K
|
atika maisha yetu ya kila siku tunakutana na mambo mbali
mbali, mambo hayo tunayoyaona,kusoma na kusikiliza yana mchango mkubwa katika
kujenga tabia zetu kwa njia moja au nyingine.
Mambo yote hayo yanaweza kutujenga na kuonyesha tabia hasi au
chanya mbele ya jamii kulingana na mazingira.
Nikimnukuu msanii wa muziki wa kufoka foka nchini Tanzania,
Farid Kubanga almaalufu kama
Fid Q katika wimbo wake wa Propaganda kuna mstari anaimba-“tunajenga tabia kisha tabia zinatujenga” …hii ni kweli kabisa, tabia tunazozijenga kutokana na mazoea mbali mbali kwa kujua au kutokujua, zinatujenga kitabia.
Fid Q katika wimbo wake wa Propaganda kuna mstari anaimba-“tunajenga tabia kisha tabia zinatujenga” …hii ni kweli kabisa, tabia tunazozijenga kutokana na mazoea mbali mbali kwa kujua au kutokujua, zinatujenga kitabia.
Ijulikane kuwa,tabia ikijijenga ni vigumu kuibadili, ukweli
huu ni sawa alivyoimba msanii wa muziki wa mashairi ya kughani Mrisho Mpoto katika wimbo wake wa “Nikipata nauli” kuwa, tabia ni kama ngozi ya mwili hauwezi kuibadili…ni
afadhali iwe njema, ikiwa mbaya ni hatari kwa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Ikiwa unasikiliza,kusoma au kutazama masuala yenye mtazamo
hasi na yenye hali ya hofu ya kutothubutu, ni hakika kabisa kuwa utakuwa ni mtu
wa mashaka katika maisha yako.
Pia kuna masuala yanayovuta hisia na faida yake ni kitambo
kidogo, haya yote kwa namna moja au nyingine yanajenga tabia ya
msomaji,mtazamaji au msikilizaji na hatimaye kupelekea kuonyesha tabia hizo kwa
vitendo mbele ya jamii.
Kwa hakika, tabia zetu na matendo yetu ni mazao ya masuala
mbali mbali tunayoyasoma,kuyasikia na kuyaona.Hii hutokea pale tu tunapoamua
kujifunza na kuyaweka katika utekelezaji kwa mazoea na hatimaye kuwa tabia.Unaweza
usiamini haya niyasemayo, kwa sababu yanatokea kwetu bila kujijua…hadi mtu
mwingine mwenye kujua tabia za watu atueleze.
Nikitoa mfano mdogo tu wa tabia ya ukatili kwa binadamu
wenzetu, hii hutokea kwa mtu kuwa na mazoea ya kusoma,kusikiliza,kutazama
sinema/video za watu makatili.Utaniuliza inawezekanaje mazoea yakasababisha mtu
kuwa katili kwa wengine? Hii hutokea kwa sababu ya kuchukulia matendo ya watu
makatili tunaowaona,kuwasikiliza na kusoma taarifa zao kimazoea katika maisha
ya kawaida.Filamu mbali mbali za kikatili huwaaminisha watu kuwa matendo
yaonekanayo ni ya kawaida tu ilhali si kweli.
Mfano mwingine ni ule wenye kuchochea tabia njema na yenye
maendeleo na kupelekea mtu kubadilika kitabia kutokana na kusoma vitabu vyenye
kuonyesha mbinu za mafanikio pia kuangalia filamu zenye kuchochea maarifa na
utendaji bora wa kazi, hivyo kuleta maendeleo kwa mtu husika na taifa kwa
ujumla.Fuatilia historia ya mafanikio ya watu mashuhuri duniani utagundua
ukweli wa jambo hili.
Kufikia hapa unaweza kujichunguza mwenyewe, unapendelea
kusoma,kusikiliza,kutazama mambo gani? Je, yana tija ya kukukomboa kiuchumi au
yanakufanya uwe msindikizaji ya mafanikio ya wengine? Au yanakupa hofu ya
kuchukua hatua ya kuthubutu kuelekea katika safari ya mafanikio? Sambamba na
hilo, je unatumia muda katika njia ya kuzalisha faida au hasara? Majibu unayo
mwenyewe…Tumia muda huu kuchagua kusoma,kusikiliza au kutazama mambo
yanayojenga tabia njema, amini usiamini hutakuwa vile ulivyo sasa.
Nakutakia kila la heri katika kujiepusha na mambo yasiyojenga tabia
njema na kukutisha na kukukatisha tama ya kusonga mbele kimaendeleo…soma,angalia,sikiliza
mambo yenye kuchochea mtazamo chanya…utapata ujasiri wa kuleta mabadiliko yenye
tija ya maendeleo binafsi na nchi yako
kwa ujumla.
Imetayarishwa na kutolewa na
Jielimishe Kwanza!
Jielimishe Kwanza!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni