“And the only way to
do great work is to love what you do”-Steve Job
Njia pekee ya kufanya kazi kwa ufanisi ni kupenda kile
unachofanya-Steve Job
Utendaji kazi na wenye tija
ya mafanikio huanzia ndani ya moyo.Mtu anaweza kufanya kazi kwa bidii ila ndani
ya moyo wake anasononeka na kuwaeleza wengine kuwa anapata ujira usiokidhi
mahitaji yake.Hapa tunasema mtu huyu hana moyo wa kazi…
Picha:www.telegraph.co.uk |
Watu wengi hufanya kazi wasizozipenda
ilimradi tu wapate kipato kwa wakati husika, pia kwa sababu wamekosa
kazi.Naomba nikuhakikishie ndugu msomaji, hakuna kitu kibaya kama kufanya kazi
usiyoipenda! Ukifanya kazi usiyoipenda, hata kama unafanya kwa bidii vipi
utajiona ni mtumwa tu.
Nikimnukuu Mama Theresa anasema;
usitarajie mambo makubwa, tenda mambo madogo kwa moyo- kwa lugha ya kiingereza: “Don't look for big things, just do small
things with great love.”Ukitenda mambo madogo kwa moyo ni rahisi sana
kukupeleka kwenye mambo makubwa.Anasisitiza
tena kuwa; Kufanya kazi pasipo
upendo ni utumwa. “Work without love
is slavery.”
Hapa nitatengeneza swali,
moyo upi tena ikiwa natafuta kipato cha kukidhi mahitaji? Naweza kuliweka hili
sawa kuwa, hupaswi kufanya kazi fulani usiyoipenda kwa minajili kuwa ina kipato kikubwa…kama nilivyosema awali,
utakuwa mtumwa wa kipato! Ndiyo maana kila siku wafanyakazi wanalalamika kuwa
kipato hakitoshi, hii ni kwasababu wamejikita sana kwenye kuangalia maslahi
pekee bila kuonyesha moyo wa kazi, pia hawalinganishi na ubora wa kazi wauletao
kwenye soko.Kama alivyosema Jim Rohn kuwa, “watu
hulipwa kutokana na uthamani wauletao kwenye soko.”Thamani kubwa zaidi kwenye
soko, ujira mkubwa zaidi.Je, utawezaje kuleta uthamani kwenye soko kama huipendi
kazi yako?
Ubora wa kazi hauwezi
kupatikana kama watu wakitoa udenda kwanza kwenye kipato kabla ya kuonyesha
moyo wa kujitoa na kuipenda kazi.Kwa lugha rahisi kabisa, onyesha moyo na nia
ya kazi uifanyayo bila kutoa macho makubwa kwenye ujira.
Nimeshuhudia baadhi ya
wafanyakazi wanaofanya kwa moyo- mh! Kama ukiwaona ndugu msomaji, unaweza
kufikiri wanalipwa ujira mkubwa sana, lakini nilipopata fursa ya kuwahoji,
wakanieleza kuwa wanafanya hivyo kwa sababu wanaipenda kazi, yaani wanajiona
huru kufanya kazi.
Unaweza usinielewe kwa haraka
haraka, fanya jaribio la kuipenda kazi kwanza, onyesha ubora, usinung’unike
kama wengi wafanyavyo…utastaajabu kuona kipato kikiongezeka kwa njia
nyingine.Utakuwa huru sana kwa sababu unajua sababu ya kufanya hivyo.
Ikiwa hujajua kazi uipendayo;
jitathimini, isikilize sauti ya ndani ya moyo wako, chukua hatua ya
kubadilika…simaanishi uache kazi, ila tenga muda wa ziada kuifanya kazi
unayoipenda.
Kuna wakati mwingine nitakufahamisha faida za
kufanya kazi unayoipenda.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!
Kama unataka ushauri usisite kuwasiliana
nasi,
Barua pepe:
jielimishekwanza@gmail.com
Skype: JielimisheKwanza13
Facebook: Jielimishe
Kwanza!
+255 754 572 143
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni