inspire

inspire

Lebo

AFYA (8) AJIRA (5) BIASHARA (39) ELIMU (14) MAHUSIANO (2) MALEZI (16) MAZINGIRA (12) SAIKOLOJIA (48) VIJANA (7)

Business registration

Green Consulting

business consultancy

business consultancy

Business consulting-2

Business consulting-2

Professional Consulting

PDC

Swahili translator

Swahili translator

TANGAZO-KITABU

E-BOOK: MTAZAMO WAKO NI UPI?

TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- .... TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- ....

TANGAZO TUWEZESHANE

TANGAZO TUWEZESHANE

DARDY'S INVST-20/10/2017

DUNIA IKUONE

DUNIA IKUONE

Alhamisi, 21 Mei 2015

AJIRA: UHURU WA KUUNDA NA KUJIUNGA NA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

-->
Picha na www.eventbrite.ca

UTANGULIZI.
Uhuru wa kujumuika unawapa wafanyakazi uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Vilevile unawapa wafanyakazi haki ya kushiriki katika shughuli za vyama vyao kwa uhuru bila hofu ya kubaguliwa au kunyanyaswa au kupoteza haki yoyote.
Hata hivyo, uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi una mipaka yake. Uhuru huu umewekewa mipaka kwa wafanyakazi wa kada zifuatazo:-
a)    Mahakimu – hawa wanaweza kuunda na kujiunga na Chama cha Maafisa wa Mahakama pekee.
b)   Waendesha Mashitaka – hawa wanaweza kuunda na kujiunga na chama cha Waendesha Mashitaka au Watendaji wengine wa Mahakama pekee.
c)    Wafanyakazi wa kada ya Meneja Mwandamizi ambaye kwa nafasi yake ana mamlaka ya kutengeneza sera kwa niaba ya muajiri na ana mamlaka ya kuingia majadiliano na Chama cha Wafanyakazi, haruhusiwi kujiunga na Chama cha Wafanyakazi wasio Mameneja Wandamizi.
Pia uhuru wa kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyakazi unatoa kinga ya mfanyakazi kutobaguliwa na mtu yeyote kwa sababu ya kuwa mwanachama wa chama cha wafanyakazi au kujihusisha na shughuli halali za chama.
HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
1.   Kuwa na Katiba yake bila kuingiliwa na dola, chama cha siasa au muajiri.
2.   Kupanga na kuendesha mambo yake ya ndani na shughuli halali bila kuingiliwa.
3.   Kujiunga na kuunda shirikisho na kushiriki shughuli za shirikisho hilo.
4.   Kujiunga na mashirikisho ya kimataifa, kuchangia na kupokea misaada ya kifedha kutoka kwa vyama au mashirikisho hayo. 
UTARATIBU WA KUUNDA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya mwaka 2004, Chama cha Wafanyakazi kinaweza kuanzishwa na wafanyakazi wasiopungua 20. Wafanyakazi hao wanapaswa kuitisha kikao cha kuanzisha Chama, ambapo watajiorodhesha na kutia saini zao katika rejista ya mahudhurio. Watamteua Katibu wa kikao ambaye atatayarisha muhtasari wa kikao wenye azimio la kuanzisha chama.
MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA KUANZISHA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
1.   Chama kiwe ni chama halisi cha Wafanyakazi (Bona fide Trade Union).
2.   Kisiwe chama kwa madhumuni ya kupata au kutengeneza faida (Association not for Gain).
3.   Kiwe ni chama huru, kwa maana kwamba kisianzishwe na muajiri au waajiri au serikali.
4.   Kianzishwe na wafanyakazi wasiopungua 20.
5.   Kiwe na katiba na kanuni zinazozingatia kifungu cha 47 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya 2004.
6.   Kiwe na jina lisilofanana na jina la chama kingine, kuzuia mkanganyiko au kuwapotosha watu.
7.   Kiwe na makao yake makuu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
UTARATIBU WA KUSAJILI CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Chama cha Wafanyakazi kinapaswa kusajiliwa ndani ya miezi sita (6) kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwake. Maombi ya usajili yatafanyika kwa kujaza fomu maalum ambayo itajazwa kikamilifu na kusainiwa na katibu wa kikao kilichoanzisha chama hicho.
Fomu hiyo ya maombi inapaswa kuambatana na nakala zilizothibitishwa za rejista ya mahudhurio, na nakala zilizothibitishwa za katiba na kanuni, na kuziwasilisha kwa msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na waajiri.
MAJUKUMU YA CHAMA KILICHOSAJILIWA.
Chama kilichosajiliwa kinapaswa kuwasilisha kwa msajili kila ifikapo tarehe 31 Machi au kila mwaka taarifa zifuatazo:-
a)    Taarifa ya fedha zilizokaguliwa kwa kipindi cha fedha kinachoishia tarehe 31 Desemba ya mwaka uliopita.
b)   Orodha ya wanachama inayoonesha jumla ya wanachama kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Desemba ya mwaka uliopita.
c)    Majina ya viongozi walioteuliwa au kuchaguliwa na anuani zao ndani ya siku 30 tangu uteuzi au uchaguzi kufanyika.
d)   Mabadiliko ya kanuni ndani ya siku 30 kuanzia siku ya mabadiliko hayo.
Chama pia kina jukumu la kutunza kwa miaka isiyopungua mitano kumbukumbu zifuatazo:-
1.   Orodha ya wanachama katika fomu maalumu.
2.   Mihtasari ya Vikao.
3.   Karatasi za kura.

Chama cha Wafanyakazi kinapaswa wakati wote kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa katiba, kanuni na mazoea. Endapo itatokea chama kimeshindwa kuzingatia katiba yake, msajili au wanachama wanaweza kupeleka maombi mahakama ya kazi kutengua suala hilo lililofanyika kinyume na katiba.
Kabla ya maombi hayo kupelekwa mahakamani, taratibu za ndani ya chama ni lazima zifuatwe kwanza. Isipokuwa ikiwa ni kwa maslahi ya chama, basi maombi hayo yanaweza kupelekwa mahakamani bila kufuata utaratibu wa ndani wa chama.
HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI MAHALI PA KAZI.
Chama cha Wafanyakazi kilichosajiliwa kina haki zifuatazo mahali pa kazi:-
1.   Haki ya kuingia eneo la muajiri – kwa lengo la kusajili wanachama, kuwasiliana na wanachama, kufanya vikao na wanachama, kuendesha uchaguzi. (Kifungu cha 60 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na.6 ya mwaka 2004).
2.   Makato ya Ada – kupokea ada za wanachama baada ya muajiri kuwakata kutoka kwenye mishahara yao. (Kifungu cha 61 cha Sheria ya Ajira).
3.   Kuwa na wawakilishi wake mahali pa kazi – chama cha wafanyakazi kinayo haki ya kuwa na wawakilishi mahali pa kazi kwa kuzingatia idadi ya Wanachama kama ifuatavyo:-
a)    Wanachama wasiozidi tisa (9) – muwakilishi mmoja.
b)   Wanachama kuanzia kumi (10) mpaka ishirini (20) – wawakilishi watatu.
c)    Wanachama kuanzia ishirini na moja (21) mpaka mia moja (100) – wawakilishi kumi.
d)   Wanachama zaidi ya mia moja (100) – wawakilishi kumi na tano, miongoni mwao watano lazima wawe wanawake kama wapo na ni wanachama.
MAJUKUMU YA WAWAKILISHI WA CHAMA MAHALI PA KAZI.
1.   Kuwawakilisha wanachama kwenye vikao vya kushughulikia malalamiko na nidhamu.
2.   Kuwasilisha hoja kwa niaba ya wanachama kuhusiana na kanuni, afya, usalama na ustawi wao.
3.   Kushauriana na muajiri kuhusu tija mahali pa kazi.
4.   Kukiwakilisha chama wakati wa ukaguzi na uchunguzi unaofanywa na wakaguzi kwa mujibu wa sheria yoyote ya kazi.
5.   Kuhakikisha kazi za chama kwa mujibu wa katiba ya chama.
6.   Kuendeleza uhusiano mzuri kazini.
7.   Kutekeleza majukumu waliokubaliana na muajiri.
Wawakilishi wa chama wanayohaki ya kupewa muda wa kutosha kutekeleza majukumu yao bila kukatwa mshahara na wanayo haki pia ya kupewa na muajiri taarifa zote muhimu zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Haki hizi zitatolewa na kutekelezwa vizuri bila kuvuruga kazi.
LIKIZO KWA WAWAKILISHI WA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Wawakilishi wa chama mahali pa kazi wanayo haki ya kupewa likizo ya malipo na muajiri kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo yanayohusiana na majukumu yao. Hali kadhalika viongozi wa chama cha wafanyakazi na wa shirikisho ambalo chama ni mwanachama, wanayo haki ya kupata likizo ya malipo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya chama au shirikisho.
UTARATIBU WA KUPATA HAKI ZA CHAMA.
Chama cha Wafanyakazi kilichosajiliwa kutekeleza haki za chama, kinapaswa kumtaarifu muajiri kwa kujaza fomu CMA F3 kikianisha haki ambazo kinataka kuzitekeleza pamoja na mahali pa kazi ambapo kinataka kuzitekeleza haki hizo.
Muajiri akishapokea fomu hizo anapaswa kukutana na chama ndani ya siku 30 ili kufikia makubalianao ya pamoja yatakayotoa haki hizo, na kuweka utaratibu wa kuzitekeleza. Endapo hakutakuwepo makubaliano au muajiri atashindwa kukutana na chama ndani ya muda uliowekwa, chama kinaweza kupeleka mogogoro huo mbele ya Tume kwa ajili ya usuluhishi.
Usuluhishi ukishindikana chama kinaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi kwa uamuzi.
USITISHAJI WA HAKI ZA CHAMA CHA WAFANYAKAZI.
Haki za chama zinaweza kusitishwa iwapo chama kitakiuka makubaliano ya msingi ya utoaji haki hizo au kwa amri ya mahakama inayotoa haki hizo.
Ikitokea hali hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano, muajiri anaweza kupeleka mgogoro huo mbele ya Tume kwa ajili ya usuluhishi. Usuluhishi ukishindikana, muajiri anaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi akiiomba Mahakama isitishe makubaliano ya kutoa haki hizo au iondoe amri yake ya kutoa haki hizo
HITIMISHO.
Mara nyingi katika maeneo ya kazi kumekuwa na migogoro mingi sana inayohusu masuala ya haki za vyama vya wafanyakazi. Waajiri kwa kutokujua au kwa makusudi wamekuwa wakikataa kutoa haki za chama kwa wafanyakazi wanachama wa vyama vya wafanyakazi. Hali hii imekuwa ikipelekea kuibuka kwa migogoro hiyo ambayo huatarisha mahusiano mazuri kati ya muajiri na wafanyakazi.
Mara nyingine wanachama wamekuwa wakizitumia haki zao vibaya katika maeneo yao ya kazi, jambo ambalo pia linamfanya muajiri kutoridhika na hali hiyo ambapo pia hupelekea migogoro ya kikazi kuibuka.
Makala hii imelenga kutoa ufafanuzi na uelewa juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Vyama vya Wafanyakazi na Haki zilizomo kwa pande zote mbili (muajiri na wafanyakazi). Aidha imeainisha majukumu ya chama na wanachama kwa ujumla.
Ni matumaini yangu kuwa itasaidia kutoa uelewa kwa wadau wa sekta ya ajira, hasa waajiri na wafanyakazi na hivyo kusaidia kupunguza migogoro ya kikazi na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wadau hao.
Imeandaliwa na Emmanuel C. Zongwe kwa msaada wa vitabu mbalimbali, mitandao na uelewa binafsi katika masuala ya Ajira na Mahusiano Mahala pa Kazi.

Simu: +255 (0) 717 058 045/ +255 (0) 755 223 697

E-mail: ezongwe@yahoo.com

Imetolewa na 
Jielimishe Kwanza.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni