“I
like oppositions and criticism, the two make me behave better with
perfection-Henry Kazula
____________________________________________________________
Picha:managing-employee-performance.com |
Napenda kukukumbusha ndugu
masomaji wa Blog hii kuhusu moja ya makala zetu iliyobeba kichwa Ujasiriamali: wanaokupinga, kukudharau, kukuwekea vikwazo na kukukejeli wanakujenga bila wewe na wao kujijua…kwa mantiki kuwa
hatupaswi kuogopa kukoselewa kwa minajili kuwa tutakatishwa tamaa au kudharaulika
kwa maamuzi, mawazo au ubunifu wetu.
Katika safu hii leo napenda
tuangazie upande mwingine wa yule au wewe unayependa kukosoa wengine kwa namna
isiyo na lengo la kuboresha ubora wa utendaji ila kuwakwaza na kuwakatisha
tamaa wengine. Yawezekana unafanya ukosoaji huo kwa kujua unachofanya au kwa
kutojua uzito wa maneno yako kwa mhusika.
Kwa kuzingatia mtazamo wa
kisaikolojia, Jielimishe Kwanza! Blog inakudadavulia kinaga ubaga njia za
kipekee za kukosoa wengine bila ya kumkwaza mhusika, wakati huo huo uhusiano
ukiimarika na mhusika kujihisi vizuri na kutafakari kwa kina maoni aliyopewa.
Tumefanikiwa kukuletea njia
5 za msingi kuzitumia ili kuwa na uwezo wa
kukosoa kwa tija (constructive
criticism) bila kuwakwaza wengine na sisi kujiongezea heshima na uthamani
katika maeneo ya kazi;
1. ANZA KWA KUTUMIA LUGHA ILIYO CHANYA…
DaleCarnegie, mwandishi wa kitabu “How to win
Friends & Influence People” anasisitiza mtazamo chanya hasa katika
kukosoa wengine bila kuleta ugomvi ukizingatia kuwa watu wengi hawapendi
kukosolewa na hujiona wakamilifu muda wote.
Chukulia
mfano wa kimtazamo ufuatao: Ikiwa umegundua kosa la kiutendaji au ni mapungufu
tu ya kiutendaji kutoka kwa mfanyakazi unaweza kumwambia; “ukiongeza jitihada kidogo katika utendaji kazi wako utakuwa bora zaidi
na kuongeza sifa ya kampuni” …na si kumwambia; sifurahishwi kabisa na utendaji kazi wako, ukiendelea hivyo
nitakufukuza kazi”....
Au,
unaweza kuwakuta watu wakitupa taka taka katika eneo lisilo rasmi ilihali kuna
bango linaloonyesha sehemu sahihi ya kuhifadhi taka taka na kuwaambia; tafadhali naona ni vyema kama mngehifadhi
taka taka zenu katika chombo kilichoonyeshwa…badala ya kusema; ninyi vipi! hamuoni bango linaloonyesha
sehemu sahihi ya kutupa uchafu wenu?
2. ZINGATIA LENGO KUU KWA KUJENGA HOJA
Ni
vyema kufahamu na kuzingatia sababu kuu ya wewe kukosoa mawazo au utendaji kazi
wa wengine.Kwa kuzingatia lengo kuu utaweza kujua kwa kina maeneo yenye uzito
na uhitaji wa maboresho zaidi, hivyo kutoa maoni yako yenye kukosoa kwa lugha iliyo
rafiki.
3. FUATILIA KWA UKARIBU UTEKELEZAJI WA
MAONI YAKO
Si
jambo baya ukimuona mhusika moja kwa moja na kumueleza ushauri wako juu ya
utendaji kazi au mawazo fulani.Pia ukimuuliza mara kwa mara juu ya utendeaji
kazi au utekelezaji wa maoni yako.Mhusika atakuona una lengo zuri la kutaka
afanikiwe katika utendaji kazi.
4. TAFUTA MUDA MUAFAKA WA KUKOSOA/KUTOA
MAONI YAKO
Inapendeza
kutafuta muda na mahali sahihi kumueleza mtu kuhusu mapungufu yake ya
kiutendaji au mawazo ya kibiashara na si kuropoka mbele za watu kuhusu
mapungufu yake. Inakera sana na kukatisha tamaa mara tu mtu anapokukosoa mahali
pasipo sahihi au muda usio sahihi, haijalishi ubora wa ushauri kutoka upande
mwingine.
5. SIMAMIA UKWELI, USIFANYE KISHABIKI!
Tunapotoa
ukosoaji haimaanishi kufanya ushabiki ili upande unaokosolewa ushindwe kutimiza
malengo yake na kukata tamaa, la hasha! Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kunatokea
maboresho chanya ya kiutendaji kutokana na ushauri au maoni yaliyotolewa.Ni
vyema kuzingatia ukweli wa kila hoja ukizingatia lengo kuu la kuhamasisha
utendaji na si kudhoofisha mawazo au utendaji kazi wa wengine.
Kuhusu kufanikiwa kuishi na watu vizuri
na kuwahamasisha, Soma kitabu:
"How
to Win Friends and Influence People" by Dale Carnegie.
Imetayarishwa
na
Mwandishi
wa Kitabu-Mtazamo Wako Ni Upi?
Imetolewa
na
Jielimishe
Kwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni