Tunapolitazama suala zima la kujieleza mbele
ya hadhira si suala rahisi kama hofu itakutawala.Itawale hofu!
Watu wengi ni waoga sana
kusimama mbele ya hadhira.Mfano: utamwona mtu anatetemeka mara tu anaposimama
mbele ya hadhira au kuongea maneno nusu nusu na hatimaye kushindwa kuwasilisha
ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira.Je, tatizo ni nini? Tatizo limeanzia wapi?
Awali ya yote kabla ya kueleza MBINU 5 za
kukufanya ufanikiwe kujieleza mbele ya hadhira bila hofu, ni vyema tukajua chanzo cha
tatizo kupitia maswali hayo
mawili yaliyotajwa.
Tatizo la kuogopa kuongea mbele za watu au
hadhira linanzia tangu shuleni, pale mwanafunzi anapochekwa hasa akiwa anaongea
mbele ya darasa hivyo kujikuta akikosa ujasiri wa kuendelea kuongea.Hili
linawafanya wanafunzi wengine kuogopa kusimama mbele ya hadhira na mwisho
hubaki kutupiana mpira wa kujieleza inapofika hatua ya majadiliano na uwasilishaji darasani.
Pia, mfumo wa elimu- mfano nchini Tanzania
haujaweka msisitizo wa kutosha kwa wanafunzi kuhusiana na suala zima la
kujieleza mbele ya hadhira.Wanafunzi wamekosa ujasiri wa kuelezea vitu
walivyoviandika kwa ufasaha katika hali ya kawaida.Hili linatokana na kuwa na
mtazamo wa moja kwa moja wa kuandika kwa lengo la kufaulu mitihani na si kuwa
ujasiri wa kukielezea walichokiandika kimatendo mbele ya wengine na kupambana na changamoto za maisha ya kila siku.
Athari hii kwa mwanafunzi haishii hapo bali
huathiri maisha ya ukubwani.Ndiyo maana utaona watu wengi hushindwa kujieleza
kwa ufasaha kwa sababu ya hofu.
Tuje moja kwa moja kwenye MBINU 5 za kuwa na
ujasiri wa kuongea mbele ya hadhira:
1. JIANDAE
VYA KUTOSHA! FANYA ZOEZI UKIWA MWENYEWE...
Ni vyema kujiandaa kuhusiana na kile
unachataiwa kukieleza mbele ya hadhira.Ifahamu hadhira utakayokwenda kuielezea
jambo fulani. Usiende kuongea mbele ya hadhira ukifikiria kuwa maneno
yatapatikana ukiwa mbele yao.
Unashauriwa kufanya zoezi la kujieleza ukibashiri kama unaongea na hadhira.Kipekee zaidi ukimtazama mtu mmoja akiwakilisha hadhira yote.Hili ni la muhimu sana katika maandalizi, unapaswa kujua kuwa huwezi kukidhi matakwa ya kila mtu.
Inashauriwa uongee ukiwa unajitazama kwenye kioo au ukamwomba rafiki yako akurekodi.Hii itakusaidia kuondoa mapungufu uliyonayo na itakujengea ujasiri zaidi hata utakapokuwa ukiongea na hadhira halisia.
MUHIMU: Hakikisha unaifahamu hadhira utakayokwenda kuongea nayo, itakusaidia kupanga mbinu za kuwasilisha hoja zako.
2. EPUKA
KUKARIRI HOTUBA YAKO KWA KILA NENO…ELEWA!
Si jambo baya kuandika hotuba yako kwenye
karatasi au kijitabu, lakini kuwa makini sana wakati wa kutumia ukiwa mbele ya
hadhira. Ni vyema kuelewa kile unachotaka kukiwasilisha mbele ya hadhira.
3. EPUKA
KUSOMA HOTUBA YAKO NENO KWA NENO
Ukizingatia mbinu namba 2, itumie hotuba yako
uliyoandika kwa kujikumbusha sehemu zenye utata.Usiisome hotuba
yako…utawachosha wasikilizaji watasema; “
ni vyema angetupatia hotuba yake tukajisomee nyumbani…”
4. USIOGOPE
KUHUSU WOGA WAKO
Itambulike kuwa kila binadamu ana chembe ya
woga. Ni vyema kuitambua hofu yako na kujaribu kupambana nayo bila kujulikana
na hadhira pia bila kuharibu uwasilishaji wako.
5. USIJIWEKE
KUWA MKAMILIFU WAKATI WOTE
Unapaswa kujua kuwa hata waongeaji maarufu wa
hadhara hufanya makosa.Hivyo usifikiri kuwa hutakuwa na makosa katika
uwasilishaji wako.Ni vizuri ukuamua kurekodiwa kwenye video ili ujitazame baada
ya hotuba yako.Itakusaidia kujua makosa uliyoyafanya wakati wa uwasilishaji
hivyo kuboresha utendaji wako siku hadi siku.
Sambamba na mbinu hizi, ni vyema pia kuboresha muonekano wako-mfano mavazi nadhifu, uongeaji wako na uhusiano mzuri na hadhira (kuwatazama moja kwa moja).Pia matendo yako yaendane na kile unachotaka watu waelewe.
Nakutakia kila la heri katika kutumia mbinu hizi na kuboresha ujasiri wako wa kuongea mbele ya hadhira. Ukifanikiwa, ni sehemu mojawapo ya kupata ajira na kuwa mahiri katika fani yako...Itambulike kuwa suala la kuongea mbele ya hadhira HUWEZI KULIKWEPA, ipo siku tu utatakiwa kusimama mbele ya hadhira na kutoa neno.
BOFYA HAPA KUTAZAMA VIDEO UONE JINSI UNAVYOTAKIWA KUONGEA MBELE YA HADHIRA...