Kama ilivyo ada kila mwaka,
tarehe 5 Juni duniani kote tunaungana kwa sauti moja na kauli mbiu moja
kuadhimisha siku hii muhimu kwa mustakabali wa maisha yetu; kwa kuzingatia
kuhifadhi na kuitunza “nyumba” (mazingira) inayotutunza.
Siku hii muhimu duniani
ilianzishwa katika Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN General Assembly) mwaka 1972.Hivi leo “Siku Ya Mazingira Duniani” inaendelea
kuheshimiwa duniani pote pia kusimamiwa kikamilifu na Kitengo cha Umoja wa Mataifa
cha Mazingira-United Nations Environment Program (UNEP).Tukiwa kama familia moja
duniani, husindikizwa na kauli mbiu itolewayo kila mwaka kwa kuzingatia maoni
ya wataalam na wadau wa Mazingira duniani.
Kwa bahati nzuri kauli mbiu
ya mwaka huu isemayo“Seven Billion
Dreams.One Planet.Consume With Care”
kwa tafsiri ya lugha ya Kiswahili-Ndoto
bilioni saba. Sayari moja.Tumia kwa uangalifu inatukumbusha kutumia
rasilimali tulizonazo kwa uangalifu ukizingatia kuwa kuna ongezeko la idadi ya
watu duniani (bilioni 7 hadi sasa)
wenye ndoto tofauti tofauti, mabadiliko ya tabia nchi na wakati huo huo
rasilimali nyingi zilizopo si rejereshi; zinatumika na hazijirudii au kurudishwa
tena.
Shirika hilo la Umoja wa
mataifa linalohusika na Mazingira duniani (UNEP) limeweka angalizo kuu kuwa
kutokana na mfumo wa maisha ya binadamu, na uhitaji wa rasilimali ambazo kwa
kiasi fulani zinaelekea kutokidhi ongezeko la idadi ya watu duniani; kuna
hatari kubwa kuwa kama hali itaendelea kama kawaida kwa kuangalia makisio ya
ongezeko hilo la watu bilioni 9.6 ifikapo
mwaka 2050 tutahitaji kuwa na sayari 3 ili kukidhi mahitaji yetu.Unashangaa!
Ndiyo huko tunakoelekea na vizazi vyetu. Wengine naona wameanza kuangalia
uwezekano wa kuishi kule kwenye sayari ya “Mars”.Mimi na wewe je? Natania tu…
Imefika wakati wa kuamka
sasa, kila mtu kuchukua wajibu sasa, kufanya pale anapoweza kuhakikisha kuwa
rasilimali zilizopo zinatumika kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia maendeleo endelevu- maendeleo
yanayokumbuka na kuchukua taadhali kubwa kuwa kuna vizazi vijavyo
vitakavyohitaji rasilimali zilizopo sasa.Ni maendeleo
yanayozingatia manufaa ya jamii, mazingira
yenyewe na uchumi kwa ujumla
wake.Maendeleo yanayosahau kimoja kati ya hivyo vitatu, si maendeleo endelevu;
yanapaswa kukosolewa, kubezwa na kuzomewa kwa kelele nyingi.Anza sasa!
Imetayarishwa
na
Mwandishi
wa Kitabu-“Mtazamo
Wako Ni Upi?”
Imetolewa
na
Jielimishe
Kwanza!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni