In order to succeed, your desire for
success should be greater than your fear of failure.-Bill Cosby
__________________________
Picha na www.e-marketingassociates.com |
Mafanikio ya kirahisi
bila kulipa gharama kupitia changamoto yana mashaka! Wanawake waliambiwa utazaa
kwa uchungu na mwishowe kufurahia mtoto aliyezaliwa na kusahau hali ya uchungu
wao, vile vile kwa wanaume waliambiwa utakula kwa jasho mwishowe kusahau
machungu ya kazi zao kipindi cha kusheherekea mafanikio; Maandiko Matakatifu
yameainisha kuhusu hili.
Hakuna mtu asiyependa
kutimiza malengo yake yaliyo sanjali na shauku
ya mafanikio. William Henry "Bill" Cosby mchekeshaji na mwana harakati maarufu mwenye mafanikio makubwa duniani
anaweka angalizo kuhusu jinsi ya kupata mafanikio kwa kuzingatia shauku ya
mafanikio kwa kusema; “ili kufanikiwa,
shauku ya mafanikio yako inapaswa kuwa kubwa kuliko hofu ya kushindwa.”
Ukifuatilia kwa
makini mtazamo wa Cosby kuhusu
mafanikio utabaini kuwa watu wengi hukinzana naye kwa kutanguliza hofu ya kushindwa kabla ya kukabiliana
na hali halisi kuelekea mafanikio yenye msukumo wa ndani wa shauku ya mafanikio.
Kipimo Cha Mafanikio
Watu wengi wanashindwa
kuweka uwiano mzuri kati ya shauku ya mafanikio
na hofu ya kushindwa…uhalisia uliopo ni
kwamba, watu wengi hutawaliwa na hofu ya kushindwa ipelekeayo kuelemea shauku
ya mafanikio! Sambamba na hali hii tujiulize maswali ya msingi kuhusu
kipimo cha uwiano wa mafanikio; je, nini kipimo cha mafanikio ya mtu binafsi? …je,
ni ule uwezo wa mtu kuzishinda changamoto? au ni ule uwezo wenye uthubutu wa kuishinda
hofu ya kushindwa kwanza?
Kutoa majibu ya
maswali hayo si jambo la haraka haraka; namaanisha si kuangalia kigezo kimoja
na kujiaminisha au kujiridhisha kimtazamo.Mara nyingi katika mafunzo yangu
nasisitiza kuwa; mtazamo ulionao kukuhusuukijilinganisha na ule wa watu wengine unakuwa uhalisia wako kama utaamini nakujichukulia.(Mfano: mtu aweza kujiaminisha kuwa mafanikio ya wengi
kiuchumi si kwa njia halali; ni lazima ufanye wizi, ukiuke taratibu za
kiutendaji, utumie uchawi au ufanye mauaji…huu unakuwa uhalisia wa maisha yake
kwa sababu ni mtazamo wake uliohusisha kujiaminisha.
Mafanikio ya kweli,
yenye kuzingatia shauku ya mafanikio
kwanza kuliko hofu ya kushindwa
hupimwa kwa kuzingatia uwezo wa kifedha/kipato halali (uhuru wa kipato) kukidhi mahitaji mbali mbali ya kibinadamu (human needs) sanjali na kutimiza hitaji la msingi la kisaikolojia
(uhuru wa nafsi na fikra).
Kutimiza hali ya
kisaikolojia sambamba na mafanikio inatazamwa kwa jicho lingine na mwanasaikolojia
Maslow (1943, 1954) hasa katika
kutimiza mahitaji ya kibinadamu kupitia hatua au ngazi ya juu namba 5, mtaalamu
Maslow ameiita “self-actualization of
human needs” … na ni nadra sana kufikia hatua hii kwa sababu ya vikwazo na
kutotimiza mahitaji ya ngazi ya chini kama; hali
ya kisaikolojia (1), usalama (2),
uhusiano wa kijamii (3), na uwezo wa kujitambua na kujiamini(4).
Katika hali isiyo ya
kawaida, watu wengi wamekuwa wakipima mafanikio yao au ya wengine kwa kipimo
cha macho ya matamanio pekee hasa kwa kuangalia umiliki wa mali (material things) kama kumiliki magari,
majumba ya kifahari na mengine mengi yanayovuta macho na hisia lakini
kusahau hali ya kisaikolojia kama vile furaha, uhuru wa nafsi na fikra n.k. Pia
wanaamini kuwa pesa pekee huleta furaha na uhuru wa fikra na ule wa nafsi.
Ndugu msomaji,
ijulikane kuwa kupima mafanikio yako yaliyo ya dhati usiangalie kigezo kimoja
tu, ni vyema kuzingatia mafanikio endelevu yajumuishayo kutimiza shauku au
hitaji la moyo bila kutanguliza hofu kwanza na kubwa kuliko ni lile la kutimiza hitaji la kisaikolojia kama
alivyoainisha Mwanasaikolojia Maslow- kutimiza mahitaji ya ngazi ya chini ili kupelekea kupata
mafanikio ya kweli yasiyo na mawaa.
Makala inayohusiana: The Truth About What It Means to Be Successful
Makala inayohusiana: The Truth About What It Means to Be Successful
Imetayarishwa
na
Mwandishi
wa Kitabu-Mtazamo Wako Ni Upi?
Imetolewa
na
Jielimishe
Kwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni