Leo imekuwa ni siku ya kilele cha mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana-wahitimu wa vyuo vikuu mbali mbali nchini.
Mafunzo hayo yaliyowashirikisha vijana 40, yameongeza chachu kwa vijana hao hasa katika kuwajengea uwezo wa kuandika mipango ya kibiashara,uwezo wa kujiajiri na kuweza kuajiri wengine.
Kwa kushirikiana na chuo kikuu Dar es salaam, kitengo cha ujasiriamali, Baraza la uwezeshaji la Taifa kiuchumi limeweza kufanikisha mafunzo hayo na kuwatunuku wahitimu 40 vyeti katika Hotel ya Blue Pearl Hotel, ukumbi wa Crystal Hall-Ubungo Plaza, jijini Dar es salaam leo.
Zoezi hilo liliambatana na utolewaji wa zawadi kwa washiriki watatu(3) waliofanya vizuri katika zoezi la uandikaji miradi ya biashara.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, akiwa mgeni rasmi alipewa nafasi kuwatunuku vyeti wahitimu hao na zawadi kwa washindi watatu(3) ambao ni Bw. Anthony Seleli Mhanda aliyepata sh.milioni 10, Bw. Ale Alex Kaaya aliyepata sh.milioni 8 na , Bi Selina Julius Otacho aliyepata sh. milioni 6.
Mwisho kabisa Dr. Nagu alitoa hotuba fupi kwa wahitimu na umma kwa ujumla wake.Aliwapongeza wahitimu kwa kuthubutu kuchukua uamuzi wa kujiajiri na ofisi yake haitawaacha, itashirikiana nao kuhakikisha mafunzo waliyoyapata yanazaa matunda.
Aliainisha kuwa, katika nchi yetu kuna makundi matatu ya mifumo ya kujipatia mkate wa kila siku; kundi la kwanza ni la watanzania wanaobangaiza bangaiza-wanabahatisha maisha, la pili ni lile la waajiriwa na wachacharikaji ingawaje kipato chao ni kidogo na hakikidhi, kundi la tatu ni la wajasiriamali-kundi hili lina watu wachache, ni watu wenye kuona fursa na kuzitumia ikiwa sambamba na kutengezea vyanzo vingine vya ajira.
Alishauri kuwa, imefika wakati kwa watanzania kuhamia katika kundi hili la tatu ambalo linakwenda kuongeza idadi ya ajira na kukuza uchumi wa kila mtu na si kutegemea kukua kwa uchumi wa Taifa. Akimaanisha kuwa; uchumi wa mtu mmoja ukikua, wa Taifa utakua.
Ilitaadharisha kuwa kukua kwa uchumi wa Taifa si kiashiria kizuri cha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja.Hivyo watu wasijidanganye na kutegemea kukua kwa uchumi wa Taifa ila inapaswa wananchi wenyewe, mmoja mmoja achukue jukumu la kukuza uchumi wake ili uchumi wa Taifa ukue.
Dr.Nagu alikazia kwa kusema; ukosefu wa ajira kwa vijana nchini unatokana na kutegemea kuajiriwa katika sekta rasmi...
PICHA NA MATUKIO:
Washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali wakiwa katika ukumbi wa mkutano |
Henry Kazula, akitunukiwa cheti cha mafunzo ya ujasiriamali |
Waziri, Dk.Mary Nagu akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali |
Waziri, Dk.Mary Nagu akijadiliana na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali |
Henry Kazula (wa kwanza kutoka kushoto), akiwa na wahitimu wenzake |
Imeandikwa na Henry Kazula,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni