaguzi kufanyika.
d)
Mabadiliko
ya kanuni ndani ya siku 30 kuanzia siku ya mabadiliko hayo.
Chama pia kina jukumu la kutunza kwa
miaka isiyopungua mitano kumbukumbu zifuatazo:-
1.
Orodha
ya wanachama katika fomu maalumu.
2.
Mihtasari
ya Vikao.
3.
Karatasi
za kura.
Chama cha Wafanyakazi kinapaswa wakati
wote kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa katiba, kanuni na mazoea. Endapo
itatokea chama kimeshindwa kuzingatia katiba yake, msajili au wanachama
wanaweza kupeleka maombi mahakama ya kazi kutengua suala hilo lililofanyika
kinyume na katiba.
Kabla ya maombi hayo kupelekwa
mahakamani, taratibu za ndani ya chama ni lazima zifuatwe kwanza. Isipokuwa
ikiwa ni kwa maslahi ya chama, basi maombi hayo yanaweza kupelekwa mahakamani
bila kufuata utaratibu wa ndani wa chama.
HAKI
ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI MAHALI PA KAZI.
Chama cha Wafanyakazi kilichosajiliwa
kina haki zifuatazo mahali pa kazi:-
1.
Haki
ya kuingia eneo la muajiri – kwa lengo la kusajili wanachama, kuwasiliana na
wanachama, kufanya vikao na wanachama, kuendesha uchaguzi. (Kifungu cha 60 cha
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya mwaka 2004).
2.
Makato
ya Ada – kupokea ada za wanachama baada ya muajiri kuwakata kutoka kwenye
mishahara yao. (Kifungu cha 61 cha Sheria ya Ajira).
3.
Kuwa
na wawakilishi wake mahali pa kazi – chama cha wafanyakazi kinayo haki ya kuwa
na wawakilishi mahali pa kazi kwa kuzingatia idadi ya Wanachama kama
ifuatavyo:-
a)
Wanachama
wasiozidi tisa (9) – muwakilishi mmoja.
b)
Wanachama
kuanzia kumi (10) mpaka ishirini (20) – wawakilishi watatu.
c)
Wanachama
kuanzia ishirini na moja (21) mpaka mia moja (100) – wawakilishi kumi.
d)
Wanachama
zaidi ya mia moja (100) – wawakilishi kumi na tano, miongoni mwao watano lazima
wawe wanawake kama wapo na ni wanachama.
MAJUKUMU
YA WAWAKILISHI WA CHAMA MAHALI PA KAZI.
1.
Kuwawakilisha
wanachama kwenye vikao vya kushughulikia malalamiko na nidhamu.
2.
Kuwasilisha
hoja kwa niaba ya wanachama kuhusiana na kanuni, afya, usalama na ustawi wao.
3.
Kushauriana
na muajiri kuhusu tija mahali pa kazi.
4.
Kukiwakilisha
chama wakati wa ukaguzi na uchunguzi unaofanywa na wakaguzi kwa mujibu wa
sheria yoyote ya kazi.
5.
Kuhakikisha
kazi za chama kwa mujibu wa katiba ya chama.
6.
Kuendeleza
uhusiano mzuri kazini.
7.
Kutekeleza
majukumu waliokubaliana na muajiri.
Wawakilishi wa chama wanayohaki ya
kupewa muda wa kutosha kutekeleza majukumu yao bila kukatwa mshahara na wanayo
haki pia ya kupewa na muajiri taarifa zote muhimu zitakazowawezesha kutekeleza
majukumu yao kikamilifu. Haki hizi zitatolewa na kutekelezwa vizuri bila
kuvuruga kazi.
LIKIZO
KWA WAWAKILISHI WA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Wawakilishi wa chama mahali pa kazi
wanayo haki ya kupewa likizo ya malipo na muajiri kwa ajili ya kuhudhuria
mafunzo yanayohusiana na majukumu yao. Hali kadhalika viongozi wa chama cha
wafanyakazi na wa shirikisho ambalo chama ni mwanachama, wanayo haki ya kupata
likizo ya malipo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya chama au shirikisho.
UTARATIBU
WA KUPATA HAKI ZA CHAMA.
Chama cha Wafanyakazi kilichosajiliwa
kutekeleza haki za chama, kinapaswa kumtaarifu muajiri kwa kujaza fomu CMA F3
kikianisha haki ambazo kinataka kuzitekeleza pamoja na mahali pa kazi ambapo
kinataka kuzitekeleza haki hizo.
Muajiri akishapokea fomu hizo anapaswa
kukutana na chama ndani ya siku 30 ili kufikia makubalianao ya pamoja
yatakayotoa haki hizo, na kuweka utaratibu wa kuzitekeleza. Endapo hakutakuwepo
makubaliano au muajiri atashindwa kukutana na chama ndani ya muda uliowekwa,
chama kinaweza kupeleka mogogoro huo mbele ya Tume kwa ajili ya usuluhishi.
Usuluhishi ukishindikana chama kinaweza
kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi kwa uamuzi.
USITISHAJI
WA HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Haki za chama zinaweza kusitishwa iwapo
chama kitakiuka makubaliano ya msingi ya utoaji haki hizo au kwa amri ya
mahakama inayotoa haki hizo.
Ikitokea hali hiyo ya ukiukwaji wa
makubaliano, muajiri anaweza kupeleka mgogoro huo mbele ya Tume kwa ajili ya
usuluhishi. Usuluhishi ukishindikana, muajiri anaweza kupeleka mgogoro huo
Mahakama ya Kazi akiiomba Mahakama isitishe makubaliano ya kutoa haki hizo au
iondoe amri yake ya kutoa haki hizo
HITIMISHO.
Mara nyingi katika maeneo ya kazi
kumekuwa na migogoro mingi sana inayohusu masuala ya haki za vyama vya
wafanyakazi. Waajiri kwa kutokujua au kwa makusudi wamekuwa wakikataa kutoa
haki za chama kwa wafanyakazi wanachama wa vyama vya wafanyakazi. Hali hii
imekuwa ikipelekea kuibuka kwa migogoro hiyo ambayo huatarisha mahusiano mazuri
kati ya muajiri na wafanyakazi.
Mara nyingine wanachama wamekuwa
wakizitumia haki zao vibaya katika maeneo yao ya kazi, jambo ambalo pia
linamfanya muajiri kutoridhika na hali hiyo ambapo pia hupelekea migogoro ya
kikazi kuibuka.
Makala hii imelenga kutoa ufafanuzi na
uelewa juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Vyama vya Wafanyakazi na Haki
zilizomo kwa pande zote mbili (muajiri na wafanyakazi). Aidha imeainisha
majukumu ya chama na wanachama kwa ujumla.
Ni matumaini yangu kuwa itasaidia kutoa
uelewa kwa wadau wa sekta ya ajira, hasa waajiri na wafanyakazi na hivyo
kusaidia kupunguza migogoro ya kikazi na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya
wadau hao.
Imeandaliwa na Emmanuel C. Zongwe kwa
msaada wa vitabu mbalimbali, mitandao na uelewa binafsi katika masuala ya Ajira
na Mahusiano Mahala pa Kazi.
Simu: +255 (0) 717 058 045/ +255 (0)
755 223 697
E-mail: ezongwe@yahoo.com
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza.