inspire

inspire

Lebo

AFYA (8) AJIRA (5) BIASHARA (39) ELIMU (14) MAHUSIANO (2) MALEZI (16) MAZINGIRA (12) SAIKOLOJIA (48) VIJANA (7)

Business registration

Green Consulting

business consultancy

business consultancy

Business consulting-2

Business consulting-2

Professional Consulting

PDC

Swahili translator

Swahili translator

TANGAZO-KITABU

E-BOOK: MTAZAMO WAKO NI UPI?

TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- .... TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- ....

TANGAZO TUWEZESHANE

TANGAZO TUWEZESHANE

DARDY'S INVST-20/10/2017

DUNIA IKUONE

DUNIA IKUONE

Jumatano, 21 Oktoba 2015

MTAZAMO: JINSI YA KUTATHMINI UTENDAJI KAZI WAKO…

 
Picha na www.sonsteinfinancial.com

Tukirejea makala yetu ya TAMBUA UWEZO WAKO KIUTENDAJI, USISUBIRIKUAMBIWA, iliangazia tafiti mbali mbali zinazohamasisha kujifanyia tathmini binafsi ya kiutendaji kabla ya kuomba ridhaa ya wengine kututathimini. Michelle Roccia, mtendaji msaidizi wa kitengo cha “Employee Engagement” katika kampuni ya WinterWyman anasema; The self-assessment is an essential part of performance evaluation because it's an opportunity for you to assess your own achievements. You own the performance appraisal. You should look across the past year and tell your manager what you've done and areas you'd like to focus on," Anasisitiza kuwa tathmini binafsi ya kiutendaji ni fursa kwako kujua maendeleo na mafanikio katika utendaji kazi wako.Pia ni kipimo cha utendaji wa kazi au biashara yako.Kwa kuzingatia mwaka uliopita unaweza kujionea ni maeneo yapi unayopaswa kuweka maboresho na msisitizo ili kuongeza ufanisi wako na uzalishaji.

Tunaweza tena kujifunza zaidi kuhusu mbinu stahiki za kujitathmini wenyewe kwa kuzingatia hatua zifuatazo;
1.JIWEKEE MALENGO KATIKA KAZI YAKO
2.LINGANISHA UTENDAJI WAKO KATIKA MUDA ULIOJIWEKEA
3.JIAMINI KUWA UNAWEZA KUTIMIZA MALENGO YAKO 
4.JIWEKEE VIGEZO VYA MAFANIKIO KULINGANA NA UTENDAJI WAKO
5.ZINGATIA MAAMUZI YAKO KIUTENDAJI UKIFUATA KANUNI ZA KAZI.
                                 Kwa ufafanuzi zaidi na maulizo, tuwasiliane:


Whatsapp +255(0) 754 572 143
Imetayarishwa na
Mwandishi wa Kitabu-“Mtazamo Wako Ni Upi?”
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!

Jumamosi, 12 Septemba 2015

MTAZAMO: KILIMO CHA KIJASIRIAMALI; ANZIA ULIPO...



“ …Kufanya biashara yenye mafanikio si kutegemea kuona mafuriko ya pesa kwa mkupuo; ila ni kukusanya faida/pesa kidogo kidogo kutoka vyanzo vidogo vidogo vya mapato” 
-Bw.Baraka Mponda-
______________________
Tunapozungumzia kilimo cha kijasiriamali ni kilimo kinachofanyika na kufanikiwa katika mazingira yenye changamoto ambazo hubadilishwa kuwa fursa. Mkulima mvumilivu na makini huona na kuitumia fursa ambayo wengine hawajaiona au wameiona na kupuuzia.
Jicho la blog hii kimtazamo liliweza kumuona mkulima  makini na mjasiriamali mwenye mafanikio Bw. Baraka Mponda (44) wa kitongoji cha Patandi, Tengeru-Mita chache kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela -Arusha anayejihusisha na kilimo cha kijasiriamali cha mboga mboga na viungo. Alianza  kujihusisha na kilimo mnamo mwaka 1992 katika eneo la nyumba yake ambalo tumemkuta.
Bw. Baraka Mponda (44) akielezea jambo kwa mwandishi-Henry Kazula kushoto kwake.                      



































____________                                                                                                                        _________
Yafuatayo ni mahojiano yetu na Bwana Mponda ikiwa ni hamasa kwa vijana na wakulima wengine wenye kianzio lakini wanashindwa kuchukua hatua nyingine ya kiujasiri kuondoa changamoto na kuzibadilisha kuwa fursa.
Mahojiano yalianza hivi:
·        Je, ni shughuli hii hii ya kilimo cha kijasiriamali cha mboga mboga na viungo, ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku wa kienyeji imekufikisha katika mafanikio tunayoyaona leo? Ukizingatia kuwa unauza mboga kwa shilingi 100 kwa fungu moja!
“ …Kufanya biashara yenye mafanikio si kutegemea kuona mafuriko ya pesa kwa mkupuo; ila ni kukusanya faida/pesa kidogo kidogo kutoka vyanzo vidogo vidogo vya mapato” 
alisema Bw.Baraka Mponda kwa kujiamini.
Bw. Baraka Mponda (44) akionyesha kiwango cha fungu la viuongo-mboga kwa sh.100(TZS).
·        Ni lini umeanza kujishughulisha na kilimo cha kijasiriamali na kiutaalamu kwa mfumo wa umwagiliaji matone-“drip irrigation” kupitia njia ya “pump” na kisima ulichochimba.Vipi ulitumia gharama kiasi gani kwa huu mfumo wa “drip irrigation”?
…Mfumo huu wa kilimo cha kijasiriamali cha-“Drip irrigation” nimeanza mwanzoni mwa mwaka 2015 kwa gharama ya shilingi milioni 5, ingawaje nilianza kujishughulisha na kilimo cha mboga mboga na viungo mnamo mwaka 1992. Mipira ya kutandaza kwenye matuta iliyounganishwa katika mfumo wa maji ya kisima cha kuchimba mwenyewe na “pump” nimenunua kutoka kampuni ya “Bulton Tanzania Limited” kwa teknolojia kutoka Israel...Alisema Bw.Mponda.
Mfumo wa umwagiliaji katika shamba la Bw. Baraka Mponda (44) nyumbani kwake.
·        Unaweza kuelezea jinsi ulivyoweza kuchimba na kuhifadhi maji kwenye "reservoir"; umetumia gharama kiasi gani?
…Chanzo cha maji kwa matumizi ya nyumbani na kilimo ni kupitia kisima cha kuchimba na kuhifadhi maji kutumia “pump” katika “tank” na “reservoir” yenye ujazo wa 36,000ml. Zoezi zima la kupata maji limenigharimu shilingi milioni 7…alisema kwa ujasiri Bw.Mponda.
Hapa ndipo chanzo cha maji (kisima) kwa matumizi ya nyumbani na kilimo.Maji hupandishwa kwa "pump" ya umeme kwenye "tank"na "reservoir" iliyojengwa katika mwinuko mita chache kutoka nyumbani kwake kama inavyoonekana katika picha hapa chini.
Nyumba ya Bw. Baraka Mponda (44) inavyoonekana katika mwinuko ilipo "reservoir" kwa ajili ya kilimo.
·        Nini mafanikio yako tangu uanze kujihusisha na kilimo cha kitaalam na kijasiriamali?
…Mimi ni baba wa watoto 3, nina uwezo wa kuwahudumia watoto wangu kwa kila kitu ikiwa pamoja na kielimu hadi ngazi ya chuo kikuu. Mtoto wangu wa kwanza anaenda chuo kikuu mwaka huu, wa pili yupo shule ya sekondari nzuri na inafanya vizuri kitaaluma. Nina nyumba yangu  na Magari mawili; moja la kutembelea mke wangu na lingine la shughuli za shamba.Pia nimeajiri vijana 3 wanaonisaidia shughuli za shamba na ufugaji…alijibu kwa tabasamu Bw.Mponda.
Bw. Baraka Mponda (44) na mke wake(katikati), nyuma ni magari wanayomiliki.Wengine ni mwandishi Henry Kazula(kushoto) na John Karugah (kulia); wote ni wanafunzi shahada ya uzamili- Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia-Nelson Mandela.

·      Je unajishughulisha na nini kingine zaidi ya kilimo?
Mimi ni msambazaji wa mboga mboga kwa “tender” katika mahoteli jijini Arusha  (shughuli hii inayohitaji kuwa na mtaji wa shilingi milioni 10).
·    Nini malengo yako ya siku za usoni?
…Malengo yangu ya baadaye ni kulima kisasa zaidi kwa kutumia “greenhouse” hasa kwa zao la Hoho nyekundu na Njano…Alisema Bw.Mponda.
·    Kipato chako cha mwezi ni wastani wa sh.ngapi?
…haina shida! Kipato changu kwa mwezi hakipungui milioni 2 ikiwa nilianza na mtaji wa shilingi 10,000 kununua mbegu.
·      Umepitia changamoto zipi hadi leo tunaona mafanikio yako?Ulifanyaje kupambana nazo?
…Bila kuficha, hakuna kazi isiyo na changamoto; Kutokuwezeshwa kimtaji; mafanikio niliyonayo yangeweza kuwa makubwa zaidi na kutoa fursa ya ajira kwa wengine.Kutokata tamaa/uvumilivu na kuthamini kidogo unachopata ni msingi mkubwa katika kukua kibiashara.Maisha ni kupambana hata katika mazingira magumu.
·   Tumalizie kwa kutoa ushauri  wako kwa vijana na wakulima wengine:
…Nawashauri vijana na wakulima wenzangu kuwa na Uvumilivu na kupambana…alijibu kwa kifupi.
·    Nini rai yako kwa wadau wa kilimo na serikali?
…Nasisitiza utolewaji wa semina na warsha kwa vijana zenye kuwawezesha na kutoa fursa za kujiajiri katika kilimo. Pia, Serikali inatakiwa iwafungulie vijana milango ya kujiajiri kwa kumaanisha na isiwe kuongea tu bila utekelezaji…alimalizia Bw.Mponda.
Picha zote na Paul Lucas- mwanafuzi shahada ya uzamili, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia-Nelson Mandela.
Imetayarishwa na
Mwandishi wa Kitabu-“Mtazamo Wako Ni Upi?”
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!






Jumapili, 28 Juni 2015

BIASHARA: TAMBUA UKWELI HUU MCHUNGU; KWA NINI BIDHAA ZA MAKAMPUNI YA KIMTANDAO (MULTI-LEVEL MARKETING-MLM COMPANIES) NI GHARAMA?

                Picha na shutterstock
Biashara iendeshwayo na Makampuni ya Kimtandao almaarufu kama “Multi-Level Marketing (MLM) Companies”  imeshamili na kuwa ni gumzo kwa takribani zaidi ya muongo mmoja katika nchi zinazoendelea (Afrika- Kenya, Nigeria, Ghana, Zimbabwe, Namibia, Afrika Kusini….), ingawaje tafiti zinaonyesha kuwa ilianza kwa mara ya kwanza miaka ya 1940s nchini Marekani. Hivyo basi biashara hii si mpya kama wengi wanavyofikiria na kuwaaminisha wengine.  Nchini Tanzania kampuni nyingi za MLM huingia nchini kupitia nchi ya Kenya, nisingependa kuzianisha,; unazifahamu na yawezekana nawe upo huko na umekwisha jijengea fikra ya “be your own boss” kwa kuwatoa wengine sadaka kama wasambazaji ili ufaidike kwa kupanda cheo kupitia ngazi (levels) mbali mbali kama zilizokubaliwa na kampuni unayoitumikia.
Kutokana na ukimya na sintofahamu nyingi kuhusu uwepo na gharama kubwa katika bidhaa zinazosambazwa kupitia MLM, Jielimishe Kwanza Blog tumeona ni vyema tuvunje ukimya huu kupitia kufanya utafiti wa kina kuhusu Makampuni yanayojihusisha na MLM na kukushirikisha.
Makampuni hayo yanayojihusisha na biashara ya Kimtandao  hutengeneza na kuuza bidhaa wanazoziamini sana na kuwaaminisha wengine kuwa zinatibu magonjwa sugu, kuboresha kinga ya mwili, kuthibiti uzito na mwisho wa yote ni ahadi kem kem za maisha bora yenye uhuru wa kipato na ile ya “kumiliki biashara yako mwenyewe”.
Swali la msingi ambalo kila Mtanzania anapenda kujua ni hili la kuwepo kwa gharama kubwa ya bidhaa zinazozalishwa na makampuni ya MLM. Kupitia utafiti binafsi wa Jielimishe Kwanza Blog! umebaini yafuatayo;
Tracy Coenen- mtaalamu wa masuala ya Intelijensia na upelelezi wa masuala ya biashara anasema kuwa; "The truth is that products are overpriced through multi-level marketing companies because they have to pay commissions to distributors on many levels." That’s the whole point of multi-level marketing: Many levels of distributors get a piece of the action when you buy something. Akimaanisha kuwa, gharama kubwa husababishwa na kuwalipa bakshishi/sehemu ya faida ya mauzo wasambazaji walio wanachama wa Kampuni husika.Pia huwalipa kutokana na kuwashawishi wengine kutumia na kujiunga na Kampuni husika. Bila shaka umewahi kusikia kuwepo kwa makampuni hayo hapa kwetu Tanzania yakihamasisha wengine kujiunga nao kupitia bidhaa zao, na yawezekana u mmoja wao.
Kutokana na maelezo na mafundisho yao, husingizia kuwa bidhaa zao ni bora zaidi kuliko bidhaa nyingine duniani…yaani ni kama zimeshushwa kutoka mbinguni.Tuwe na uhalisia katika hili!
Imefika wakati wa kufumbuka macho Watanzania, tusitamanishwe na mafanikio hewa kwa kutumika na wengine. Hakuna urahisi unaopatikana katika biashara hizo hasa unapoaminishwa kuwa utakuwa na uhuru wa kipato na kumiliki biashara yako mwenyewe…Biashara yako mwenyewe?...wakati unawekewa masharti na watu wengine? Mfano: hakikisha unaingiza watu 2 kwa wiki, kununua na kutumia bidhaa ndipo upate gawio la faida.Cha kusikitisha zaidi huwezi kujiunga na Makampuni hayo na kupata gawio la faida kubwa kama hujanunua bidhaa kwa gharama kubwa, kuuza bidhaa zao kwa bei waliopanga na kushirikisha wengine wajiunge kwa kuwahamasisha na kuwaaminisha kama ulivyoaminishwa kuwa zitawatoa pale walipo kimaisha. Kuhamasisha wengine wajiunge ni silaha kubwa katika kampuni hizo. Usipofanya hivyo hutaona faida ya biashara hii na mwisho wa siku itakushinda! 
Robert FitzPatrick mwandishi wa “Pyramid Scheme Alert” pia mtafiti wa masuala ya biashara za mtandao (MLM) anaweka bayana kuhusu suala zima la kuhakikisha wengine wanajiunga katika kampuni ndipo mhusika apate gawio la faida litokanalo na gharama kubwa ya kila bidhaa; “For there to be a “winner” at the top, there must be “losers” below. The ratio of losers to winners is pre-determined, usually 100 to 1.” Profit Reserved only for those at the Top. Hivyo katika wengi (watu 100) waliohamasishwa na kujiunga kama wasambazaji anayefaidika zaidi ni mtu 1 tu! Yaani, ili mtu mmoja ayaone mafanikio ya kweli ndani ya kampuni ni lazima watu 100 chini yake wapate hasara. Huu ni ukweli mchungu ambao hufichwa na washiriki wa makampuni hayo. Ndiyo maana kila kukicha wanawaza kuingiza watu wapya katika kampuni. Ki uhalisia utafanikiwa kwa kuwekeza zaidi muda wako na pesa nyingi katika kampuni hizi ili upate mafanikio si kutokana na kupendwa sana na Makampuni yao, ila ni hela na muda uliowekeza kuisaidia kampuni kutimiza malengo yake. Ndiyo maana tunapingana vikali na dhana ya kusema kuwa “be your own boss” katika biashara hii.
Siri kubwa ya makampuni hayo ni wewe kuhakikisha unahamasisha wengine wajiunge kuwa wasambazaji na watumiaji wa bidhaa zao ndipo ulipwe…hii si kazi rahisi kama wanavyoeleza na kurahisisha katika mafundisho yao. 
Nasisitiza tena, Watanzania tufumbuke macho, tusome, Tujielimishe Kwanza kabla ya kutaka kupapatikia biashara zinazoonekana kuwa na mteremko ilihali hatujui yaliyojificha; mbele kukiwa na mlima mkubwa unaolighalimu taifa katika siku za usoni.
Chaguo ni lako, kujiunga au kutokujiunga na Makampuni hayo.Ukitaka kutoka nayo kimaisha, wekeza zaidi muda na pesa yako, hamasisha wengine wakubali kujiunga.
Pia kuwa makini; kuna bidhaa kama za Makampuni ya MLM zina gharama nafuu sana na zinafanya kazi vizuri na zina ubora zaidi ya hizo za MLM. 
Usidanganyike na urembo au madoido ya vifungashio vya bidhaa hizo, zipo kama kivuli cha kuficha ujanja ujanja unaofanywa na wamiliki wa Makampuni ya MLM.
Huo ndiyo ukweli unaofichwa ili kuneemesha wengine.
Ukiwa na maoni, manung’uniko na kuhitaji ufafanuzi zaidi usisite kutuandikia.
Imetolewa na,
Jielimishe Kwanza!




Jumamosi, 20 Juni 2015

MTAZAMO: TAMBUA UWEZO WAKO KIUTENDAJI, USISUBIRI KUAMBIWA!

Picha na www.trinityp3.com
-->
Wengi hujiuliza, mimi nikiwa mmoja wao; hivi utendaji kazi wangu unaendana na matakwa ya mwajiri au malengo ya kazi niliyojiwekea? Wengi wao hushindwa kupata majibu sahihi kupitia uhakiki au tathmini binafsi “self- assessment” kutokana na kukosekana kwa mbinu stahiki. Hii imepelekea wengi kuwa tegemezi kwa kupata tathmini zisizokidhi kiu zao kutoka kwa wengine kuhusu utendaji kazi wao; ingawaje ni jambo jema pia kupata tathmini ya wengine kukuhusu na kuhusu utendaji kazi wako.
Kutegemea tathmini ya wengine pekee kuhusu utendaji kazi wetu inaweza isiwe njia sahihi zaidi kuliko ile binafsi-“self assessment” kutokana na kuwepo kwa ubinafsi/ unafsi na roho za korosho au roho za kwanini yeye? baina ya mfanyakazi mmoja na mwingine, kadhalika kati ya mfanyabiashara mmoja na mwingine.Hakuna anayependa mafanikio ya mwingine katika utendaji kazi na biashara.
Katika karne hii ya utandawazi iliyo na mabadiliko kila kukicha, bila kusahau ubunifu wenye ushindani mkubwa -ujulikanao kama "creative destruction" kama alivyowahi kuainisha Joseph Schumpeter (1883–1950), ni muhimu kutambua kuwa upo umuhimu mkubwa wa kujitathmini mwenyewe kiutendaji ili kuboresha mapungufu uliyo nayo kwa haraka zaidi ukiendana na uhitaji wa soko la ajira au biashara.Ubunifu wenye tija unahitajika sana katika wakati huu tulio nao.
Kwa bahati nzuri sana; kumekuwepo na tafiti mbali mbali zinazohamasisha kujifanyia tathmini binafsi ya kiutendaji kabla ya kuomba ridhaa ya wengine kututathimini. Michelle Roccia, mtendaji msaidizi wa kitengo cha “Employee Engagement” katika kampuni ya WinterWyman anasema; “The self-assessment is an essential part of performance evaluation because it's an opportunity for you to assess your own achievements. You own the performance appraisal. You should look across the past year and tell your manager what you've done and areas you'd like to focus on," Anasisitiza kuwa tathmini binafsi ya kiutendaji ni fursa kwako kujua maendeleo na mafanikio katika utendaji kazi wako.Pia ni kipimo cha utendaji wa kazi au biashara yako.Kwa kuzingatia mwaka uliopita unaweza kujionea ni maeneo yapi unayopaswa kuweka maboresho na msisitizo zaidi ili kuongeza uzalishaji.
Ford Myers, mwandishi wa kitabu "Get The Job You Want, Even When No One's Hiring anaongezea tena kwa kukazia fikra kuhusu “self-assessment” akisema kuwa; "It's an opportunity for you to reflect on how you're doing in your career, not just your job".Use it to think about where you are going long-term and where you are in your career. Akimaanisha kuwa; tathmini binafsi ni fursa kwako kuvuta taswira ya jinsi unavyofanya katika ujuzi na utendaji wako na si kazi pekee. Itumike kutafakari kwa kina kuhusu mwenendo wako kiutendaji na wapi ulipo kiutendaji.
Pia tathmini binafsi hupelekea kujiongezea sifa katika soko la ajira-bringing value to the market place; kama alivyosema Jim Rohn. Mtu binafsi kwa kufanya tathmini binafsi anaweza kujifunza mbinu mbali mbali za kujiongezea utendaji kazi zinazohitajika katika soko la biashara au ajira kutokana na mapungufu au uhitaji alio nao.
Ukizingatia faida tajwa za kujifanyia tathmini binafsi ya kiutendaji, ni vyema kuanza sasa kuangalia wapi ulipo katika utendaji kazi wako; ikiwa unafanya kazi bora upate ujira pekee au unafanya kazi ili kujiongezea fursa za kupata pesa zaidi; utaamua wewe.
 Nimeandika makala hii kwa makusudi kabisa ikiwa ni sawa na “kurusha jiwe kwenye giza nene”; yeyote atakayepiga kelele huko, limempata kwa nafasi yake kiutendaji.Utaangalia ni eneo gani upo katika utendaji kazi, hivyo anza sasa kujitathmini mwenyewe, usisubiri kuambiwa na wengine kwa kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa. Najua kuna swali mahsusi unataka kuuliza tena; nawezaje kujitathmini mwenyewe?  How can I make self -assessment?
Ungana nami wakati mwingine kama huu utajibiwa bila hiyana ikiwa tu utaniandikia kuhusu kuguswa na makala hii.
 Whatsapp +255(0) 754 572 143
Imetayarishwa na
Mwandishi wa Kitabu-“Mtazamo Wako Ni Upi?”
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!


Jumamosi, 30 Mei 2015

MAZINGIRA: KUELEKEA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI JUNI 5


Kama ilivyo ada kila mwaka, tarehe 5 Juni duniani kote tunaungana kwa sauti moja na kauli mbiu moja kuadhimisha siku hii muhimu kwa mustakabali wa maisha yetu; kwa kuzingatia kuhifadhi na kuitunza “nyumba” (mazingira) inayotutunza.
Siku hii muhimu duniani ilianzishwa katika Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN General Assembly) mwaka 1972.Hivi leo “Siku Ya Mazingira Duniani” inaendelea kuheshimiwa duniani pote pia kusimamiwa kikamilifu na Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Mazingira-United Nations Environment Program (UNEP).Tukiwa kama familia moja duniani, husindikizwa na kauli mbiu itolewayo kila mwaka kwa kuzingatia maoni ya wataalam na wadau wa Mazingira duniani.
Kwa bahati nzuri kauli mbiu ya mwaka huu isemayo“Seven Billion Dreams.One Planet.Consume With Care kwa tafsiri ya lugha ya Kiswahili-Ndoto bilioni saba. Sayari moja.Tumia kwa uangalifu inatukumbusha kutumia rasilimali tulizonazo kwa uangalifu ukizingatia kuwa kuna ongezeko la idadi ya watu duniani (bilioni 7 hadi sasa) wenye ndoto tofauti tofauti, mabadiliko ya tabia nchi na wakati huo huo rasilimali nyingi zilizopo si rejereshi; zinatumika na hazijirudii au kurudishwa tena.
Shirika hilo la Umoja wa mataifa linalohusika na Mazingira duniani (UNEP) limeweka angalizo kuu kuwa kutokana na mfumo wa maisha ya binadamu, na uhitaji wa rasilimali ambazo kwa kiasi fulani zinaelekea kutokidhi ongezeko la idadi ya watu duniani; kuna hatari kubwa kuwa kama hali itaendelea kama kawaida kwa kuangalia makisio ya ongezeko hilo la watu bilioni 9.6 ifikapo mwaka 2050 tutahitaji kuwa na sayari 3 ili kukidhi mahitaji yetu.Unashangaa! Ndiyo huko tunakoelekea na vizazi vyetu. Wengine naona wameanza kuangalia uwezekano wa kuishi kule kwenye sayari ya “Mars”.Mimi na wewe je? Natania tu…
Imefika wakati wa kuamka sasa, kila mtu kuchukua wajibu sasa, kufanya pale anapoweza kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinatumika kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia maendeleo endelevu- maendeleo yanayokumbuka na kuchukua taadhali kubwa kuwa kuna vizazi vijavyo vitakavyohitaji rasilimali zilizopo sasa.Ni maendeleo yanayozingatia manufaa ya jamii, mazingira yenyewe na uchumi kwa ujumla wake.Maendeleo yanayosahau kimoja kati ya hivyo vitatu, si maendeleo endelevu; yanapaswa kukosolewa, kubezwa na kuzomewa kwa kelele nyingi.Anza sasa!
Imetayarishwa na
Mwandishi wa Kitabu-“Mtazamo Wako Ni Upi?”
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!

Alhamisi, 21 Mei 2015

AJIRA: UHURU WA KUUNDA NA KUJIUNGA NA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

-->
Picha na www.eventbrite.ca

UTANGULIZI.
Uhuru wa kujumuika unawapa wafanyakazi uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Vilevile unawapa wafanyakazi haki ya kushiriki katika shughuli za vyama vyao kwa uhuru bila hofu ya kubaguliwa au kunyanyaswa au kupoteza haki yoyote.
Hata hivyo, uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi una mipaka yake. Uhuru huu umewekewa mipaka kwa wafanyakazi wa kada zifuatazo:-
a)    Mahakimu – hawa wanaweza kuunda na kujiunga na Chama cha Maafisa wa Mahakama pekee.
b)   Waendesha Mashitaka – hawa wanaweza kuunda na kujiunga na chama cha Waendesha Mashitaka au Watendaji wengine wa Mahakama pekee.
c)    Wafanyakazi wa kada ya Meneja Mwandamizi ambaye kwa nafasi yake ana mamlaka ya kutengeneza sera kwa niaba ya muajiri na ana mamlaka ya kuingia majadiliano na Chama cha Wafanyakazi, haruhusiwi kujiunga na Chama cha Wafanyakazi wasio Mameneja Wandamizi.
Pia uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi unatoa kinga ya mfanyakazi kutobaguliwa na mtu yeyote kwa sababu ya kuwa mwanachama wa chama cha wafanyakazi au kujihusisha na shughuli halali za chama.
HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
1.   Kuwa na Katiba yake bila kuingiliwa na dola, chama cha siasa au muajiri.
2.   Kupanga na kuendesha mambo yake ya ndani na shughuli halali bila kuingiliwa.
3.   Kujiunga na kuunda shirikisho na kushiriki shughuli za shirikisho hilo.
4.   Kujiunga na mashirikisho ya kimataifa, kuchangia na kupokea misaada ya kifedha kutoka kwa vyama au mashirikisho hayo. 
UTARATIBU WA KUUNDA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya mwaka 2004, Chama cha Wafanyakazi kinaweza kuanzishwa na wafanyakazi wasiopungua 20. Wafanyakazi hao wanapaswa kuitisha kikao cha kuanzisha Chama, ambapo watajiorodhesha na kutia saini zao katika rejista ya mahudhurio. Watamteua Katibu wa kikao ambaye atatayarisha muhtasari wa kikao wenye azimio la kuanzisha chama.
MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA KUANZISHA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
1.   Chama kiwe ni chama halisi cha Wafanyakazi (Bona fide Trade Union).
2.   Kisiwe chama kwa madhumuni ya kupata au kutengeneza faida (Association not for Gain).
3.   Kiwe ni chama huru, kwa maana kwamba kisianzishwe na muajiri au waajiri au serikali.
4.   Kianzishwe na wafanyakazi wasiopungua 20.
5.   Kiwe na katiba na kanuni zinazozingatia kifungu cha 47 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya 2004.
6.   Kiwe na jina lisilofanana na jina la chama kingine, kuzuia mkanganyiko au kuwapotosha watu.
7.   Kiwe na makao yake makuu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
UTARATIBU WA KUSAJILI CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Chama cha Wafanyakazi kinapaswa kusajiliwa ndani ya miezi sita (6) kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwake. Maombi ya usajili yatafanyika kwa kujaza fomu maalum ambayo itajazwa kikamilifu na kusainiwa na katibu wa kikao kilichoanzisha chama hicho.
Fomu hiyo ya maombi inapaswa kuambatana na nakala zilizothibitishwa za rejista ya mahudhurio, na nakala zilizothibitishwa za katiba na kanuni, na kuziwasilisha kwa msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na waajiri.
MAJUKUMU YA CHAMA KILICHOSAJILIWA.
Chama kilichosajiliwa kinapaswa kuwasilisha kwa msajili kila ifikapo tarehe 31 Machi au kila mwaka taarifa zifuatazo:-
a)    Taarifa ya fedha zilizokaguliwa kwa kipindi cha fedha kinachoishia tarehe 31 Desemba ya mwaka uliopita.
b)   Orodha ya wanachama inayoonesha jumla ya wanachama kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Desemba ya mwaka uliopita.
c)    Majina ya viongozi walioteuliwa au kuchaguliwa na anuani zao ndani ya siku 30 tangu uteuzi au uchaguzi kufanyika.
d)   Mabadiliko ya kanuni ndani ya siku 30 kuanzia siku ya mabadiliko hayo.
Chama pia kina jukumu la kutunza kwa miaka isiyopungua mitano kumbukumbu zifuatazo:-
1.   Orodha ya wanachama katika fomu maalumu.
2.   Mihtasari ya Vikao.
3.   Karatasi za kura.

Chama cha Wafanyakazi kinapaswa wakati wote kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa katiba, kanuni na mazoea. Endapo itatokea chama kimeshindwa kuzingatia katiba yake, msajili au wanachama wanaweza kupeleka maombi mahakama ya kazi kutengua suala hilo lililofanyika kinyume na katiba.
Kabla ya maombi hayo kupelekwa mahakamani, taratibu za ndani ya chama ni lazima zifuatwe kwanza. Isipokuwa ikiwa ni kwa maslahi ya chama, basi maombi hayo yanaweza kupelekwa mahakamani bila kufuata utaratibu wa ndani wa chama.
HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI MAHALI PA KAZI.
Chama cha Wafanyakazi kilichosajiliwa kina haki zifuatazo mahali pa kazi:-
1.   Haki ya kuingia eneo la muajiri – kwa lengo la kusajili wanachama, kuwasiliana na wanachama, kufanya vikao na wanachama, kuendesha uchaguzi. (Kifungu cha 60 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya mwaka 2004).
2.   Makato ya Ada – kupokea ada za wanachama baada ya muajiri kuwakata kutoka kwenye mishahara yao. (Kifungu cha 61 cha Sheria ya Ajira).
3.   Kuwa na wawakilishi wake mahali pa kazi – chama cha wafanyakazi kinayo haki ya kuwa na wawakilishi mahali pa kazi kwa kuzingatia idadi ya Wanachama kama ifuatavyo:-
a)    Wanachama wasiozidi tisa (9) – muwakilishi mmoja.
b)   Wanachama kuanzia kumi (10) mpaka ishirini (20) – wawakilishi watatu.
c)    Wanachama kuanzia ishirini na moja (21) mpaka mia moja (100) – wawakilishi kumi.
d)   Wanachama zaidi ya mia moja (100) – wawakilishi kumi na tano, miongoni mwao watano lazima wawe wanawake kama wapo na ni wanachama.
MAJUKUMU YA WAWAKILISHI WA CHAMA MAHALI PA KAZI.
1.   Kuwawakilisha wanachama kwenye vikao vya kushughulikia malalamiko na nidhamu.
2.   Kuwasilisha hoja kwa niaba ya wanachama kuhusiana na kanuni, afya, usalama na ustawi wao.
3.   Kushauriana na muajiri kuhusu tija mahali pa kazi.
4.   Kukiwakilisha chama wakati wa ukaguzi na uchunguzi unaofanywa na wakaguzi kwa mujibu wa sheria yoyote ya kazi.
5.   Kuhakikisha kazi za chama kwa mujibu wa katiba ya chama.
6.   Kuendeleza uhusiano mzuri kazini.
7.   Kutekeleza majukumu waliokubaliana na muajiri.
Wawakilishi wa chama wanayohaki ya kupewa muda wa kutosha kutekeleza majukumu yao bila kukatwa mshahara na wanayo haki pia ya kupewa na muajiri taarifa zote muhimu zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Haki hizi zitatolewa na kutekelezwa vizuri bila kuvuruga kazi.
LIKIZO KWA WAWAKILISHI WA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Wawakilishi wa chama mahali pa kazi wanayo haki ya kupewa likizo ya malipo na muajiri kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo yanayohusiana na majukumu yao. Hali kadhalika viongozi wa chama cha wafanyakazi na wa shirikisho ambalo chama ni mwanachama, wanayo haki ya kupata likizo ya malipo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya chama au shirikisho.
UTARATIBU WA KUPATA HAKI ZA CHAMA.
Chama cha Wafanyakazi kilichosajiliwa kutekeleza haki za chama, kinapaswa kumtaarifu muajiri kwa kujaza fomu CMA F3 kikianisha haki ambazo kinataka kuzitekeleza pamoja na mahali pa kazi ambapo kinataka kuzitekeleza haki hizo.
Muajiri akishapokea fomu hizo anapaswa kukutana na chama ndani ya siku 30 ili kufikia makubalianao ya pamoja yatakayotoa haki hizo, na kuweka utaratibu wa kuzitekeleza. Endapo hakutakuwepo makubaliano au muajiri atashindwa kukutana na chama ndani ya muda uliowekwa, chama kinaweza kupeleka mogogoro huo mbele ya Tume kwa ajili ya usuluhishi.
Usuluhishi ukishindikana chama kinaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi kwa uamuzi.
USITISHAJI WA HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Haki za chama zinaweza kusitishwa iwapo chama kitakiuka makubaliano ya msingi ya utoaji haki hizo au kwa amri ya mahakama inayotoa haki hizo.
Ikitokea hali hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano, muajiri anaweza kupeleka mgogoro huo mbele ya Tume kwa ajili ya usuluhishi. Usuluhishi ukishindikana, muajiri anaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi akiiomba Mahakama isitishe makubaliano ya kutoa haki hizo au iondoe amri yake ya kutoa haki hizo
HITIMISHO.
Mara nyingi katika maeneo ya kazi kumekuwa na migogoro mingi sana inayohusu masuala ya haki za vyama vya wafanyakazi. Waajiri kwa kutokujua au kwa makusudi wamekuwa wakikataa kutoa haki za chama kwa wafanyakazi wanachama wa vyama vya wafanyakazi. Hali hii imekuwa ikipelekea kuibuka kwa migogoro hiyo ambayo huatarisha mahusiano mazuri kati ya muajiri na wafanyakazi.
Mara nyingine wanachama wamekuwa wakizitumia haki zao vibaya katika maeneo yao ya kazi, jambo ambalo pia linamfanya muajiri kutoridhika na hali hiyo ambapo pia hupelekea migogoro ya kikazi kuibuka.
Makala hii imelenga kutoa ufafanuzi na uelewa juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Vyama vya Wafanyakazi na Haki zilizomo kwa pande zote mbili (muajiri na wafanyakazi). Aidha imeainisha majukumu ya chama na wanachama kwa ujumla.
Ni matumaini yangu kuwa itasaidia kutoa uelewa kwa wadau wa sekta ya ajira, hasa waajiri na wafanyakazi na hivyo kusaidia kupunguza migogoro ya kikazi na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wadau hao.
Imeandaliwa na Emmanuel C. Zongwe kwa msaada wa vitabu mbalimbali, mitandao na uelewa binafsi katika masuala ya Ajira na Mahusiano Mahala pa Kazi.

Simu: +255 (0) 717 058 045/ +255 (0) 755 223 697

E-mail: ezongwe@yahoo.com

Imetolewa na 
Jielimishe Kwanza.