Picha na blog.readytomanage.com |
Maisha yenye
mafanikio ni yale yanayotawaliwa na malengo halisia yanayoambatana na
utekelezaji katika wakati husika.
Nikimnukuu mwandishi wa vitabu maarufu Norman
Vincent Peale anasema;
“A goal is a dream with a
deadline” kwa lugha ya Kiswahili “lengo ni
ndoto yenye kikomo cha wakati.”
Kwa mtazamo
mwingine mwandishi na msemaji wa hadhara maarufu nchini Marekani Joel Osteen
anasisitiza kuwa ndoto ni lazima iwe na mpango mkakati; “ A dream without a plan ends up as a wish”- “Ndoto bila utendaji
unaofuata mpango mkakati ni sawa na matamanio tu.”
Ikiwa una
malengo pekee bila mpango mkakati haisaidii, cha msingi ni kuwa na malengo yaliyo
kimaandishi na mpango mkakati kuyafikia malengo yako.
Watu wengi huwa na ndoto nzuri zilizo katika hali ya shauku na matamanio pekee.Hii ni kwa
sababu hawana/wamekosa mpango mkakati wa kufanikisha ndoto zao.
Hili ni tatizo
kubwa linalowafanya watu kuwa katika hali ile ile ya maisha kwa miaka mingi.
Jielimishe Kwanza! imewahi kuwauliza watu wa makundi tofauti kama wana malengo...iligundulika kuwa watu wengi hushindwa kuyapangilia malengo yao kwa kuzingatia kiwango cha muda wa utekelezaji.
Mfano, mtu mmoja alisema anataka kumiliki chuo binafsi...alipoulizwa amechukua hatua zipi kuanza kutekeleza lengo lake...alishindwa kueleza.
AINA ZA MALENGO
Mwandishi na mhubiri maarufu nchini Marekani Joel Osteen ameainisha aina
mbili za malengo; 1) Malengo ya muda mrefu 2) Malengo ya muda mfupi
1)Malengo ya muda mrefu
Malengo haya huchukua miaka 10-20 kukamilika.Kama nilivyosema awali ni
vyema kuandika malengo yako na kujiwekea mpango mkakati.
2)Malengo ya muda mfupi
Malengo haya ni yale unayoyafanyia kazi kwa sasa.Faida ya malengo haya
ni kukufanya usheherekee ukiwa kwenye safari ya kuyafikia malengo makubwa/ya muda
mrefu.Pia hukupatia ari ya kusonga mbele kuyafikia malengo ya muda mrefu.
Kiundani tuangalie mbinu 10 zinazoweza kukuondoa hapo ulipo ili ndoto zako zilizo katika malengo
zitimie na kuzaa matunda.
1.ANDIKA MALENGO YAKO KWENYE KITABU MAALUMU
Usipuuze hata kidogo kuandika malengo yako na kuwa na mpango mkakati wa
kuyafikia.
2.USIWEKE MALENGO MAKUBWA YASIYO HALISI
Jitahidi kuweka malengo yaliyo kwenye uwezo wako.Unaweza ukawa na picha
kubwa ya maono lakini unaweza kuanza kidogo kidogo.Mfano mtu hawezi kusema ana lengo la kumiliki gari la kifahari wakati hata kula yenyewe ni ya shida.
3.HUSISHA MALENGO MAPYA NA ULIYONAYO KWA SASA
Kuna faida kubwa ya kuhusisha malengo ya sasa na yajayo, hapa unaweza kujipima uwezo wako kiutendaji katika kuyafikia malengo mapya.
4.JIKITE KWENYE MALENGO YENYE FAIDA ZA HARAKA
Ni vizuri kujiwekea vipaumbele katika malengo unayojiwekea ukizingatia faida za haraka ili upate ari ya kuyafikia malengo makubwa.Jiulize: Malengo ninayojiwekea yana faida za haraka kwa sasa?
5.ONGELEA MALENGO YAKO KATIKA HALI CHANYA
Hii itakupa ari ya kuyafanyia kazi malengo yako.Utajiona ni mtu wa kufanikiwa kila siku katika malengo yako (ya muda mfupi hata yale ya muda mrefu).
6.JIWEKEE MPANGO MKAKATI KUFANIKISHA MALENGO
Jiulize:Je ninazo taarifa? Nahitaji taarifa zipi? Je kuna mbinu na ujuzi
ninaotakiwa kujifunza?
7.YAGAWE MALENGO YAKO KATIKA HALI YA UTEKELEZAJI
Inafika wakati mtu anakuwa na malengo makubwa kupita uwezo wake wa kutekeleza.Ni vyema kabisa kuyagawa katika hatua ndogo ndogo ili mwisho wa siku ulifikie lengo kubwa ulilojiwekea.
8.TAMBUA KUWA KUYAFIKIA MALENGO YAKO SI LAZIMA UPITIE SHIDA NA KUJITOA MHANGA
Kuna kasumba iliyozoeleka kwa watu wengi eti ili uyafikie malengo ni lazima upate shida sana.Hii si kweli, bali watu hupenda kuongelea vitu kwa ujumla sana wakati kuna malengo yanaweza kutimia kwa kujipanga vizuri na kujikita kikamilifu.
Ndugu msomaji, ukifikiri kwa mtazamo kama ilivyo kasumba ya watu wengi utakata tamaa na hutajiwekea malengo hivyo kuishi maisha ya "...bora kumekucha..." "...ya leo ni afadhali ya jana..."
9.EPUKA KUWAAMBIA WATU WENYE MTAZAMO HASI MALENGO YAKO
Watu wanaokuzunguka ni wengi, na kila mmoja ana mtazamo wake.Utaniuliza, nitawajuaje?
Kuna msemaji wa hadhara na mhubiri na mwandishi wa vitabu Joyce Meyer aliwahi kusema; ukitaka kujua mtazamo wa mtu msikilize
maneno yake…Hivyo basi ni vyema kuwa muangalifu wakati wa kuchagua aina ya marafiki unaweza kuwashirikisha malengo yako.
10.USIKUBALI KUYUMBISHWA NA MTU, NG'ANG'ANIA MALENGO YAKO
Mafanikio ya malengo yako yanaanzia na wewe kifikra, kimtazamo na kiutendaji.Ukifanya kosa la kumwachia mtu mwingine asimamie na kukuendeshea malengo yako hutapiga hatua stahiki. Itambulike kuwa, si watu wote wana nia njema na malengo yako.Wapo wengine wanaotaka usiyafikie malengo uliyowaambia.
Jifunze kutokana na makosa.Tumia makosa yaliyofanyika awali kuwa changamoto na ujifunze kufanya vizuri ili utimize malengo yako kwa mafanikio makubwa.
Je, una malengo yasiyo na ufumbuzi au huna malengo yoyote? Tumia mbinu
tajwa katika makala hii kubadilika na kuwa mtu mwenye malengo yenye tija.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!