inspire

inspire

Lebo

AFYA (8) AJIRA (5) BIASHARA (39) ELIMU (14) MAHUSIANO (2) MALEZI (16) MAZINGIRA (12) SAIKOLOJIA (48) VIJANA (7)

Business registration

Green Consulting

business consultancy

business consultancy

Business consulting-2

Business consulting-2

Professional Consulting

PDC

Swahili translator

Swahili translator

TANGAZO-KITABU

E-BOOK: MTAZAMO WAKO NI UPI?

TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- .... TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- ....

TANGAZO TUWEZESHANE

TANGAZO TUWEZESHANE

DARDY'S INVST-20/10/2017

DUNIA IKUONE

DUNIA IKUONE

Jumatano, 24 Desemba 2014

TAMBUA KUWA WENGINE PIA WANA SHIDA ZAO…


Naandika makala hii nikiburudika na muziki pia maneno ya msingi kutoka moja ya mstari wa wimbo-“Sugua gaga” wa mwanamuziki maarufu wa “bongo flava” nchini Tanzania- Sara Kaisi almaarufu “Shaa”. Katika mstari huo anasema; “…kama una shida unamwambia nani? hata mimi za kwangu nimeacha nyumbani” akimaanisha kila mtu ana shida zake.Ama kwa hakika wasanii wa nchini Tanzania wanajitahidi kwa ubunifu katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii kupitia muziki, huyu ni miongoni mwa wasanii walionukuliwa katika KITABU chetu kitakachotoka mapema mwaka 2015.Wasanii wengine utakuwa umeona tulivyowanukuu na kuendelea kuwanukuu katika makala zetu kutokana na sehemu za mashairi yao yenye kukonga nyoyo na kufikisha ujumbe mahsusi kwa jamii.
Sasa turudi kwenye mada iliyopo mezani, wengine wana shida zao. Katika maisha ya kila siku iendayo kwa Mungu, kila mtu hupatwa na maswahibu au shida mbali mbali. Watu hutofautiana sana katika ujasiri na uvumilivu wa shida mbali mbali. 
Watu wengine ni wavumilivu sana kukumbatia shida zao na kupambana kwa njia moja au nyingine kupata suluhisho. Wapo makini sana kutoa shida zao kwa wengine. Huamini kuwa unapotoa shida yako kwa kila mtu ni kujidhalilisha na kujishusha thamani, hivyo basi huamua “kufa na tai shingoni” kuhusiana na shida zao.
Pia wapo wengine walio waoga sana kwa shida-wakiamini kuwa ni wao pekee duniani wenye shida. Kundi hili halitulii kukaa na shida, hivyo humweleza kila mtu wanayemfahamu shida zao. Bila kuchagua aina ya watu wa kuwaeleza shida zao; imewapelekea kukosa msaada na mwisho wa siku kuishia kutangazwa na kukimbiwa mara wawapo na shida. Hii imetokana na wao kuwa wavivu wa kuwajibika katika kutatua shida zao na kuwa tegemezi kwa wengine kupita kiasi.
Ndugu msomaji, nimeamua kuainisha makundi hayo mawili kwa kuzingatia uwezo wa kila kundi kuhimili na kustahimili shida ili iwe rahisi kwako kujichagulia kundi ulipendalo au kujiimarisha katika kundi husika kwa manufaa ya maisha yako. Suala la msingi la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa shida uliyonayo haiwasumbui wengine. Pia kujitafutia watu au mtu sahihi ambaye mtakuwa mkisaidiana.
Sitarajii kueleweka vibaya kuwa nahamasisha watu wasisaidie wenye shida, hapana! Nafanya hivyo kwa mapenzi mema ili kuhamasisha uwajibikaji wa kila mwanajamii katika kujiinua kimaisha na si kuwa tegemezi kupita kiasi. Fuatilia zaidi KITABU chetu kitakachohamasisha badiliko la kimtazamo na uwajibikaji ulio na uhusiano wa machaguo mbali mbali ya maisha bila kuwakwaza au kuwatwisha wengine majukumu.
Imetolewa na 
Jielimishe Kwanza!

Jumatatu, 22 Desemba 2014

MUENDELEZO: UTAMADUNI WA KUHOJI KWANINI...


Katika kujiuliza maswali ya msingi ni vyema kuanza na “kwa nini”, nawe waweza kuniuliza “kwa nini” tuanze na “kwa nini”? Naweza kutoa sababu za kufanya hivyo na kukuhamasisha kujijengea utamaduni huo kama ifuatavyo;
1.   Kuanza na “kwanini” katika lugha ya Biashara: Utajua sababu ya wewe kutoa maamuzi na kuwaaminisha wengine kuamini unavyo amini. Simon Sinek ananisaidia kutoa sababu ya kuanza na “kwanini” katika kufikisha ujumbe wa kibiashara kwa wateja- nanukuu; People don't buy what you do; people buy why you do it”. Katika tafsiri ya lugha ya Kiswahili isiyo rasmi -“watu hawanunui nini unafanya, ila hununua kwa nini unafanya ufanyavyo.
2.   Kuanza na “kwanini” katika kutoa maamuzi sahihi na yenye tija
Mambo mbali mbali hujitokeza katika maisha yetu na hutulazimu kutoa maamuzi pia kututoa njia panda. Tukihoji kwa kutumia neno hilo “kwa nini”, tunachochea udadisi ulio na kiu ya kutaka kujua zaidi ni kwa njia zipi tukio fulani limetokea na kutoa maamuzi sahihi.
Neno hilo huonekana kuwa ni dogo lakini nguvu yake ni kubwa kwa kubadilisha mfumo wa kawaida wa utendaji-“status quo” na ufikiri wa maisha yetu unaoendena na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Hivyo basi, ni vyema kujianzishia utamaduni huu kwa sababu utakubadilisha kimtazamo kwa vile unavyojichukulia katika maisha na kuboresha uthamani wa bidhaa na huduma (kwa mfanya biashara) na kutoa majibu sahihi ya maswali na changamoto za maisha ya kila siku.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!

