________________________________________
|
Picha:http://www.hischerishedones.org |
Furaha ni hali ya kibinadamu
inayotawaliwa na hisia au akili, hujitokeza kiasilia kwa kuchangiwa na
mazingira mazuri yanayomzunguka mtu katika shughuli zake za kila siku.Humfanya
mtu kujisikia vizuri, kujihisi kutosheka. Pia, ni kichocheo cha kusonga mbele
kiutendaji na kuboresha maisha.
Kila mtu anapenda au
anahitaji kuwa na furaha wakati wote.Swali
la msingi la kujiuliza; Je, inawezekana
kuwa na furaha wakati wote? Kiuhalisia, mwanadamu ameumbwa kukutana na
changamoto mbali mbali zichocheazo utashi wake au hisia zake.Uwezo wa asili na
akili ya binadamu kupambana na kushinda changamoto hizo huongeza furaha.Lakini,
si kila changamoto iliyopo na inayojitokeza hupelekea furaha…kuna wakati hali
huwa kinyume na matarajio kiasi cha kupoteza furaha.
Shughuli za binadamu na
mwenendo wa maisha yetu huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuikaribisha au
kuikimbiza furaha iliyo asili ya mwanadamu, ondolea mbali mambo tusioweza
kuyazuia kama kifo, magonjwa, dhoruba mbali mbali n.k. Hivyo basi, si jambo rahisi kuwa na furaha wakati wote! Hii ni sawa
sawa na kusema hatuwezi kuipata furaha ya milele tungali tunaishi katika dunia
hii yenye kila aina ya udhalimu na maovu.
Ingawaje hatuwezi kuwa na
furaha wakati wote, tumaini lipo na tunaweza kuirejesha furaha iliyopotea
kutokana na mambo yaliyo katika uwezo wa kibinadamu hasa kutokana na maisha ya
kila siku na shughuli mbali mbali za kila siku.
Je, umepoteza furaha kwa kufeli mtihani?, kukosa ajira?, kukimbiwa na marafiki?, kutengwa na ndugu?, kuachwa/kukimbiwa na akupendaye(mke/mume au mchumba?), kuchekwa na watu kwa jinsi ulivyo? na hali nyingine zinazofanana na hizo? Usikate tamaa wala kurudi nyuma.Chukua hatua hizi 10 za ujasiri au ushujaa kufanya yafuatayo; (leo zitaainishwa 5):
1.ACHA KUNUNG’UNIKA, CHUKUA
HATUA YA KUANZA UPYA!
Jinsi unavyoendelea kunung’unika
ni dhahili kuwa hali itaendelea kuwa jinsi ilivyo na ndivyo fursa nyingi
zitakapokupita.Manung’uniko huchochea hasira na chuki hivyo kuzidi kuipoza
furaha yako. Hivyo, ni vyema kuacha kunung’unika na kuchukua hatua ya ujasiri
kuanza upya, anzia ulipo ukiboresha mapungufu yaliyopo.
2.USIGEUKE NYUMA/USIKUMBUKE
YALIYOPITA, SONGA MBELE!
Hakuna kitu kibaya kama
kuendelea kukumbuka maumivu au matukio mabaya yaliyopita! Shukrani kwa Mungu
hata kutuumbia hali ya kusahau…katika hali hii, kusahau mabaya hutupatia
mtazamo chanya wa kuyaona maisha katika sura iliyo rafiki na kutujengea furaha
nyingine.Songa mbele, jiwekee mkakati wa kutokumbuka yaliyopita.Najua kuwa kuna
matukio mengine ni vigumu kuyasahau-lakini jitahidi kujibidisha, kuna wakati
utafika na kuiona furaha yako ikirejea.
3.TAMBUA KUWA, ULIVYOVIPOTEZA
HUKUZALIWA NAVYO…
Ni jambo la kipekee sana
kumshukuru Mungu kwa kuwa tunaishi! Vile tulivyo ni upekee tuliopewa.Tumezaliwa
na kuvikuta vitu na watu mbali mbali.Pia tunategemeana katika masula mbali mbali
katika kuendesha gurudumu la maisha.Ni ukweli usiopingika kuwa hakuna kitu
tumezaliwa nacho…vingi tumevikuta na tunavitafuta kila kukicha.Pia, vingine ni vigumu kuvirudisha katika hali ya mwanzo.Hivyo,tunavyovipoteza visitukatishe tamaa na kupoteza furaha zetu.Tunapaswa kuanza
upya kuanzia pale tulipo kama ilivyoelezwa katika hatua mbili zilizopita.
4.USIJIONE KUWA NI WEWE
PEKEE MWENYE SHIDA IPELEKEAYO KUKOSA FURAHA…
Hatua hii inanifanya
nikukumbushe moja ya makala zetu yenye kichwa “Tambua kuwa wengine pia wana shida zao”…kwa mantiki kuwa hakuna mtu asiye na shida; tunatofautiana jinsi ya kuziona shida na kupambana nazo.Ikiwa umepatwa na
maswahibu yapelekeayo kupoteza furaha yako, ni vyema kutafakari kuwa hauko peke
yako…yawezekana wewe una unafuu mkubwa kuliko wengine wenye shida.
5.JIJENGEE MTAZAMO MPYA WA
MAISHA ULIO CHANYA…
Katika kitabu “MTAZAMO WAKO NI UPI? Mtazamo Wako, MaishaYako” kinaeleza na kuhamasisha mtazamo ulio chanya kwa kuwa maisha yetu
hutawaliwa kwa kiasi kikubwa na mtazamo tulio nao na tunaotaka kuwa
nao.Jitahidi kujiepusha na hali au mazingira yenye kukatisha tamaa, hali ya
majonzi na kusononeka nafsi (mtazamo hasi) ili kuijenga na kuiimarisha furaha
iliyo asili yetu.
Tukutane tena siku nyingine kama hii tumalizie hatua 5 zilizobaki.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza.