Wazazi wengi nchini
na jamii nyingine wanapenda kuwaona watoto wao wakiwa kama wao walivyokuwa enzi
hizo.Kwa maana nyingine wanataka kuwaona watoto wao wakiwa kama nakala zao.
___________
Watoto wa umri kati
ya miaka 3-12(ni umri kabla ya kuanza shule na kuanza shule) huonyesha tabia za
kutaka kufanya vitu wenyewe bila kuzuiliwa na mtu yeyote.
Hupenda kujifunza
lugha, na ishara mbalimbali kwa kasi isiyo ya kawaida. Hapa wazazi wengi
huwachukulia watoto wao kuwa ni watundu na wasumbufu,la hasha! Ni umri wao
kutaka kujifunza kuhusu mambo yanayowazunguka.
Kama
mwanasaikolojia, Maria Montessori alivyoainisha kuhusu makuzi ya watoto,
anasema kuwa watoto wa rika hili hupenda kuwa na urafiki na watoto wa
rika lao.
Pia kuhusu
kuwaruhusu watoto wafanye vitu wanavyoweza kufanya na si kulazimisha
kuwasaidia.Alisema, "Never help a child
with a task at which he feels he can succeed." Yaani “Usimsaidie mtoto
kufanya kazi iliyo kwenye uwezo wake.”
Kiuhalisia makuzi ya
watoto hutegemea sana mazingira, mfano mtoto aliyekulia mazingira ya shida na
duni kiuchumi anatofautiana sana kiutendaji na yule aliyetokea mazingira ya
raha na furaha na uchumi mzuri.
Tofauti hii ambayo
inahusisha saikolojia ya makuzi ya mtoto, ina uwezo mkubwa sana wa kushusha au
kuongeza/kuimarisha utendaji wa mtoto afikiapo utu uzima.
Nitazungumzia
tofauti za watoto katika mazingira hayo mawili katika makala nyingine.Leo
napenda uungane nami katika kuyajua madhara (8) ya kumzuia mtoto wako kushiriki
michezo ya kawaida na wenzake...
Mwanasaikolojia
maarufu duniani Erick Erickson 1956 aliainisha hatua nane(8) za maendeleo ya
makuzi ya binadamu kijamii na kihisia kuanzia kuzaliwa hadi utu
uzima.Alisisitiza kuwa kila hatua ina vipingamizi vyake ni muhimu kupitia kila
hatua na kuondoa vipingamizi hivyo kabla ya kwenda hatua nyingine.
Nitapenda kujikita
hasa kwenye makuzi ya watoto ambayo yana mchango mkubwa kwa utu uzima wa
mtu.Nikizingatia hatua mbili za makuzi ya mtoto yaani hatua ya 2 na hatua ya 3
za maendeleo ya ukuaji wa mtoto kama alivyozielezea Erickson;
Katika hatua ya pili
(2) umri wa mtoto kabla ya kuanza shule (chekechea), aliangalia mambo mawili
yanayopingana yaani “Kujifunza mwenyewe Vs
Aibu (miaka 3-4)”.Akimaanisha kuwa mtoto wa umri huu hupenda kufanya mambo
mwenyewe na hujisikia aibu pale anapokatazwa kwa kuambiwa “Usi…” Mtoto
aliyekuzwa vizuri hujisikia vizuri bila kuwa na aibu yoyote.
Pia katika hatua ya
tatu (3) umri wa kuanza shule (baada ya chekechea), umri wa michezo, mtoto
hupambana na vitu viwili yanayopingana yaani Kujianzishia
kujifunza Vs Kujilaumu/Hatia.(miaka 4-12). Akimaanisha kuwa mtoto
aliyekuzwa vizuri kwa kupewa uhuru wa kujifunza (1) hujiona fahari kuwa na
wenzake,(2) hupenda kushirikiana na wenzake, (3) hupenda kuongoza pia
kuongozwa.
Kwa upande mwingine,
mtoto aliyekuzwa mazingira ya kubanwa hujihisi kuwa na hatia hivyo (1) huwa
muoga (2) hujitenga na wenzake (3) anakuwa tegemezi sana kwa wazazi (4) anakuwa
amekosa mbinu za michezo na uwezo wa ubunifu.
Nitayajumuisha
madhara (8) ayapatayo mtoto wako kwa kukosa kushiriki michezo ya kitoto na
wenzake kama ifuatavyo;
___________________
1.Mtoto kukosa uwezo
wa kujiamini mbele ya hadhara
Ukifuatilia michezo
ya watoto kama mpira,kukimbizana, na mingine mingi utagundua kuwa watoto ni
waongeaji na watendaji hasa wakiwa na watoto wa rika lao.
Endapo mtoto wako
atakosa fursa ya kukutana na wenzake, kwanza atakuwa na hofu-kwasababu
hajawazoea, pili atajihisi mnyonge mbele ya wenzake.Hivyo kuanza kuijenga tabia
ya kutokujiamini tangu utotoni.
2.Kukosa uwezo wa
kuongoza
Kutokana na hofu
aliyojingea tangu utotoni, ni dhahiri kuwa atakuwa hana mbinu za kuwasiliana
kama kiongozi, pia atakuwa na aibu iliyopitiliza mbele ya watu anaotakiwa
kuwaongoza.
3.Kuwa mtegemezi wa
maamuzi mbali mbali kwa wazazi hata yaliyo kwenye uwezo wake
Tatizo hili ni
kubwa, limepelekea vijana wengi kushindwa kuamua mambo yao wenyewe, eti “labla
nimuulize baba na mama”, kazi lazima achaguliwe na wazazi/walezi.
Hili ni tatizo
lililokuwa tangu utotoni, yaani kukosa uwezo wa kuamua kufanya hasa baada ya
kuambiwa “Usi…” na kutopata nafasi ya kuona watoto wengine wakijaribu kufanya
jambo fulani.
4.Mtoto
hujitenga na jamii
Kwa kuwa mzazi au
mlezi ulimtenga mtoto na jamii kwa kumfungia ndani wakati wote, na kumwachia
mtoto wako awe na urafiki mkubwa na Televisheni na michezo yake pekee,
usitegemee kuona mtoto wako akiwa mbali na jamii hasa afikapo ujana na hata utu
uzima.
5.Kukosa uwezo na
mbinu za kuwasiliana
Kama nilivyoeleza
awali, watoto wa umri huu hupenda kujifunza lugha na ishara mbali mbali za
mawasiliano wakiwa na watoto wa rika lao.
Hivyo basi, kama
utamfungia mtoto wakati wote asikutane na wenzake, tambua kuwa unamwandaa mtoto
ambaye atakuwa hana uwezo mzuri kimawasiliano.Ujuzi huu ni muhimu sana katika
shughuli mbali mbali za kijamii.
6.Kuwa na viungo
dhaifu na kukosa uchangamfu wa mwili
Itafahamika kuwa
uimara wa viungo vya mtoto haujengwi na vyakula pekee, bali mazoezi ya viungo
hasa kwa michezo ya kitoto ya kukimbizana hapa na pale.
Kisaikolojia, mtoto
huathirika sana anapoona watoto wengine wakicheza kwa furaha wakati yeye
anazuiliwa ama kwa kupigwa na kukaripiwa.Hii humfanya mtoto kunyongea na kukosa
uchangamfu.
7.Humpelekea mtoto
kujitengenezea tabia ya kutoroka ili atimize hisia zake
Hapa ndipo utukutu na
tabia mbaya zinapoanzia.Mtoto anaamua kujitengenezea mbinu ili aweze kushiriki
kwenye michezo ya kitoto.
Mtoto anapofikia
hatua hii, wazazi wengi hulaumu sana kuwa watoto wa siku hizi hawatulii, wakiwa
wamesahau kuwa wenyewe ndiyo chanzo cha kuwafanya watoto watoroke kwasababu ya
ulinzi mkali nyumbani.
Mtoto hawezi
kutoroka nyumbani kama anapata upendo na kueleweshwa mema na mabaya kwa
vitendo, pia kwa kumpa na kukubaliana utaratibu wa michezo.
8.Mtoto kukosa
ubunifu wenye tija ya kupambana na changamoto za maisha
Ubunifu wa mtoto
unachangiwa na kuwepo kwa ushirikiano wake na watoto wenzake.Ni hapo kipaji cha
mtoto kinapojidhirisha. Kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na
teknolojia, wazazi wengi wamewaachia watoto wao kutazama televisheni na komputa
na si kwenda kucheza na watoto wengine.
Naomba nitoe rai kwa
wazazi wa karne hii ambao mnakumbana na changamoto mbali mbali za mabadiliko ya
Sayansi na Teknolojia kiasi kwamba mnakuwa hamna muda wa kukaa na watoto, ila
ni kutoa amri kuwa hairuhusiwi mtoto kutoka nje.
Pia ni vizuri kufuatilia
kila hatua ya ukuaji wa mtoto na kuhakikisha yale mahitaji ya hatua husika
yanafikiwa, kinyume na hapo tusishangae kuona watoto wetu wamekuwa vile
tusivyotarajia.
Ungana na makala
yangu nyingine kuhusu "Sababu zinazoweza kumfanya mtoto wako
kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya akiwa katika umri mdogo."
Makala hii
imeandikwa na Henry Kazula, ikiwa ni utafiti wake binafsi ukisaidiwa na
nadharia kutoka tovuti zifuatazo:
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!
Kwa udhamini wa...........................(bofya hapa kuwa mdhamini na ujitangaze zaidi).
Kwa udhamini wa...........................(bofya hapa kuwa mdhamini na ujitangaze zaidi).
Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFutaPendekeza tovuti hii www.letspal.com
JibuFuta