Jumanne, 16 Desemba 2014

MUENDELEZO:FANYA HIVI KUEPUKANA NA UTUMWA WA KISASA KATIKA MAENEO RASMI YA KAZI…



1.Boresha ujuzi wako wa kazi kwa kujiendeleza kwa siri ukilenga kuwa mfanyakazi makini mwenye mbinu stahiki za kazi. Kwa hatua hii utajiongezea uthamani sana katika eneo lako la kazi. Itafika wakati utamfanya mwajiri akuone ni wa thamani hivyo atajitajihidi asikupoteze. Ikifika hatua hii: Unaweza kujipangia aina ya mshahara kulingana na ubora ndani ya ajira husika.
2.Usionyeshe udhaifu wako kwa mwajiri. Usionyeshe kuwa unabembeleza sana ajira yake, ukifanya hivyo ni rahisi sana kutumikishwa kama mtumwa kwa sababu umeonyesha una dhiki.
3.Onyesha uwezo au kipaji chako kwa kadri uwezavyo. Kama unakumbuka, moja ya athari za utumwa wa kisasa ni kushindwa kuonyesha kipaji chako…hakuna mazingira rafiki ya utendaji kazi! Tumia kila mbinu kuhakikisha kipaji chako na uwezo wako wa kipekee unaonekana katika mazingira ya kazi. Ukifanikiwa, unganisha na mbinu namba 1 kujiongezea ubora zaidi katika kazi.
4.Acha kunung’unika chini chini! tenda, onyesha hisia zako kwa vitendo ukihitaji kuona mazingira rafiki ya kazi.Mweleze mwajiri wako kuwa hujapendezwa na mazingira yanayoendelea katika kazi.Wafanyakazi wengi wamekuwa ni waoga kuwaeleza waajiri wao yao ya moyoni kuhusu ujira waupato ukilinganisha na utendaji…wengi hawaridhiki na vipato vyao, wananung’unika chini kwa chini.Ondoa hofu! Ni wajibu na haki yako kujadiliana na mwajiri kuhusu ujira ili kuboresha utendaji kazi.
5.Ungana na kikundi cha wapinga “utumwa wa kisasa” katika maeneo ya kazi. Sauti ya wengi ina nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko.
6.Tambua wajibu wako kwa kuhitaji “mpango wa kazi na majukumu kimaandishi” kutoka kwa mwajiri. Hakikisha unajiridhisha mapema kabla ya kuanza kazi. Majukumu uliyopewa yaendane na ujuzi ulio nao, pia yazingatie kipato unachopata.
7.Jielimishe zaidi kuhusu ajira na kanuni zake, haki za wafanyakazi kupitia vyombo mbali mbali vya habari.
8.Usifanye kazi kwa mazoea. Jitahidi kuwa mtu wa mabadiliko ukijiongezea uthamani katika soko la ajira.
Tukutakie kila la heri katika kujikomboa na utumwa wa kisasa katika maeneo rasmi ya kazi.
Imetolewa na 
Jielimishe Kwanza!

Jumatatu, 15 Desemba 2014

UTAMADUNI WA KUHOJI KWANINI…


Picha: alexrister1.wordpress.com
Neno “kwanini” au "why" kwa lugha ya Kiingereza ni la udadisi na uvumbuzi pia ni neno la kutaka kujua kulikoni. Hutusaidia pia kuweza “kujua ukweli wa mambo”-Kujielimisha! Hivyo kuweza kujua maana halisi ya mambo yanayotokea, yanayoendelea na mwisho kutoa maamuzi yaliyo sahihi kwa asilimia kubwa. Pia ni neno la msingi Kibiashara hasa wakati wa kuwasilisha bidhaa au huduma kwa wateja katika lugha igusayo hisia na kuteka soko la biashara.
Kwa bahati mbaya, nasikitika kusema kuwa ni mara chache tumekuwa na utamaduni wa kutumia neno hilo la msingi katika maisha yetu ya kila siku. Hii ni kwa sababu tunavutika haraka na neno “nini” -“what”, yaani tunavutika haraka na mambo yanayotokea na kuonekana, hivyo kuyafanyia kazi haraka bila kujua ni “kwanini” yametokea au yapo kama yaliyo.
Kwa bahati nzuri, maktaba yangu kuna kitabu nilichowahi kukisoma bila kuchoka, kinahamasisha kuendelea kusoma mara kwa mara; ni cha mwandishi, mhamasishaji na msemaji wa hadhara Simon Sinek kiitwacho-“Start With Why”-“Anza na Kwanini” kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi. Nakushauri kitafute kitabu hicho usome, utajua ni “kwanini” kuanza na “kwanini” kuna faida katika kuwasiliana kibiashara, kutoa maamuzi sahihi ya maisha yetu na kujua ukweli wa mambo.
Ndani ya kitabu hicho, Sinek anasisitiza juu ya kuanza kwa kujiuliza “kwanini” katika kutoa maamuzi ya kibiashara na maisha kwa ujumla. Ameanisha hivyo kwa kutumia duara liitwalo “The Golden cycle” lenye maneno “why”, “how” na “what” yaani “kwanini”, “kwa jinsi gani” na “ nini”.
Katika kujiuliza maswali ya msingi ni vyema kuanza na “kwa nini”, nawe waweza kuniuliza “kwa nini” tuanze na “kwa nini”?  TUKUTANE SIKU KAMA YA LEO UTAZIJUA SABABU HIZO KWA KINA.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!