Tunapolitazama suala zima la adhabu mashuleni
nchini Tanzania na nchi nyingine duniani ni kizungumkuti.Kuna mgawanyiko wa
kimtazamo na pia kiitikadi katika makundi mawili; kuna wale wanaosema ni vyema
na wajibu wanafunzi wakapata adhabu pale wanapokiuka sheria za shule na wale
wanapinga vikali kuwepo kwa adhabu ya aina yeyote ile kwa
mwanafunzi(wakisisitiza kutoa maelekezo sahihi kwa mwanafunzi).
Picha na voices.yahoo.com |
Kuna adhabu mbalimbali zilizozoeleka kwa miaka
mingi iliyopita hadi leo.Kila aliyepitia shule kwa ngazi ya awali hadi
sekondari anajua mojawapo ya adhabu hizo; kubwa kuliko zote, na iliyozoeleka,
pia inayosemekana ni rahisi kuitumia kurekebisha tabia mbaya ni ile ya
viboko…najua kila mtu atakuwa anakumbuka siku alipowahi kuchapwa viboko na
mwalimu wake.Bila shaka hakikuwa kipindi kizuri kwako.
Nchini Tanzania, adhabu ya viboko inaendelea
kwa kusimamiwa na sheria ya adhabu ya
Kitaifa ya mwaka 1979 kama ilivyotolewa katika kipengele cha 60 cha
Sheria ya Kitaifa ya Elimu ya mwaka 1978.
Mwaka 2000, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania iliweka mkazo kwa kutoa tamko la kisheria kupunguza idadi
ya viboko kwa wanafunzi kutoka 6 hadi 4 na ilisisitiza kuwa ni Wakuu wa shule
pekee wanaotakiwa kutoa adhabu hiyo.Pia ilitoa tamko la kutoa adhabu kali kwa
walimu watakao kiuka sheria hiyo.[1]
Kwa upande mwingine, sheria ya kuwalinda
watoto ya mwaka 2009 inaeleza kuwa wazazi wana wajibu wa kuwalinda watoto wao
dhidi ya uonevu wa aina yeyote ile(kipengele cha 9), ikijumuisha kupigwa
kunakopelekea maumivu kwa mtoto (kipengele cha 3).[2]
Kisaikolojia, adhabu ya viboko kwa mwanafunzi
inapingwa vikali kutokana na athari za moja kwa moja kwa mwanafunzi kama;
- Zinatengeneza mahusiano mabaya ya kibinadamu
- Huchochea hofu na hali ya kutotaka kutenda kwa mwanafunzi husika
- Huchochea hali ya kujitengenezea mbinu za kujikinga na adhabu
- Madhala ya viboko ni ya muda…maumivu ya viboko hudumu muda mfupi
- Hazichochei tabia njema bali zinaficha uovu na utukutu.Kawaida mwanafunzi au mtoto anayechapwa sana viboko, huwa na tabia mbaya.
- Huangalia zaidi makosa/tabia mbaya kuliko tabia njema
- Adhabu hii haidhibiti chanzo cha kutokea tabia mbaya ya mwanafunzi.
Tuungane pamoja kipindi kingine katika
ukurasa huu wa Elimu ili kujifunza mbinu mbadala wa viboko kwa kutumia
saikolojia bila kuleta maumivu au madhara kwa mwanafunzi wakati huo huo
ikiboresha tabia njema na ufaulu wake.
Imetayarishwa na kutolewa na
Jielimishe Kwanza!
Soma zaidi kwa kubofya viunganishi vifuatavyo kama vilivyotumika kwa sehemu katika makala hii:
[1] http://lib.ohchr.org/HRBodies/UPR/Documents/session12/TZ/GIEACPC-GlobalInitiativeEndAllCorporalPunishmentChildren-eng.pdf
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni