Ni jambo jema kuwa na
mipango au malengo yenye mikakati madhubuti ya utekelezaji na si kuwa na malengo pekee, ingawa ni bora
kuwa nayo kuliko kutokuwa nayo kabisa; kwa kuwa na malengo pekee bila mkakati wa
utekelezaji ni sawa na matamanio-alisema Joel Osteen katika moja ya mafundisho
yake. Dhana hii imeelezwa kwa kina katika mojawapo ya makala zilizosheheni
ndani ya Jielimishe Kwanza!Blog ikiwa na mtazamo chanya kabisa wa kuchochea
mabadiliko yenye chachu ya utekelezaji usiyokuwa na hofu ya kukata au
kukatishwa tamaa na hatimaye kuishia njiani.
Ingawaje inaonekana
ni rahisi kujiwekea malengo au mipango mbali mbali ya maisha na ya Taifa kwa
ujumla ila msisitizo unawekwa zaidi na unaendelea kuwekwa katika kuhakikisha kuwa kuna utekelezaji! Na ikijitokeza kuwa kuna
changamoto za kukamilisha malengo yaliyo katika hali ya utekelezaji; watu au
wanajamii wengi huchukua uamuzi mrahisi mno wa kuachana na mbio za kuyafikia
mafanikio tarajiwa.
Leo, naomba nikutie
moyo ndugu msomaji kwa kuikumbuka historia isiyoweza kufutika duniani ya
mwanariadha John Steven Akwari -kijana wa kitanzania ya mwaka 1968 kule Mexico
kwenye mashindano ya Olimpiki. Akwari aliushangaza ulimwengu kwa kuendelea na
mbio akiwa mtu wa mwisho ili kuhakikisha anamaliza safari yake licha ya kuwa na
jeraha lenye bandeji mguuni kwake. Hiyo haikutosha, alishangaza zaidi na
kuwahamasisha waliokata na wanaokata tamaa kupitia changamoto zisizotarajiwa
kwa kusema kirahisi “ Nchi yangu
haikunituma maili 5000 kuanza mbio, bali
ilinituma maili 5000 kumaliza mbio; alitoa jibu hili kwa ujasiri pale alipoulizwa kwanini hakuachana na mashindano
mara tu alipopata jeraha.
Ama kwa hakika, tukio
hilo la kihistoria na maneno ya Akwari yanahamasisha na yanachochea uwajibikaji
usio dhaifu, wenye kujali uzalendo, wenye shauku ya kufikia mafanikio, pia
kipimo cha utu wa mwanadamu pale kutokeapo changamoto au vipingamizi katika
kufikia kiu ya mafanikio.
Hivyo basi ndugu
msomaji ni vyema kuhakikisha malengo uliyojiwekea yakiwa na mpango mkakati bila
ya kukata tamaa ukiwa katikati ya mbio za kuelekea mafanikio.Hakikisha
unaimaliza safari yako kuelekea mafanikio licha ya kuwepo changamoto au
vipingamizi vya hapa na pale.
Imetayarishwa na
Henry Kazula,
Mwandishi wa Kitabu-MTAZAMO WAKO NI UPI?
Na kutolewa na
Jielimishe Kwanza!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni