USITEGEMEE KULIPWA SAWA SAWA NA WEMA ULIOTENDA…
Picha na http://www.simplemindfulness.com/2013/09/29/the-art-of-helping-others/ |
Watu wengi wamekuwa na
mtazamo unaokinzana na ule usemi maarufu wa Kiswahili usemao; “tenda wema uende zako, usingoje shukrani”.
Kupitia utafiti wa kimtazamo uliofanywa na Jielimishe Kwanza! Blog kuhusu kutenda
mema kwa marafiki au ndugu umebaini kuwa 99.99% ya wanajamii nchini Tanzania
hutarajia kurudishiwa wema ule ule waliomtendea mtu mwingine wakati wa shida au
raha. Mfano mdogo tu ni wakati wa kutoa mchango wa harusi, watu hutoa mchango
wakitarajia kuwa utamchangia vile vile kama alivyokuchangia.
Ifahamike kuwa, unapomsaidia
ndugu au rafiki katika shida au raha ni sehemu mojawapo ya wewe kuonyesha
ushirikiano na upendo kwa wanajamii kufanikiwa katika maswala mbali mbali.Isiwe
kinyume chake kwa kumsaidia mtu na mwisho kutarajia malipo na yasipopatikana
kama ulivyotarajia ni matusi na masimango-“eti
fulani bwana nilimchangia na kufanikisha shughuli yake…yeye hakunichangia, watu
wengine bwana! hawana shukrani!”
Pia inapaswa wanajamii
kufahamu kuwa si kila anayekutendea wema umeweza kumlipa vile vile kama
ulivyotendewa.Tunasaidiwa au watoto na ndugu zetu wa karibu wanasaidiwa na
wengine kwa njia moja hadi nyingine kiasi kwamba tumeshindwa kurudishia wema
ule ule.Ikiwa hali halisi ni hiyo, kwa
nini sisi tuwe wa kwanza kudai shukrani kutoka kwa wenzetu?
Kiuhalisia ni kwamba tupo
duniani ili tufaidiane, hakuna aliye mkamilifu wa kila kitu…hata hao wanasiasa
na vigogo hutegemea sana wananchi wawaweke madarakani kwa kutoa ahadi kadha wa
kadha, mwisho wa siku huwaacha solemba na kuwadharau kabisa hadi kipindi kingine cha
kuomba na kubembeleza uongozi kifike.Sipigii makofi tabia hii hata kidogo!
Namaanisha kuwa tuishi na watu vizuri tukijua maana na lengo halisi la
kutegemeana na kufaidiana.Isiwe faida ya upande mmoja kila wakati, inapobidi
toa shukrani kuthamini mchango wa wengine.Pia tunapotoa msaada au kutenda wema
tusidai shukrani, kwa kuwa shukrani ya mtu iliyo ya dhati hugusa dhamiri ya mtu
kwa kuzingatia uwezo wa wakati husika.
Nitofautiane pia na mtazamo
wa wengine kuwa watendapo wema kwa mtu au watu ni kama wamewekeza; wakitarajia malipo ya shukrani vile vile kwa
wema waliowatendea wengine.Ijulikane kuwa tutendapo wema kwa wengine tunajifungulia
milango ya baraka kwa njia nyingine…bila kutarajia tunaweza kupata wema zaidi
na usiopimika kupitia mlango mwingine kuliko kung’angana na kudai au kutegemea
shukrani kutoka kwa wengine.
Hivyo basi, tusikate tamaa
ya kuwasaidia wengine kwa kutotarajia malipo kutoka kwao.Tujitoe kwa raha na
shida za wengine, wengine kupitia mlango usiofahamika watajitoa kutusaidia
tukiwa na raha au shida.
Pia tunaposaidiwa, tuthamini
sana mchango wa wengine kwetu; tukijitahidi sana kuwasaidia wengine kwa upendo tu ulio na ushirikiano wa dhati kwa wanajamii wengine na si kwa
lengo la kulipiza wema ule ule kwa matarajio ya shukrani.
Imetolewa kwa udhamini wa Jielimishe Kwanza! Social Enterprise.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni