Kumekuwa na msemo uliozoeleka na kuaminika na watu kuwa "raha ya pesa ni matumizi" au "tumia pesa ikuzoee" ... ni kweli kabisa pesa inaendana na matumizi lakini ni vyema kuweka angalizo: zingatia aina ya matumizi unayofanya.
Jiulize "Je, matumizi ninayofanya yanakwenda kubadilisha maisha yangu na kunifanya niwe na fedha zaidi au yananipelekea kwenye umasikini wa kutupa?
Watu wengi wanajishangaa...wanapata fedha nyingi lakini hawaelewi zinakokwenda huku wakati huo huo ndoto zao hazitimii na hali zao za maisha zikizidi kuwa duni bila mabadiliko kila mwaka.
________________________________________
Kama huelewi fedha zako zinakokwenda fanya yafuatayo:
1.EPUKA MADENI
Jaribu kufuatilia kwa karibu ni kiasi gani
cha pesa kinaenda kwenye madeni utapata jibu kuwa ukiyaepuka madeni utaiona
pesa yako.Hii ni njia ya haraka ya kuhifadhi pesa yako
2.JIWEKEE MPANGO WA KUTUNZA PESA
Ni rahisi sana kufanya mpango huu kwa malengo
ya muda mfupi.Mfano unataka kununua samani za ndani, fuatilia na ujue
itakugharimu kiasi gani cha fedha.
Pia kama unataka kununua au kujenga nyumba
fanya utafiti na ujue itakugharimu kiasi gani cha fedha kwa nyumba
unayoitaka...ni muhimu uwe na ramani ya nyumba yako mapema itakusaidia kukokotoa
gharama ya nyumba, hivyo kuanza mpango wa kutunza fedha, mwishowe kuanza kwa
hatua moja hadi nyingine.
Kwa malengo ya muda mrefu hasa kustaafu,
inabidi ujue na ufanye mpango yakinifu kujua ni kiasi gani cha fedha utahitaji
kukufanya uishi bila kutegemea watoto kwa kipindi cha miaka 20-30 baada ya
kustaafu au kuacha kufanya kazi, pia unatakiwa kujua aina ya uwekezaji
utakaotimiza malengo yako.
3.WEKA KIKOMO CHA MUDA KUTIMIZA UHITAJI WAKO
Mfano: Unaweza kusema kwa dhati kuwa “Nataka
kununua gari ndani ya miaka miwili kuanzia sasa”.
Weka kimaandishi siku maalumu kwa tarehe
kutimiza malengo ya muda mfupi na uhakikishe malengo yako yanafikiwa ndani ya
muda husika.
Ujue fika kuwa usipoweka lengo linaweza kufikiwa utakata tamaa
hivyo kutumia pesa ovyo kwa kitu ukipendacho kwa wakati husika bila ya kupanga.
4.JICHUNGUZE NI KIASI GANI CHA FEDHA
UNATAKIWA KUTUNZA KWA WIKI,MWEZI AU KWA KILA MSHAHARA KUTIMIZA MALENGO YAKO
Ainisha vitu unavyovitaka na gharama yake,
hivyo amua ni kiasi gani cha fedha unatakiwa kutunza kuanzia sasa.
Kwa
mafanikio mazuri ni vizuri kutunza kiwango kile kile cha pesa kwa muda
uliojipangia. Mfano: Unataka kulipia kodi ya nyumba Shilingi 1,800,000 kwa
mwaka, utahitaji kujiwekea akiba ya Shilingi 150,000 kwa kila mwezi.
Kuanzia
hapo linganisha na kipato chako kwa mwezi, kama nacho ni Shilingi 150,000 kwa
mwezi itakuwa vigumu sana kutimiza mahitaji mengine ya msingi.
5.WEKA KUMBUKUMBU YA MATUMIZI YAKO
Jichunguze umetumia kiasi gani cha fedha na
umeingiza kiasi gani fedha kwa siku au mwezi kwa maandishi.Jitahidi kuwa makini
uwezavyo kujichunguza matumizi yako na usipuuze wala kuacha kuandika matumizi
madogo.Ukiweza kusimamia matumizi yako, utakuwa makini sana na pesa yako.
Tenga kwa makundi kama Kodi ya pango,Bima ya
gari, nauli,gharama za simu,gesi,chakula,burudani, gharama za ving’amuzi na
mengineyo.
·
Jiwekee utaratibu wa kutembea na kidaftari
kidogo kwa ajili ya kumbukumbu zako za matumizi.
·
Mwisho wa wiki kaa,tulia,tafakari na uchukue
risiti za manunuzi na hamisha kumbu kumbu za matumizi yako kwenye daftari
kubwa la matumizi
·
Pia unaweza kutumia simu yako kutunza kumbukumbu
za matumizi yako
6.EPUKA MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA
Ukichunguza vizuri matumizi yako kwa wiki au
mwezi utashangaa mwenyewe kuona kuwa kuna wakati umefanya matumizi yasiyo ya
lazima…ambayo hayakuwepo kabisa kwenye mpango wako.
Ukilinganisha na kiasi cha
fedha unachohitaji kwa malengo uliyojiwekea unaweza kufanya maamuzi magumu ya
kujibana kimatumizi.Fikiria sana vipaumbele vya malengo yako.
7.CHUNGUZA LENGO LAKO LA KUJIWEKEA AKIBA
Unaweza kufanya hesabu rahisi kwa kutoa
gharama za matumizi kutoka kwenye kipato chako halisi(baada ya makato mbali
mbali …kama ni mwajiriwa).Vipi tofauti yake? Je inashabihiana na lengo la
kujiwekea akiba?
8.ANDIKA BAJETI YAKO
Ukifanikiwa kusawazisha kipato chako na
malengo yako ya kujiwekea akiba na matumizi andika bajeti itakayokuwezesha
kujua kila mwezi ni kiasi gani cha fedha utatumia.
9.USILIPE KWA MKOPO, WALA KWA KUTUMIA
“CHECKS”-LIPA FEDHA TASLIMU!
Ni rahisi sana kuongeza matumizi zaidi ya
malengo yako kwa mtindo wa mkopo.
Ukilipa pesa taslimu utaona jinsi mfuko wako
unavyopungua hivyo ni rahisi kujidhibiti na matumizi yako.
10.FUNGUA AKAUNTI YA AKIBA YENYE ZAO LA FAIDA
Ni vyema kuwa na akiba inayotengeneza faida
kwa kipindi fulani cha muda.
11.KUWA WAKWANZA KUJILIPA
Katika kipato chako usisahau kujipa mwenyewe
hasa kwa jitihada zako, muda uliotumia kuzalisha.Hii ni njia nzuri kwa
wafanyabiashara, mara nyingi hujisahau kabisa kuwa jitihada zao na muda
waliotumia ni wa thamani sana hivyo wanapaswa kujilipa kwanza.
12.USIFANYE “WINDOW-SHOPPING” UKIWA NA PESA
MFUKONI
Utajikuta umetamani kitu fulani na
kushawishika kununua bila ya kuwa na malengo ya awali.
13. USIKATE TAMAA, ANZA SASA!
Jiamini kuwa unaweza kufikia malengo yako na
kuwa mtu mwenye fedha nyingi kwa kujikita kikamilifu katika suala zima la
kujiwekea akiba.
Kama Waswahili wasemavyo; mambo mazuri
hayataki haraka-wakimaanisha huchukua muda hivyo basi jinsi unavyojiwekea akiba
ndivyo faida inavyokuwa kubwa na utajiri kukunyemelea.
Makala inayohusiana:
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!