Picha na shutterstock |
Biashara iendeshwayo na
Makampuni ya Kimtandao almaarufu kama “Multi-Level
Marketing (MLM) Companies” imeshamili na kuwa ni gumzo kwa takribani zaidi
ya muongo mmoja katika nchi zinazoendelea (Afrika- Kenya, Nigeria, Ghana,
Zimbabwe, Namibia, Afrika Kusini….), ingawaje tafiti zinaonyesha kuwa
ilianza kwa mara ya kwanza miaka ya 1940s nchini
Marekani. Hivyo basi biashara hii si mpya kama wengi wanavyofikiria
na kuwaaminisha wengine. Nchini
Tanzania kampuni nyingi za MLM huingia nchini kupitia nchi ya Kenya, nisingependa
kuzianisha,; unazifahamu na yawezekana nawe upo huko na umekwisha jijengea fikra
ya “be your own boss” kwa kuwatoa wengine
sadaka kama wasambazaji ili ufaidike kwa kupanda cheo kupitia ngazi (levels) mbali mbali kama zilizokubaliwa na kampuni unayoitumikia.
Kutokana na ukimya na
sintofahamu nyingi kuhusu uwepo na gharama kubwa katika bidhaa zinazosambazwa
kupitia MLM, Jielimishe Kwanza Blog tumeona
ni vyema tuvunje ukimya huu kupitia kufanya utafiti wa kina kuhusu Makampuni
yanayojihusisha na MLM na kukushirikisha.
Makampuni hayo yanayojihusisha
na biashara ya Kimtandao hutengeneza na
kuuza bidhaa wanazoziamini sana na kuwaaminisha wengine kuwa zinatibu magonjwa sugu,
kuboresha kinga ya mwili, kuthibiti uzito na mwisho wa yote ni ahadi kem kem za maisha bora
yenye uhuru wa kipato na ile ya “kumiliki biashara yako mwenyewe”.
Swali la msingi ambalo kila Mtanzania anapenda kujua ni hili la kuwepo kwa gharama kubwa ya bidhaa
zinazozalishwa na makampuni ya MLM. Kupitia utafiti binafsi wa Jielimishe Kwanza Blog! umebaini
yafuatayo;
Tracy
Coenen- mtaalamu wa masuala ya Intelijensia na upelelezi wa masuala ya biashara anasema kuwa; "The truth is that products are overpriced
through multi-level marketing companies because they have to pay commissions to
distributors on many levels." That’s the whole point of multi-level marketing:
Many levels of distributors get a piece of the action when you buy something. Akimaanisha kuwa, gharama kubwa husababishwa
na kuwalipa bakshishi/sehemu ya faida ya mauzo wasambazaji
walio wanachama wa Kampuni husika.Pia huwalipa kutokana na
kuwashawishi wengine kutumia na kujiunga na Kampuni husika. Bila shaka umewahi
kusikia kuwepo kwa makampuni hayo hapa kwetu Tanzania yakihamasisha wengine kujiunga nao kupitia bidhaa zao, na yawezekana u mmoja
wao.
Kutokana na maelezo na mafundisho
yao, husingizia kuwa bidhaa zao ni bora zaidi kuliko bidhaa nyingine
duniani…yaani ni kama zimeshushwa kutoka mbinguni.Tuwe na uhalisia katika hili!
Imefika wakati wa kufumbuka
macho Watanzania, tusitamanishwe na mafanikio hewa kwa kutumika na wengine. Hakuna urahisi unaopatikana katika biashara
hizo hasa unapoaminishwa kuwa utakuwa na uhuru wa kipato na kumiliki biashara
yako mwenyewe…Biashara yako mwenyewe?...wakati unawekewa masharti na watu
wengine? Mfano: hakikisha unaingiza watu 2 kwa wiki, kununua na kutumia bidhaa
ndipo upate gawio la faida.Cha kusikitisha zaidi huwezi kujiunga na
Makampuni hayo na kupata gawio la faida kubwa kama hujanunua bidhaa kwa gharama
kubwa, kuuza bidhaa zao kwa bei waliopanga na kushirikisha wengine wajiunge kwa
kuwahamasisha na kuwaaminisha kama ulivyoaminishwa kuwa zitawatoa pale walipo kimaisha. Kuhamasisha
wengine wajiunge ni silaha kubwa katika kampuni hizo. Usipofanya hivyo hutaona faida ya biashara hii na mwisho wa siku itakushinda!
Robert FitzPatrick mwandishi wa “Pyramid
Scheme Alert” pia mtafiti wa masuala ya biashara za mtandao (MLM) anaweka
bayana kuhusu suala zima la kuhakikisha wengine wanajiunga katika kampuni ndipo
mhusika apate gawio la faida litokanalo na gharama
kubwa ya kila bidhaa; “For there to
be a “winner” at the top, there must be “losers” below. The ratio of losers to
winners is pre-determined, usually 100 to 1.” Profit Reserved only for those at
the Top. Hivyo katika wengi (watu 100) waliohamasishwa na kujiunga kama
wasambazaji anayefaidika zaidi ni mtu 1 tu! Yaani, ili mtu mmoja ayaone mafanikio ya kweli ndani ya kampuni ni lazima watu 100 chini yake wapate hasara. Huu ni ukweli mchungu ambao
hufichwa na washiriki wa makampuni hayo. Ndiyo maana kila kukicha wanawaza
kuingiza watu wapya katika kampuni. Ki uhalisia utafanikiwa kwa kuwekeza zaidi
muda wako na pesa nyingi katika kampuni hizi ili upate mafanikio si kutokana na kupendwa
sana na Makampuni yao, ila ni hela na muda uliowekeza kuisaidia kampuni
kutimiza malengo yake. Ndiyo maana tunapingana vikali na dhana ya kusema kuwa “be your own boss” katika biashara hii.
Siri kubwa ya makampuni hayo
ni wewe kuhakikisha unahamasisha wengine wajiunge kuwa wasambazaji na watumiaji
wa bidhaa zao ndipo ulipwe…hii si kazi rahisi kama wanavyoeleza na kurahisisha
katika mafundisho yao.
Nasisitiza tena, Watanzania
tufumbuke macho, tusome, Tujielimishe Kwanza kabla ya kutaka kupapatikia biashara
zinazoonekana kuwa na mteremko ilihali hatujui yaliyojificha; mbele kukiwa na
mlima mkubwa unaolighalimu taifa katika siku za usoni.
Chaguo
ni lako, kujiunga au kutokujiunga na Makampuni hayo.Ukitaka kutoka nayo
kimaisha, wekeza zaidi muda na pesa yako, hamasisha wengine wakubali kujiunga.
Pia
kuwa makini; kuna bidhaa kama za Makampuni ya MLM zina gharama nafuu sana na
zinafanya kazi vizuri na zina ubora zaidi ya hizo za MLM.
Usidanganyike na urembo au madoido ya vifungashio vya bidhaa hizo, zipo kama kivuli cha kuficha ujanja ujanja unaofanywa na wamiliki wa Makampuni ya MLM.
Huo ndiyo ukweli unaofichwa ili kuneemesha wengine.
Huo ndiyo ukweli unaofichwa ili kuneemesha wengine.
Ukiwa na maoni, manung’uniko na kuhitaji
ufafanuzi zaidi usisite kutuandikia.
Imetolewa na,
Jielimishe Kwanza!