Na
Emmanuel C. Zongwe
Mtaalamu
wa Masuala ya Mahusiano Mahali pa Kazi.
____________________________________________
Makala inayohusiana: AJIRA: USITISHWAJI WA AJIRA KWA SABABUYA UTOVU WA NIDHAMU MAHALA PA KAZI.
Picha na www.gradientpixels.ca |
UTANGULIZI
Kuachisha kazi kwa ujumla
maana yake ni kumalizika/kuvunjika kwa mkataba wa ajira kati ya muajiri na
muajiriwa. Kwa maneno mengine, ni kumalizika kwa mahusiano ya kiajira kati ya
muajiri na muajiriwa. Kusitishwa kwa mahusiano hayo kunaweza kuanzishwa na
upande wowote wa mkataba huo (muajiri au muajiriwa).
Katika Kanuni za Ajira na
Mahusiano Kazini (Kanuni za Utendaji Bora) za mwaka 2007, imeelezwa kuwa
kuachishwa kazi kazi itakuwa ni apamoja na:-
a) Kuachisha
kazi chini ya Sheria ya Kimila ya Uingereza (Common Law).
b) Muajiri
kusababisha ugumu kwa muajiriwa kuendelea na ajira.
c) Kushindwa
kuongeza mkataba wa muda maalum kwa masharti yaleyale au yanayofanana kama
kulikuwa na matumaini ya kuongeza mkataba.
d) Kushindwa
kumruhusu mfanyakazi kurejea kazini baada ya likizo ya uzazi au ulezi.
e) Kushindwa
kumuajiri tena mfanyakazi pale ambapo muajiri amewaachisha kazi wafanyakazi
kadhaa kwa sababu kama hiyo au zinazofanana na ametoa nafasi z ajira kwa baadhi
ya wafanyakazi walioachishwa kazi tu.
KUACHISHA KAZI KIHALALI
Katika Sheria ya Kimila ya
Uingereza (Common Law), kuachisha kazi kihalali kumeelezwa kuwa ni pamoja na :-
i.
Kuachisha kazi kwa makubaliano – hapa ni pale
ambapo muajiri na muajiriwa wanakuwa wamekubaliana kusitisha mahusiano yao ya
kiajira. Kwa mfano; kama mkataba wa ajira ni wa mwaka mmoja na muda huo
umekwisha, hapo mkataba huo utakuwa umefikia ukomo.
ii.
Ajira kukoma yenyewe – hapa ni pale ambapo
mkataba wa ajira unakuwa umesitishwa katika mazingira kama kifo au kumalizika
kwa shughuli ya muajiri.
iii.
Kuachishwa kazi kunakofanywa na muajiri –
muajiri pia anaweza kusitisha mkataba wa ajira lakini itampasa kwanza
kuzingatia na kufuata taratibu za kisheria.
Ø Katika
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na. 6 ya mwaka 2004 kumetajwa vigezo vine
ambavyo vinahalalisha uachishaji kazi unaofanywa na muajiri. Vigezo hivyo ni
pamoja na:-
a)
Mwenendo mbaya (misconduct)
b)
Kutokuwa na uwezo (incapacity)
c)
Kutohitajika (incompatibility)
d) Mahitaji
ya kiuendeshaji (operational requirement)
iv.
Ukatishwaji wa ajira unaofanywa na muajiriwa
– hapa ni pale ambapo mfanyakazi analazimika kuacha kazi baada ya muajiri
kuvunja mkataba wa ajira baina yake na muajiriwa.
Ø Katika
Kanuni za Ajira na Mahusiano Kazini (Kanuni za Utendaji Bora) za mwaka 2007,
Kanuni ya 7 (1) inasema kuwa, “… pale ambapo muajiri anafanya ajira kushindwa
kuvumilika, ambapo inaweza kusababisha muajiriwa ajiuzulu, kujiuzulu huko
kutakuwa sawa na kuacha kazi kwa kulazimika.”
Sheria ya Ajira na Mahusiano
Kazini na Kanuni zake, pia imeeleza kuwa ili kuachisha kazi kuwe ni halali basi
ni lazima kuwe na sababu halali na ya haki (valid and fair reason) na utaratibu
wa haki (fair procedure) uwe umefuatwa. Muajiri anapaswa kuwa na sababu halali
na awe amefuata utaratibu wa haki katika kumuachisha kazi muajiriwa.
Taratibu za kuachisha kazi
zinatofautiana kulingana na sababu inayopelekea kuachisha kazi, lakini taratibu
zote hizo ni lazima zimpe muajiriwa nafasi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wa
kumuachisha kazi. Bila kujali uzito wa kosa lililofanywa na muajiriwa, bila
kujali kuwa muajiri wake ana ushahidi wa kutosha, ni lazima kisheria kufuata
taratibu za kumuachisha kazi kama zilivyoelezwa katika Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini na. 6 ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2007.
Kushindwa kufuata taratibu
hizo kutamaanisha muajiriwa ameachishwa kazi bila kupewa nafasi ya kujitetea
(summary dismissal). Kutokumpa muajiriwa nafasi ya kujitetea au kujieleza ni
kumnyima haki yake ya kisheria. Kwa mujibu wa Sheria za kazi, kuachisha kazi
kwa namna hii ni sawa na kuachisha kazi kusivyo halali (unfair termination).
Endapo itathibitika kuwa
kuachisha kazi kulikofanywa na muajiri si halali inaweza kuamuriwa kuwa muajiri
atekeleze moja ya mambo yafuatayo kwa mfanyakazi/muajiriwa husika.
1. Kumrudisha
muajiriwa kazini (reinstatement) – hapa muajiriwa atarudishwa kazini na
itahesabika alikuwepo kazini kutokea siku alipoachishwa kazi na atastahili
kulipwa stahiki zake alizostahili kulipwa kwa kipindi chote tangu kuachishwa
kwake. Pale ambapo amri ya kumrudisha muajiriwa kazini imetolewa na muajiri
ameshindwa kutekeleza amri hiyo, atapaswa kumlipa mfanyakazi huyo fidia ya
mishahara ya miezi isiyopungua kumi na mbili (12) na stahiki nyingine
alizostahili kulipwa tangu kuachishwa kwake.
2. Kumuajiri
upya mfanyakazi kwa masharti mapya yatakayoamuliwa na Tume ya Usuluhishi na
Uamuzi au Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi (Labour Court). Endapo muajiri
atashindwa kutekeleza amri hii, atalazimika kulipa fidia ya mishahara ya miezi
isiyopungua kumi na mbili pamoja na stahiki nyingine ambazo muajiriwa
alistahili kulipwa tangu siku aliyoachishwa kazi isivyo halali.
3. Kumlipa
mfanyakazi fidia ya mshahara wa miezi isiyopungua kumi na mbili. Pamoja na fidia
hiyo, pia atalazimika kumlipa stahiki zake nyingine anazostahili kulipwa kwa
mujibu wa Sheria yoyote ile au makubaliano yoyote yaliyokuwepo kati ya muajiri
na muajiriwa.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza