Wanafunzi wengi kuanzia darasa la tano hadi kuelekea sekondari huwa
katika umri wa kubarehe (wavulana) na kuvunja ungo (wasichana) ambao huwa na
changamoto nyingi zinazoweza kupelekea kushuka kwa taaluma zao kama
hawatajitambua.
Hii ni hatua kubwa katika makuzi na maendeleo ya kijana inaanzia umri wa
miaka 12-18.Mwanasaikolojia Erick Erickson aliainisha bayana kuwa
katika kila hatua ya makuzi na maendeleo ya mwanadamu kuna changamoto, na kila
changamoto inapaswa kupitiwa na kushinda. Hivyo katika makuzi na maendeleo ya
mwanadamu hupambana na vikwazo hivi ili kufanikiwa kuendelea hatua nyingine kwa
mafanikio.
Kama nilivyosema awali, wanafunzi wengi huwa katika umri wenye
mabadiliko makubwa ya ujinsia ambayo huendana sana na kutamani kujihusisha na
tendo la ndoa.
Ni katika hatua hii wanafunzi na vijana wa umri huu hujiamini na kuona
wanaweza kufanya lolote hapa duniani.Tukumbuke kuwa huu ni wakati wao muhimu
kujifunza na kuandaa maisha yao wenyewe, ila wanakuwa wanapambana na hali ya
matamanio ya mwili.
Ili kufanikiwa katika masomo ni vyema waweze kushindana na kupambana na
hali hii ya matamanio ambayo kama mwanafunzi au kijana hatakuwa makini basi
huweza kuharibikiwa kiafya na kiakili.Hatari kubwa kuliko ni kuweza kupata
magonjwa ya zinaa na UKIMWI, na ujauzito katika umri mdogo bila kutarajia, pia
kupoteza uelekeo wa maisha.
Vijana wanapaswa kujitambua kuwa hiki ni kipindi cha mpito, hivyo ni
vizuri kuwa makini ili waweze kutimiza malengo yao katika maisha.
____________________
Mwanafunzi au kijana aweza kukishinda kipindi hiki cha makuzi kwa
kuzingatia yafuatayo:
1. SHIRIKI KATIKA IBADA MARA KWA MARA
Kumjua Muumba wako hasa kwa kupitia neno lake utajifunza njia nzuri ya
kuishi na jamii, pia kujitambua. Utajifunza kufuata sheria zilizopo kwenye
maandiko zikiwa kama mwongozo wa maisha na malengo yako.
2.EPUKA KUANGALIA PICHA ZINAZOCHOCHEA
NGONO
Katika mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, mambo mengi
yamerahisishwa kwa faida na hasara.Picha zinazochochea ngono zipo nje nje
kupitia sinema, mikanda ya video na intaneti.
Ningependa kukushauri mwanafunzi na kijana, tumia teknolojia kwa
faida ikiwa ni kutafuta masuala yanayoendana na masomo na kutafuta pesa kwa
njia halali.
3.JIWEKE MBALI NA MAKUNDI YENYE TABIA MBAYA
Kipindi cha shule ni kipindi chenye marafiki wengi; wazuri na
wabaya.Epuka sana marafiki wanaoweza kukupeleka katika njia zisizofaa kama
ulevi,uvutaji sigara na bangi.Matumizi ya vilevi huchochea ngono hata kufikia
hatua ya ubakaji.
4.SHIRIKI KWENYE MICHEZO
Kama inavyoshauriwa na wataalamu wa sayansi ya afya kuwa michezo
huboresha afya ya mwili na akili.Kuna faida lukuki za kujihusisha na michezo,
moja ni kukuondolea mawazo ya kujihusisha na ngono hii ni kwa sababu unakuwa
umechoka hivyo utahitaji kupumzika.
5.JIEPUSHE NA UPWEKE
Hakuna kitu kibaya kama upweke.Hali hii hukupelekea kuwa na mawazo mbali
mbali hasa yakilenga kupambana na hali hiyo.
Mama Teresa aliwahi kusema umasikini mkubwa kuliko wote ni upweke, na
kujifikiria hupendwi" kwa lugha ya kiingereza inasomeka “The
most terrible poverty is loneliness, and the feeling of being unloved.” ― Mother Teresa.
Bila kujijua, upweke unaweza kukufanya ushawishike kujiingiza
kwenye mahusiano ukidhani upweke utaisha.Kupambana na tatizo la upweke fuata
mbinu namba 3,5 na 6.
6.JIBIDISHE NA MASOMO, SOMA VITABU
Ukijibidisha na masomo utajikuta tu upo "busy" na hivyo kuweza
kutimiza majukumu ulipewa shuleni hivyo kuongeza ufaulu wako.
Pia, ukisoma vitabu vya lugha na maarifa vitakujenga kiakili na maarifa,
hivyo kujiongezea upeo wako wa kufiriki.Hivyo basi unaweza kugundua wito wako
na kipaji chako na mwishowe utajitambua.
7.JIPANGIE RATIBA UTAKAYOIFUATA WIKI NZIMA
Wataalamu wa masuala ya kutunza muda wamethibitisha kuwa mtu asiyejua
mpangilio wa mambo yake kwa siku nzima ni sawa sawa na mfu au bendera
inayofuata upepo. Hivyo, weka utaratibu wa siku kwa wiki nzima kimaandishi
utakaouheshimu na kuufuata.
8.USIOGOPE KUOMBA USHAURI
Watumie wazazi, walimu na ndugu waliokuzidi umri ili wakushauri pale
unapoona mambo hayaendi sawa.
Najua katika umri wenu kiasilia huchukulia kuwa wakubwa hawakuwahi
kupitia hatua kama hiyo ya makuzi.
Naomba nikuhakikishie kuwa watumie hao wakubwa wakupe ushauri, wanayajua
hayo mapitio.
9.SHIRIKI KWENYE MIDAHALO YA VIJANA
Ushiriki wako katika midahalo yenye kuelimisha vijana kuhusu mwenendo wa
maisha ni muhimu sana.Kupitia mafunzo hayo utajitambua na kuishi kwa malengo,
wakati huo huo ukipata fursa ya kujieleza na kuboresha uwezo wako wa
kuwasiliana na kujiamini mbele ya kadamnasi.
Mwandishi
wa Kitabu-Mtazamo Wako Ni Upi?
Imetolewa
na
Jielimishe
Kwanza.
Tunashukuru sana
JibuFuta