USIDHARAU MAMBO YANAYOONEKANA KUWA NI MADOGO…
Ni mara nyingi jamii imekuwa
ikipotezea sana masula au mambo yanayoonekana kuwa ni madogo "small things" kwa wakati
husika.Inafika wakati natafakari, nashawishika, pia kuchelea kukumbuka na kuikumbusha jamii
misemo hii ya Kiswahili inayoonekana kupitwa na wakati kama; “mdharau
mwiba mguu huota tende” na ule wa “usipoziba
ufa utajenga ukuta”.
Katika kuendana na wakati,
pia uhalisia wa mambo yatokeayo kila siku; misemo hiyo tajwa ina maana kubwa na
kwa hakika haijapitwa, wala haitapitwa na wakati abadani.Misemo hiyo au
“methali” za Kiswahili zilikuwepo na kutumika kuweka taadhali kwa mambo yanayoonekana
kupuuzwa na kuwa ni mzaha ilihali mwisho wa siku madhara yake ni makubwa sana kuliko
ilivyodhaniwa awali.
Nchini Tanzania na bila
shaka kungineko duniani kuna tabia na mazoea yaliyojijenga ndani ya jamii yenye
kupuuza masuala au mambo yanayoonekana kuwa madogo kwa wakati husika.Kuainisha
baadhi ya masuala hayo ni kama;
· kutupa
takataka ovyo kwa minajili eti ni kidogo tu ikitupwa nje ukiwa ndani ya chombo
cha usafiri haitakuwa na madhara yoyote
·
pia utupaji wa taka ngumu kiholela katika
mazingira yetu
·
kuchoma na kukata miti ovyo bila urejeshaji
wake
·
kutiririsha maji taka ovyo kwenye bahari na
vyanzo vingine vya maji,
· kutupa taka hewa angani kwa minajili kuwa
zitasafiri kwa upepo na kwenda sehemu nyingine zikipungua madhara
yake.Taka hewa hizo ni kama hewa ukaa
(CO2), na gesi taka nyinginezo za viwandani na vyombo vya usafiri
vitumiavyo mafuta.
Nimeainisha masuala machache
yanayochukuliwa kama mzaha na madogo sana kwa wakati uliopo, ila madhara yake
ni makubwa kadiri siku zinavyoyoyoma.Madhara
ya mambo yanayoonekana kuwa ni madogo hujikusanya kidogo kidogo bila jamii kutambua
kwa wakati husika. Chukulia mfano halisi wa tatizo la mmong’onyoko wa
udongo unavyotokea; huanza taratibu kwa udogo kuondolewa katika uso wa ardhi-
katika eneo moja lililo wazi kwa kukosa miti na nyasi hadi eneo lingine kidogo
kidogo kwa upepo na mvua, hatimaye kupelekea kuwepo kwa mabonde na ardhi
isiyofaa kwa shughuli mbali mbali.
Pia kuna madhara mengine huripuka na
kuiacha jamii na wataalamu kuhaha huku na huko kutafuta tiba ya matatizo
yaliyosababishwa na mkusanyiko wa mambo madogo madogo. Mfano mwingine ni huu wa
“wimbo wa dunia” wa “mabadiliko ya tabia
ya nchi” yapelekeayo kuongezeka kwa joto duniani-kwa lugha ya huko majuu hujulikana kama “climate change” ni matokeo ya shughuli
za kila siku za binadamu zenye kupuuza masuala madogo madogo kwa miaka nenda
rudi.
Katika kipindi hicho cha kuhaha, msemo
mwingine ndani ya jamii wa “kinga ni bora
kuliko tiba” hujitokeza kama sehemu ya kujikumbusha uzembe uliotokea awali
wa kudharau masuala na mambo yaliyoonekana kuwa ni madogo. Hapa jamii hukumbuka
kujikinga na madhara yaliyotokea kwa kudharau mambo madogo.Kampeni nyingi zenye
pesa hujitokea ili kuhamasisha mbinu mbadala za kujikinga na madhara
yaliyotokana na mambo madogo, pia kujipatia matumaini ya kurejesha hali pendwa
ilikuwepo awali.
Kiuhalisia, ni rahisi sana kufanikiwa
kupambana na kupata suluhisho la mambo yapelekeayo madhara makubwa katika hali
ya awali kabisa-hali ya udogo wake na si kupuuza udogo wake.
Hivyo basi, ni vyema na ni wajibu wa
kila mwanajamii kutopuuza hata kidogo mambo au masuala yanayoonekana madogo kwa
kujiridhisha upeo wetu kwa wakati husika.
Soma zaidi kujua ni nani anawajibu wa
kutunza mazingira kwa kutopuuza mambo madogo madogo yaliyoanishwa.
Imetolewa na Jielimishe Kwanza! Social
Enterprise kwa udhamini wa “Ide@Spot” na “Enviro-Forum”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni