-->
Picha na dailyjobads.com |
Usitishaji wa ajira ni kukoma kwa ajira (mkataba wa ajira) kunakosababishwa
na mambo mbalimbali kama; mfanyakazi kujiuzulu (kuacha kazi kwa hiari), muajiri
kusababisha mazingira magumu kwa muajiriwa kuendelea na kazi, muajiri kushindwa
kumruhusu muajiriwa kurudi kazini baada ya likizo (ya uzazi au ya mwaka) na
mfanyakazi kuachishwa kazi kwa utovu wa nidhamu.
Utovu
wa nidhamu ni sababu kubwa inayoweza kupelekea kusitisha ajira. Hata hivyo
muajiri hapaswi kuchukua hatua zozote za kinidhamu dhidi ya muajiriwa mpaka
pale atakapokutana naye kwanza na kujadili suala hilo. Pia katika Kanuni za
Utendaji Bora Mahala pa Kazi za mwaka 2007 imeelezwa wazi kuwa muajiri anapaswa
kuweka kanuni za kusimamia nidhamu zinazoeleza namna mfanyakazi anavyopaswa
kuzingatia nidhamu mahali pa kazi. Muajiri anapaswa kuwafahamisha wafanyakazi
kanuni hizo wakati wa kuajiri.
Kama
hiyo haitoshi, Kanuni hizo pia zimetoa muongozo/utaratibu wa kusitisha ajira
kwa sababu ya utovu wa nidhamu. Kabla ya kumuachisha kazi mfanyakazi, muajiri
anatakiwa kufikiria kwa umakini na kuzingatia mambo yafuatayo:-
i.
Je,
mfanyakazi amekiuka kanuni za nidhamu za kampuni/ taasisi?
ii.
Je,
kanuni iliyokiukwa ni ya msingi na haki?
iii. Je,
kanuni iliyokiukwa inaeleweka kwa mfanyakazi na haina utata? Na
iv.
Je,
kanuni iliyokiukwa imekuwa ikitumika na muajiri kwa usawa?
Katika
Kanuni za Utendaji Bora Mahala pa Kazi za mwaka 2007, Kanuni ya 12 (2)
imeelezwa kuwa kosa la kwanza la mfanyakazi halihalalishi adhabu ya kuachisha
kazi isipokuwa pale itakapothibitika kuwa kosa ni kubwa kiasi cha kuharibu
uhusiano wa kiajira kiasi cha kutovumilika. Pia katika Kanuni ya 12 (3)
yametajwa makosa makubwa yanayoweza kuhalalisha mfanyakazi kuachishwa kazi kwa
kosa la kwanza. Makosa hayo yametajwa kuwa ni pamoja na:-
a) Kukosa uaminifu kulikokithiri
b) Kuharibu mali kwa makusudi
c) Uzembe uliokithiri
d) Kuhatarisha usalama wa watu wengine kwa
kukusudia
e) Kushambulia wafanyakazi wengine, wateja
au mtu mwingine yeyote mwenye kuhusiana na muajiri
f) Ukaidi uliokithiri.
Pamoja
na muajiri kuweza kumuachisha kazi mfanyakazi mara moja kutokana na makosa
yaliyoainishwa hapo juu, Kanuni zimeweka utaratibu wa haki ambao muajiri
anapaswa kuufuata kabla ya kuchukua hatua za kinidhamu juu ya mfanyakazi anayetuhumiwa
kwa kosa la kinidhamu.
Kabla
ya kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mfanyakazi mtuhumiwa, muajiri
anatakiwa kufanya uchunguzi ili kubaini iwapo kuna haja ya kuitisha kikao cha
nidhamu. Muajiri atakapobaini kuwa ipo haja ya kuitisha kikao cha nidhamu
atapaswa kufanya mambo yafuatayo:-
i.
Kutoa
kwa mfanyakazi taarifa ya tuhuma kwa namna ambayo mfanyakazi ataelewa tuhuma
hizo.
ii.
Kumpa
mfanyakazi muda usiopungua saa 48 ili aweze kuandaa utetezi wake.
iii.
Kumueleza
mfanyakazi haki yake ya kuwasilishwa na mfanyakazi mwenzake au kiongozi wa
chama katika kikao cha nidhamu.
iv.
Kuteua
mwenyekiti wa kikao hicho ambaye hajahusika na tatizo lililopelekea kuitishwa
kwa kikao cha nidhamu.
v.
Kumpa
mfanyakazi nafasi ya kuwahoji mashahidi wa muajiri na ikibidi kuleta mashahidi
wake.
vi.
Kikao
kitakapothibitisha tuhuma dhidi ya mfanyakazi mtuhumiwa, muajiri atoe nafasi
kwa mfanyakazi kueleza hoja ya kupunguziwa adhabu.
vii.
Kutoa
nafasi kwa mtendaji wa chama kuwakilisha katika kikao hicho endapo mfanyakazi
mtuhumiwa ni kiongozi au muwakilishi wa chama mahali pa kazi.
viii.
Endapo
adhabu inayokusudiwa ni kuachisha kazi, muajiri ni lazima aeleze sababu na pia
aeleze haki ya mfanyakazi kukata rufaa.
ix.
Kumpa
mfanyakazi nakala ya fomu ya kusikilizia shauri la kinidhamu baada ya kikao.
Pamoja
na uwepo wa taratibu hizi, mara kwa mara waajiri wamejikuta wakiingia kwenye
migogoro ya kiajira dhidi ya wafanyakazi kwa kuzikiuka.
Sheria
ya Ajira na Mahusiano Kazini na. 6 ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2007
imeweka utaratibu huu ili kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la waajiri
kusitisha ajira au kuachisha kazi wafanyakazi kwa makosa ya kubambikiwa, lakini
pia kumfanya mfanyakazi azingatie suala la nidhamu mahali pa kazi.
Imeandaliwa na Emmanuel C. Zongwe kwa msaada wa vitabu vya sheria na machapisho
mbalimbali.
Emmanuel
C. Zongwe ni msomi na mtaalamu wa masuala ya Ajira
na Mahusiano Mahali pa Kazi. Pia ni Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa
Mashambani na Kilimo (TPAWU), Wilaya ya Mufindi, Iringa.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza.
Nashukuru kwa kulijua hilo...
JibuFuta