Naandika makala hii nikiburudika na muziki
pia maneno ya msingi kutoka moja ya mstari wa wimbo-“Sugua gaga” wa mwanamuziki maarufu wa “bongo flava” nchini Tanzania- Sara Kaisi almaarufu “Shaa”. Katika
mstari huo anasema; “…kama una shida
unamwambia nani? hata mimi za kwangu nimeacha nyumbani” akimaanisha kila
mtu ana shida zake.Ama kwa hakika wasanii wa nchini Tanzania wanajitahidi kwa
ubunifu katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii kupitia muziki, huyu ni
miongoni mwa wasanii walionukuliwa katika KITABU chetu kitakachotoka mapema mwaka 2015.Wasanii wengine utakuwa umeona
tulivyowanukuu na kuendelea kuwanukuu katika makala zetu kutokana na
sehemu za mashairi yao yenye kukonga nyoyo na kufikisha ujumbe mahsusi kwa
jamii.
Sasa
turudi kwenye mada iliyopo mezani, wengine
wana shida zao. Katika maisha ya kila siku iendayo kwa Mungu, kila mtu
hupatwa na maswahibu au shida mbali mbali. Watu hutofautiana sana katika
ujasiri na uvumilivu wa shida mbali mbali.
Watu
wengine ni wavumilivu sana kukumbatia shida zao na kupambana kwa njia moja au
nyingine kupata suluhisho. Wapo makini sana kutoa shida zao kwa wengine.
Huamini kuwa unapotoa shida yako kwa kila mtu ni kujidhalilisha na
kujishusha
thamani, hivyo basi huamua “kufa na tai
shingoni” kuhusiana na shida zao.
Pia
wapo wengine walio waoga sana kwa shida-wakiamini kuwa ni wao pekee duniani
wenye shida. Kundi hili halitulii kukaa na shida, hivyo humweleza kila mtu
wanayemfahamu shida zao. Bila kuchagua aina ya watu wa kuwaeleza shida zao;
imewapelekea kukosa msaada na mwisho wa siku kuishia kutangazwa na kukimbiwa
mara wawapo na shida. Hii imetokana na wao kuwa wavivu wa kuwajibika katika
kutatua shida zao na kuwa tegemezi kwa wengine kupita kiasi.
Ndugu
msomaji, nimeamua kuainisha makundi hayo mawili kwa kuzingatia uwezo wa kila
kundi kuhimili na kustahimili shida ili iwe rahisi kwako kujichagulia kundi
ulipendalo au kujiimarisha katika kundi husika kwa manufaa ya maisha yako.
Suala la msingi la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa shida uliyonayo haiwasumbui
wengine. Pia kujitafutia watu au mtu sahihi ambaye mtakuwa mkisaidiana.
Sitarajii
kueleweka vibaya kuwa nahamasisha watu wasisaidie wenye shida, hapana! Nafanya
hivyo kwa mapenzi mema ili kuhamasisha uwajibikaji wa kila mwanajamii katika
kujiinua kimaisha na si kuwa tegemezi kupita kiasi. Fuatilia zaidi KITABU chetu kitakachohamasisha badiliko la kimtazamo na uwajibikaji ulio na uhusiano wa machaguo mbali mbali ya
maisha bila kuwakwaza au kuwatwisha wengine majukumu.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!