Picha imetolewa www.alidavies.com |
Wataalamu wa masuala ya uchumi na biashara wamemtambua mtu
aitwaye mjasiriamali kuwa ni mtu anayechukua hatua ya uthubutu wenye tija, ulio na uwezekano wa hatari bila
hofu ya kupoteza.
Pia yupo tayari kwa lolote litalotokea ilihali ana nia ya
kutumia fursa iliyopo kujiongezea kipato chake na ikiwezekana kutengeneza
milango ya fursa ya kipato kwa wengine.
Kuna sababu mbali mbali zinazowafanya vijana kuchukua muda
mrefu, hasa katika suala zima la uthubutu; hofu ya kupoteza kile kidogo walicho
nacho,hofu ya kukataliwa na kutengwa na marafiki au ndugu, kutegemea faida ya
papo kwa hapo(wengi si wavumilivu wa mafanikio…kila mmoja anataka mafanikio ya
haraka).
Swali, tunatokaje hapo tulipo kuelekea kwenye hatua a
uthubutu wenye tija unaoendana na ujasiriamali?
Kabla ya kutoa mbinu za kutumia ili kufanikiwa kwenye
uthubutu wenye tija ni muhimu kufahamu kuwa suala la uthubutu linaambatana na
kukutana na uwezekano wa hatari, kwa lugha ya Kiingereza hujulikana kama “risk”.
Hivyo,ni muhimu kujifunza jinsi ya
kupunguza uwezekano wa hatari hizo.
Daktari maarufu wa masuala ya ubongo na neva za fahamu,
nchini Marekani-Dk.Ben Carson, katika kitabu chake cha
“Take The Risk” ameainisha njia ya kufuata kuelekea kuchukua hatua
ya uthubutu wenye uwezekano wa hatari.
Awali ya yote, amesema “katika maisha
kila kitu kina uwezekano wa hatari ndani yake”…mfano mdogo tu, unapotembea kuna
uwezekano wa hatari kutokea, unaweza kugongwa na gari, baiskeli,guta,pikipiki
au ukiwa unaendesha gari kuna uwezekano wa kupata ajali.Uwezekano wote huu wa
kupata hatari hauwafanyi watu kuacha kutembea kwa mguu au kuendesha au
kuendeshwa kwenye magari.
Dk. Carson ameainisha njia mbili lakini ni nne ndani yake
zilizo sanjali na kujiuliza maswali;
·
Ni kitu gani kizuri kitatokea kama nikifanya?
·
Ni kitu gani kizuri kitatokea kama nisipofanya?
·
Ni kitu gani kibaya kitatokea kama nikifanya?
·
Ni kitu gani kibaya kitatokea kama nisipofanya?
Kwa uzoefu na umahiri wake katika upasuaji wa ubongo na
neva za fahamu Dk.Carson amekuwa akitumia njia hii ya kujiuliza maswali hayo
manne.Pia, unaweza kuyatumia maswali haya katika mazingira mbali mbali yanayohusu kutoa maamuzi magumu.
Hivyo basi msomaji ni vizuri kujiuliza na kupata majibu ya
maswali yote manne kabla ya kutoa maamuzi yaliyo katika njia panda.
Jielimishe Kwanza!
Tenda! Ishi Ndoto!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni