Ijumaa, 3 Mei 2013
Wazazi wengi nchini na jamii nyingine wanapenda kuwaona watoto wao
wakiwa kama wao
walivyokuwa enzi hizo.Kwa maana nyingine wanataka kuwaona
watoto wao wakiwa kama nakala zao.
Watoto wa umri kati ya miaka 3-12(ni umri kabla ya kuanza shule na
kuanza shule) huonyesha tabia za kutaka kufanya vitu wenyewe bila kuzuiliwa na
mtu yeyote. Hupenda kujifunza lugha, na ishara mbalimbali kwa kasi isiyo ya
kawaida. Hapa wazazi wengi huwachukulia watoto wao kuwa ni watundu na
wasumbufu,la hasha! Ni umri wao kutaka kujifunza kuhusu mambo yanayowazunguka.
Kama mwanasaikolojia, Maria Montessori alivyoainisha kuhusu makuzi ya
watoto, anasema kuwa watoto wa rika hili
hupenda kuwa na urafiki na watoto wa rika lao. Pia kuhusu kuwaruhusu watoto
wafanye vitu wanavyoweza kufanya na si kulazimisha kuwasaidia.Alisema, "Never help a child with a task at which he
feels he can succeed." Yaani “Usimsaidie
mtoto kufanya kazi iliyo kwenye uwezo wake.”
Kiuhalisia makuzi ya watoto hutegemea sana mazingira, mfano mtoto
aliyekulia mazingira ya shida na duni kiuchumi anatofautiana sana kiutendaji na
yule aliyetokea mazingira ya raha na furaha na uchumi mzuri.Tofauti hii ambayo
inahusisha saikolojia ya makuzi ya mtoto, ina uwezo mkubwa sana wa kushusha au
kuongeza/kuimarisha utendaji wa mtoto afikiapo utu uzima.
Nitazungumzia tofauti za watoto katika mazingira hayo mawili katika
makala nyingine.Leo napenda uungane nami katika kuyajua madhara (8) ya kumzuia
mtoto wako kushiriki michezo ya kawaida na wenzake...
Mwanasaikolojia maarufu duniani Erick Erickson 1956 aliainisha hatua
nane(8) za maendeleo ya makuzi ya binadamu kijamii na kihisia kuanzia kuzaliwa
hadi utu uzima.Alisisitiza kuwa kila hatua ina vipingamizi vyake ni muhimu
kupitia kila hatua na kuondoa vipingamizi hivyo kabla ya kwenda hatua nyingine.
Nitapenda kujikita hasa kwenye makuzi ya watoto ambayo yana mchango
mkubwa kwa utu uzima wa mtu.Nikizingatia hatua mbili za makuzi ya mtoto yaani hatua ya 2 na hatua ya 3 za
maendeleo ya ukuaji wa mtoto kama alivyozielezea Erickson;
Katika hatua ya pili (2) umri wa mtoto kabla ya kuanza shule
(chekechea), aliangalia mambo mawili yanayopingana yaani “Kujifunza mwenyewe Vs Aibu (miaka 3-4)”.Akimaanisha kuwa mtoto wa
umri huu hupenda kufanya mambo mwenyewe na hujisikia aibu pale anapokatazwa kwa
kuambiwa “Usi…” Mtoto aliyekuzwa vizuri hujisikia vizuri bila kuwa na aibu
yoyote.
Pia katika hatua ya tatu (3) umri wa kuanza shule (baada ya chekechea),
umri wa michezo, mtoto hupambana na vitu viwili yanayopingana yaani Kujianzishia kujifunza Vs Kujilaumu/Hatia.(miaka
4-12). Akimaanisha kuwa mtoto
aliyekuzwa vizuri kwa kupewa uhuru wa kujifunza (1) hujiona fahari kuwa na
wenzake,(2) hupenda kushirikiana na wenzake, (3) hupenda kuongoza pia
kuongozwa.
Kwa upande mwingine, mtoto aliyekuzwa mazingira ya kubanwa hujihisi
kuwa na hatia hivyo (1) huwa muoga (2) hujitenga na wenzake (3) anakuwa
tegemezi sana kwa wazazi (4) anakuwa amekosa mbinu za michezo na uwezo wa
ubunifu.
Nitayajumuisha madhara (8) ayapatayo mtoto wako kwa kukosa kushiriki
michezo ya kitoto na wenzake kama ifuatavyo;
___________________
1.Mtoto kukosa uwezo wa kujiamini mbele ya hadhara.
Ukifuatilia
michezo ya watoto kama mpira,kukimbizana, na mingine mingi utagundua kuwa
watoto ni waongeaji na watendaji hasa wakiwa na watoto wa rika lao.Endapo mtoto wako atakosa
fursa ya kukutana na wenzake, kwanza atakuwa na hofu-kwasababu hajawazoea, pili
atajihisi mnyonge mbele ya wenzake.Hivyo kuanza kuijenga tabia ya kutokujiamini
tangu utotoni.
2.Kukosa uwezo wa kuongoza
Kutokana
na hofu aliyojingea tangu utotoni, ni dhahiri kuwa atakuwa hana mbinu za
kuwasiliana kama kiongozi, pia atakuwa na aibu iliyopitiliza mbele ya watu
anaotakiwa kuwaongoza.
3.Kuwa mtegemezi wa maamuzi
mbali mbali kwa wazazi hata yaliyo kwenye uwezo wake
Tatizo
hili ni kubwa, limepelekea vijana wengi kushindwa kuamua mambo yao wenyewe, eti
“labla nimuulize baba na mama”, kazi lazima achaguliwe na wazazi/walezi.
Hili ni
tatizo lililokuwa tangu utotoni, yaani kukosa uwezo wa kuamua kufanya hasa
baada ya kuambiwa “Usi…” na kutopata nafasi ya kuona watoto wengine wakijaribu
kufanya jambo fulani.
4.Mtoto
hujitenga na jamii
Kwa
kuwa mzazi au mlezi ulimtenga mtoto na jamii kwa kumfungia ndani wakati wote,
na kumwachia mtoto wako awe na urafiki mkubwa na Televisheni na michezo yake
pekee, usitegemee kuona mtoto wako akiwa mbali na jamii hasa afikapo ujana na
hata utu uzima.
5.Kukosa uwezo na mbinu za kuwasiliana
Kama
nilivyoeleza awali, watoto wa umri huu hupenda kujifunza lugha na ishara mbali
mbali za mawasiliano wakiwa na watoto wa rika lao.Hivyo basi, kama utamfungia
mtoto wakati wote asikutane na wenzake, tambua kuwa unamwandaa mtoto ambaye
atakuwa hana uwezo mzuri kimawasiliano.Ujuzi huu ni muhimu sana katika shughuli
mbali mbali za kijamii.
6. Kuwa na viungo dhaifu na kukosa
uchangamfu wa mwili
Itafahamika
kuwa uimara wa viungo vya mtoto haujengwi na vyakula pekee, bali mazoezi ya
viungo hasa kwa michezo ya kitoto ya kukimbizana hapa na pale.Kisaikolojia,
mtoto huathirika sana anapoona watoto wengine wakicheza kwa furaha wakati yeye
anazuiliwa ama kwa kupigwa na kukaripiwa.Hii humfanya mtoto kunyongea na kukosa
uchangamfu.
7.Humpelekea mtoto kujitengenezea tabia ya kutoroka ili atimize
hisia zake
Hapa
ndipo utukutu na tabia mbaya zinapoanzia.Mtoto anaamua kujitengenezea mbinu ili
aweze kushiriki kwenye michezo ya kitoto.Mtoto anapofikia hatua hii, wazazi
wengi hulaumu sana kuwa watoto wa siku hizi hawatulii, wakiwa wamesahau kuwa
wenyewe ndiyo chanzo cha kuwafanya watoto watoroke kwasababu ya ulinzi mkali
nyumbani. Mtoto hawezi kutoroka nyumbani kama anapata upendo na kueleweshwa
mema na mabaya kwa vitendo, pia kwa kumpa na kukubaliana utaratibu wa michezo.
8.Mtoto kukosa ubunifu wenye tija
ya kupambana na changamoto za maisha
Ubunifu
wa mtoto unachangiwa na kuwepo kwa ushirikiano wake na watoto wenzake.Ni hapo
kipaji cha mtoto kinapojidhirisha. Kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na
teknolojia, wazazi wengi wamewaachia watoto wao kutazama televisheni na komputa
na si kwenda kucheza na watoto wengine.
Naomba
nitoe rai yangu kwa wazazi wa karne hii ambao mnakumbana na changamoto mbali
mbali za mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kiasi kwamba mnakuwa hamna
muda wa kukaa na watoto, ila ni kutoa amri kuwa hairuhusiwi mtoto kutoka
nje.
Ni vizuri kufuatilia kila hatua ya ukuaji wa mtoto na kuhakikisha yale mahitaji ya hatua husika yanafikiwa, kinyume na hapo tusishangae kuona watoto wetu wamekuwa vile tusivyotarajia.
Ni vizuri kufuatilia kila hatua ya ukuaji wa mtoto na kuhakikisha yale mahitaji ya hatua husika yanafikiwa, kinyume na hapo tusishangae kuona watoto wetu wamekuwa vile tusivyotarajia.
Ungana na mkala yangu nyingine kuhusu "Sababu zinazoweza kumfanya mtoto wako kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya akiwa katika umri mdogo."
SOMA HII PIA KUMSAIDIA MTOTO WAKO KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA INTANETI NA RUNINGA http://jielimishekwanza.blogspot.com/2013/05/malezi-na-familia.html
SOMA HII PIA KUMSAIDIA MTOTO WAKO KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA INTANETI NA RUNINGA http://jielimishekwanza.blogspot.com/2013/05/malezi-na-familia.html
Makala hii imeandikwa na Henry Kazula, ikiwa ni utafiti wake binafsi ukisaidiwa na nadharia kutoka tovuti zifuatazo:
http://www.dailymontessori.com/montessori-theory/
http://www.dailymontessori.com/montessori-theory/
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni