Kuna wakati tunajiona na kujichukulia
kama hatuna bahati, haki wala uwezo wa kumiliki vitu vya thamani, kusoma hadi
ngazi za juu za elimu tuitakayo au kuwa na uhuru wa kipato kutuwezesha kutatua
matatizo mengine ndani ya maisha yetu.Hii ni kwa sababu tunawaona wengine
wakituzidi kimaisha kwa kumiliki vitu vya thamani na kusonga mbele kiuchumi
ilihali hatujui wamepitia njia zipi kuvipata. Msemo ufuatao katika lugha ya Kiingereza unakazia...
Mwisho
wa siku tunabaki kunung’unika, kulaumu wengine kwa wajibu wetu na hata kufikia
hatua ya kumkufuru Mungu… “eti ana upendeleo” La hasha!
Tunasahau kuwa kwa vile au kile tulicho
nacho, tukionacho kidogo kwa mtazamo wetu wa kibinadamu kuna wengine wamekosa kabisa na wanatamani wawe
kama sisi. Je, ndugu msomaji unalitambua hilo? Pia una tambua kuwa kuna watu
wengine hawajui walale wapi? na hawajui wale nini?... Haya ni maswali machache
tu yanayoweza kututofautisha na wengine, na mwishowe kujiona tuna nafuu kuliko hao
wengine.
Pia, ijulikane kuwa kuna watu ambao
wanaombea kesho ifike salama, na wengine wanaomshukuru Mungu kwa uhakika wa
pumzi tu! waipatayo kila siku ipitayo… kwa kifupi hawana uhakika wa maisha.
Wengine ni wagonjwa wamelala vitandani kwa muda mrefu sasa…wanashauku kubwa ya
kutembea na kufanya kazi tena.
Ndugu msomaji, kwa umakini kabisa naomba
jichunguze, jilinganishe na wasio nacho na wenye shida utaona kuwa una nafuu
kubwa kuliko hao wengine!
Ni sahihi kusema kuwa mwanadamu hatosheki
na haridhiki kwa kile alicho nacho kwa wakati husika.Siku zote tunajitahidi kujiongeza,
ndiyo maana matajiri hawachoki kutafuta pesa na mali…kila kukicha wanasaka pesa
na kujilimbikizia mali, wakati huo huo watu wengine wakiwa hawaijui kesho yao.
Hali hii hukinzana kidogo na mtazamo wa mtaalam,
mwanasaikolojia Maslow (1943, 1954) katika “Maslow’s Hierarchy of needs” anasema; mwanadamu
ana mahitaji yaliyoainishwa kwa ngazi 5 muhimu. Mwanadamu huamasika kufikia
hitaji fulani…likitimia huitaji tena kufikia hitaji lingine, lingine na
lingine. Inafikia wakati uhitaji wa mwanadamu “human needs” hufikia kikomo cha kujitosheleza kiasi cha kuweza
kutoa msaada kwa wengine wasio nacho, hatua au ngazi hiyo ya juu namba 5,
mtaalamu Maslow ameiita “self-actualization
of human needs” … na ni nadra sana kufikia hatua hii kwa sababu ya vikwazo
na kutotimiza mahitaji ya ngazi ya chini kama; hali ya kisaikolojia(1), usalama
(2), uhusiano wa kijamii (3), na uwezo wa kujitambua na kujiamini(4).
Ngazi zote tano (5) ameziainisha kwa umbo
la “pyramid”-umbo la nyumba za
kihistoria za Wamisri, ukianzia ngazi ya chini (1) kwenda ngazi juu ya ukomo
(5).
Katika hali isiyo ya kawaida, watu
wanaoonekana wamefika kikomo cha uhitaji, wanaonekana kutoridhika na hali hiyo
kiasi kwamba huendelea kuwanyonya kiuchumi wasio nacho.Nisiingie sana kiundani
hapa kuwahusu hao waliofika hali ya kikomo cha uhitaji kama wanavyojiona.
Sitaki kukuhamisha kwenye mada kuu…wengine wamekosa kabisa! Ila tuache
kunung’unika, tulizike kwa kidogo tulicho nacho! ili kiwe chumvi ya hamasa
katika kuelekea mafanikio makubwa tutakayo kuwa nayo.
Waswahili wanasema ridhika na kidogo ulicho
nacho, usitafute makuu usiyoyaweza kwa wakati husika! Kinyume na hapo utaingia tamaa
bure ya kuiba, kudhurumu wengine, kukiuka maadili ya kazi na hata kufikia
hatua ya kuua wengine kwa kutamani pesa na mali.Sina maana tubweteke, kukaa na kusubiri
miujiza au kuacha kukaza buti kujinasua kihalali katika hali ngumu ya maisha…La!
Huu ni mtazamo tu wa Jielimishe Kwanza!
…unaweza kukusaidia, usikate tamaa.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza! Social Enterprise.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni