inspire

inspire

Lebo

AFYA (8) AJIRA (5) BIASHARA (39) ELIMU (14) MAHUSIANO (2) MALEZI (16) MAZINGIRA (12) SAIKOLOJIA (48) VIJANA (7)

Business registration

Green Consulting

business consultancy

business consultancy

Business consulting-2

Business consulting-2

Professional Consulting

PDC

Swahili translator

Swahili translator

TANGAZO-KITABU

E-BOOK: MTAZAMO WAKO NI UPI?

TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- .... TANGAZO:Kitabu kipya. Kitabu! Kitabu!Kinauzwa Katika Maduka Ya Vitabu.Pia M-Pesa 0754 572 143, Tigo Pesa 0716 075 826.Ili Kikufikie Ulipo, Tafadhali Ongezea Sh.10,000/- ....

TANGAZO TUWEZESHANE

TANGAZO TUWEZESHANE

DARDY'S INVST-20/10/2017

DUNIA IKUONE

DUNIA IKUONE

Ijumaa, 31 Mei 2013

UJASIRIAMALI NA VIJANA: WAZIRI WA UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI DK. MARY NAGU AFUNGA RASMI MAFUNZO YA WAHITIMU (40)WAJASIRIAMALI LEO !

Leo imekuwa ni siku ya kilele cha mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana-wahitimu wa vyuo vikuu mbali mbali nchini.

 

Mafunzo hayo yaliyowashirikisha vijana 40, yameongeza chachu kwa vijana hao hasa katika kuwajengea uwezo wa kuandika mipango ya kibiashara,uwezo wa kujiajiri na kuweza kuajiri wengine.

 

Kwa kushirikiana na chuo kikuu Dar es salaam, kitengo cha ujasiriamali, Baraza la uwezeshaji la Taifa kiuchumi limeweza kufanikisha mafunzo hayo na kuwatunuku wahitimu 40 vyeti katika Hotel ya Blue Pearl Hotel, ukumbi wa Crystal Hall-Ubungo Plaza, jijini Dar es salaam leo.

 

Zoezi hilo liliambatana na utolewaji wa zawadi kwa washiriki watatu(3) waliofanya vizuri katika zoezi la uandikaji miradi ya biashara.

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, akiwa mgeni rasmi alipewa nafasi kuwatunuku vyeti wahitimu hao  na zawadi kwa washindi watatu(3) ambao ni Bw. Anthony Seleli Mhanda aliyepata sh.milioni 10, Bw. Ale Alex Kaaya aliyepata sh.milioni 8 na , Bi Selina Julius Otacho aliyepata sh. milioni 6.

 

Mwisho kabisa Dr. Nagu alitoa hotuba fupi kwa wahitimu na umma kwa ujumla wake.Aliwapongeza wahitimu kwa kuthubutu kuchukua uamuzi wa kujiajiri na ofisi yake haitawaacha, itashirikiana nao kuhakikisha mafunzo waliyoyapata yanazaa matunda.

 

Aliainisha kuwa, katika nchi yetu kuna makundi matatu ya mifumo ya kujipatia mkate wa kila siku; kundi la kwanza ni la watanzania wanaobangaiza bangaiza-wanabahatisha maisha, la pili ni lile la waajiriwa na wachacharikaji ingawaje kipato chao ni kidogo na hakikidhi, kundi la tatu ni la wajasiriamali-kundi hili lina watu wachache, ni watu wenye kuona fursa na kuzitumia ikiwa sambamba na kutengezea vyanzo vingine vya ajira.

 

Alishauri kuwa, imefika wakati kwa watanzania kuhamia katika kundi hili la tatu ambalo linakwenda kuongeza idadi ya ajira na kukuza uchumi wa kila mtu na si kutegemea kukua kwa uchumi wa Taifa. Akimaanisha kuwa; uchumi wa mtu mmoja ukikua, wa Taifa utakua.

 

Ilitaadharisha kuwa kukua kwa uchumi wa Taifa si kiashiria kizuri cha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja.Hivyo watu wasijidanganye na kutegemea kukua kwa uchumi wa Taifa ila inapaswa wananchi wenyewe, mmoja mmoja achukue jukumu la kukuza uchumi wake ili uchumi wa Taifa ukue.

 

Dr.Nagu alikazia kwa kusema; ukosefu wa ajira kwa vijana nchini unatokana na kutegemea kuajiriwa katika sekta rasmi...

 

PICHA NA MATUKIO:

Washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali wakiwa katika ukumbi wa mkutano

 

Henry Kazula, akitunukiwa cheti cha mafunzo ya ujasiriamali
Waziri, Dk.Mary Nagu akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali


Waziri, Dk.Mary Nagu akijadiliana na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali







Henry Kazula (wa kwanza kutoka kushoto), akiwa na wahitimu wenzake

Imeandikwa na Henry Kazula,

Mshiriki wa mafunzo ya ujasiriamali,

Mkurugenzi mtendaji;

1.Jielimishe Kwanza!

2."Science and Fine arts Resource Centre (SFRC)"

 

Kampuni inayokwenda kutoa elimu ya masomo ya sayansi(Baolojia,Kemia na Fizikia) na uchoraji kupitia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) au kwa kiingereza Information Communication Technology (ICT).

 

Ukiwa mdau wa elimu na unayependa utolewaji wa elimu bora  na inayozingatia mabadiliko ya teknolojia kwa vijana unaweza kuwasiliana na Henry Kazula kupitia: 

 

Simu ya mkononi:

+255 754 572 143/ +255 716 o75 826/ +225 785 175 157.

Barua pepe:jielimishekwanza@gmail.com

Imetolewa na

Jielimishe Kwanza!

(2013).


 


Alhamisi, 30 Mei 2013

MICHEZO: MJAPANI MWENYE UMRI WA MIAKA (80) AVUNJA REKODI YA KUKWEA KILELE CHA MLIMA MREFU DUNIANI-MLIMA EVEREST!




PICHA:Yuichiro Miura,(80):www.outsideonline.com
Mlima Everest, urefu mita 8,848:Picha imetolewa: www.guardian.co.uk
Mpandaji milima Yuichiro Miura, 80, amefanikiwa kufika kilele cha mlima Everest [Mei 23 2013], na kuwa mzee kikongwe wa kwanza duniani kupanda mlima huo mrefu kuliko yote duniani.Hili ni jaribio lake la tatu la kukwea mlima huo, jaribio hilo lenye mafanikio kwake lilihitaji uvumilivu na jitihada ya pekee, 


bila kujali umri wake na uwezo wa afya yake aliamua kujitoa mhanga.

Akielezea changamoto alizopata katika kukwea mlima licha ya uzee wake,kikongwe huyo alisema, "ilikuwa ni changamoto ya aina yake kukifikia kilele cha mlima" "Imekuwa hivi kama heshima kubwa kwa asili ya Mama"alisema hayo kupitia mtandao wake"Akitumaini kuongeza hata chembe ya kuishi."

Miura hakufanikiwa katika jaribio lake la kwanza la kufika juu ya mlima Everest hadi mwaka 2003, akiwa na umri wa miaka 70. Alifanikiwa kutembea umbali mrefu akiwa na mtoto wake, na kujiwekea rekodi ya mtu mzee duniani kupanda mlima.

Habari hii ya kikongwe Miura iwe funzo kwetu tulio na nguvu na damu yenye kuchemka.Vipi tumejiwekea malengo? je kuna jitihada yoyote tunayofanya kuyafikia malengo? au tunabaki kila siku kusema"One day yes! au Kama Mungu akipenda..." na hali tukiwa tumebweteka na vile vidogo 
tulivyo navyo?
 

Imetolewa na 

Jielimishe Kwanza!


Jumatano, 29 Mei 2013

MALEZI NA FAMILIA:HIZI NI TABIA ZA AWALI KABISA KWA MTOTO/KIJANA ANAYEANZA KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA!

Jumanne, 14 Mei 2013 niliandika makala kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana. 

http://jielimishekwanza.blogspot.com/2013/05/vijana-matumizi-ya-madawa-ya-kulevya.html


Picha kutoka:blog.stopyouraddiction.com


Sambamba na makala hiyo, napenda kutoa angalizo kwa wazazi na walezi kuhusu tabia na mwenendo wa watoto na vijana wao.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema "kinga ni bora kuliko tiba."Hivyo ni vyema kufahamu mabadiliko ya tabia kwa watoto/vijana na kufanyia kazi mapema.

Tafiti mbali mbali zimeainisha kuwa vijana na watoto hubadilika ghafla kitabia pale tu waanzapo kutumia madawa ya kulevya.

Zifuatazo ni tabia na ishara za awali na za wazi kwa mtoto/kijana anayeanza kutumia madawa ya kulevya;

1. KUJITENGA NA WANAFAMILIA

Mtoto/kijana hupenda kujitenga na wanafamilia kwa kujifungia chumbani, pia hujitenga katika suala la mlo wa pamoja; kwa kifupi hupenda kula peke yake.Pia hukwepa kujihusisha na masuala mengine ya kifamilia;
Ni vizuri kulitazama badiliko hili la tabia na kulifanyia kazi bila kuchelewa. 

2.KUJIHUSISHA NA MAKUNDI MAOVU

Picha kutoka:http://alcoholism.net/alcohol-abuse/alcohol-abuse
Utashangazwa kumuona mtoto wako akiwa na marafiki waovu na wasio na mwelekeo wa maisha, hapa kuwa makini, chukua hatua.

 Badiliko hili la kitabia huambatana na kuongezeka kwa tabia ya ugomvi inayoendana na kulipa visasi.

3.KUJIAMINI KUPITA KIASI

Mtoto/kijana hubadilika kitabia, kwa kujiona na pia kuona kuwa hakuna kitu kinachomshinda kwenye dunia hii, na hugeuka kabisa kutokubali kushauriwa na mtu yoyote   kuhusu maisha yake.

4 .KUJIBIZANA NA WAZAZI/WALEZI BILA HOFU

Kutokana na sababu ya (3), utashangazwa sana kumuona mtoto/kijana wako akikujibu majibu ya hovyo pale unapomweleza mambo ya maana kuhusu maisha yake.Katika hatua hii kuwa makini sana, unaweza kujikuta unapata "stroke" kwa kuona mtoto/kijana wa kumzaa anakudharau kupita kiasi!

5.KUOMBA PESA MARA KWA MARA

Kutokana na kuongezeka kwa matumizi na uhitaji wa madawa ya kulevya katika mfumo wa fahamu, mtoto/kijana wako atakuwa mhitaji mkubwa wa madawa hayo ambayo yanauzwa.Ukijaribu kumuuliza atakwambia kuna vitu anataka kununua.

6.KUIBA VITU VYA NYUMBANI NA KUUZA

 Endapo mtoto/kijana atashindwa kupata pesa ya kununulia madawa ya kulevya, usishangae kuona vitu vinapungua nyumbani na kuelekea kusikojulikana.Hapa fanya uchunguzi na uchukue hatua.

Kipindi kingine nitaeleza jinsi ya kumsaidia mtoto/kijana aliyapatwa na janga hili!

Lakini tusisubiri tiba ilihali dalili tunaziona, mzazi/mlezi usichukulie mabadiliko hayo kama kitu cha kawaida... 

Jielimishe Kwanza!

Masomo zaidi:




Jumanne, 28 Mei 2013

ELIMU NA UTENDAJI: KUFAHAMU BILA YA KUTENDA NI SAWA NA KUTOFAHAMU KABISA! KUJIFUNZA BILA YA KUTENDA NI SAWA NA KUTOJIFUNZA KABISA!

Nimeamua kutumia maneno haya makali kutoka kwa mwandishi Stephen R.Covey katika kitabu chake “The 8th Habits of highly effective people” ili kukumbushana kuhusu masuala muhimu katika elimu na utendaji.
Picha kutoka:www.vpi-inc.com

Nikizingatia mfumo mzima wa elimu, ambao umetuandaa kuwa waajiriwa na si kutumia ufahamu na ujuzi tuliosomea kujiajiri na ikiwezekana kuajiri wengine ni muhimu sana kutafakari na kuwa na mtazamo mwingine.
Utakubaliana na mimi kuwa wafanyakazi wengi nchini Tanzania wanafanya kazi nje ya taaluma zao.Lengo kubwa hapa ni kuangalia maslahi, wakati huo huo wakiweka pembeni ubora na tija katika utendaji. Hapa tunapata tatizo la kushuka kwa ubora wa huduma mbali mbali, hivyo kushusha pato la Taifa.
Imezoeleka kuwa, ili mtumishi apande cheo au kupanda ngazi ya mshahara, ni lazima aende kusoma zaidi.Swali la kujiuliza, je wanachoenda kukisomea wanakitumia kuboresha utendaji?...jibu unalo msomaji. Hapa nitarejea maneno yale yale…kujifunza bila kutenda ni sawa na kutojifunza kabisa!
Kuna ugonjwa mkubwa sana katika Taifa hili, hasa kwa wafanyakazi au waajiriwa kupenda kufanya kazi kwa mazoea na si kutumia taaluma.Wengine wamebaki kunung'unika bila ya kuchukua hatua kwa kufuata utaratibu unaostahili.
Kuna tatizo jingine, hasa kwa wahitimu kutoka vyuoni, utamwona “graduate” anajitamba na vyeti vyake kuwa anafahamu mambo mengi kuhusiana na taaluma yake.Lakini tukimwambia onyesha uwezo wako katika utendaji…mh! Ni shida kubwa.
Ningependa kuwafumbua macho vijana wengi waliomaliza vyuo.Katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya uchumi yanayochochewa na Sayansi na Teknolojia ni muhimu kuwa mtendaji na si mtu wa kufahamu peke yake.
Kama malengo yako ni kuajiriwa basi tambua kuwa unatakiwa kuwa mchangiaji wa ubora katika kampuni au sekta fulani. Ukikosa kuwa na mchango wa ubora katika kampuni au sekta hiyo basi ujue utakosa kazi au kupewa ujira usiolingana na ndoto zako.
Mwandishi na msemaji maarufu wa hadhira-Jim Rohn aliwahi kusema “people get paid by bringing value to the market place” akimaanisha, “watu hulipwa ujira kulingana na ubora wa kazi waletao kwenye soko, tunapozungumzia soko inamaanisha uhitaji katika jamii.

Naomba nikuache na usemi kutoka kwa Raisi wa 26 wa Marekani Theodore Roosevelt alisema:
 "Great thoughts speak only to the thoughtful mind, but great actions speak to all mankind."-Mawazo makuu au fikra kubwa hueleweka kwa walio na upeo wa kufikiri, bali matendo makuu hueleweka kwa kila binadamu"

Imeandaliwa na Henry Kazula,
Jielimishe Kwanza! 
 




Jumamosi, 25 Mei 2013

MAZINGIRA: ONGEZEKO KUBWA LA HEWA UKAA DUNIANI!!!

Utafiti uliofanywa na wanasayansi katika maabara ya serikali nchini Marekani huko Hawaii zimethibitisha kuwepo kwa ongezeko kubwa zaidi la hewa ukaa duniani kufikia mia nne kwa milioni moja ya sehemu za dunia. Ongezeko hili ni la kwanza kihistoria.

Wakiripoti kupitia BBC Swahili, walieleza kuwa ongezeko hilo liliwahi kutokea miaka milioni tatu hadi milioni tano iliyopita ambapo ilikuwa chini ya mia nne kwa sehemu milioni moja za dunia(400ppm).

Wanasayansi hao wamebaini kuwa kuna sababu mbali mbali zinazochangia ongezeko la hewa ukaa duniani, hasa ni hewa ukaa itokanayo na gesi inayotengenezwa na binadamu.

Hii ikimaanisha kuwa ongezeko kubwa la idadi ya watu limepelekea ongezeko kubwa la hewa ukaa.

Vile vile, walibaini kuwa ongezeko kubwa la hewa ukaa limepelekea kuongezeka kwa joto duniani mara dufu.

__________________

Gesi kutoka viwandani katika kuchangia ongezeko la hewa ukaa.                                     www.rose-kajivo.blogspot.com

Nikiungana na sababu moja ya kuwa binadamu ndiye chanzo cha ongezeko la hewa ukaa duniani na nyingine ambazo hazikuanishwa, naweza kusema kubwa ni shughuli za binadamu hasa ongezeko la viwanda duniani vinavyotoa hewa ukaa kwa wingi, utumiaji wa magari na motokaa hasa yale mabovu.

Sababu nyingine ni uharibifu mkubwa wa misitu ambayo kisayansi ina mchango mkubwa sana katika kupunguza hewa ukaa kupitia mfumo wa utengenezaji wa chakula.

Uharibifu wa mazingira unachangiwa sana na umasikini uliokithiri hasa katika nchi za Afrika.Pia kubadilisha maeneo la misitu kuwa makazi ya kudumu.

Kukata miti kama kuni kwa matumizi ya nishati www.lukwangule.blogspot.com




 

Juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa na hasa zinaanza na usimamiwaji mzuri wa sera na sheria na kanuni za kila nchi kuhusu utunzaji wa mazingira.

Ukiangalia kwa kina kuhusu chanzo cha tatizo, kinahusu nchi zilizoendelea(kupitia viwanda vikubwa na utumiaji wa magari na motokaa) na nchi zinazoendelea (ukataji wa miti kwa matumizi ya nyumbani kama nishati ya kupikia, magari mabovu na yenye kiwango cha chini).

Tunaweza pia, kuanzia hapo, hasa kwa kubadilisha gesi za viwandani kwa matumizi mengine na si kutupiwa angani.Kupunguza matumizi ya motokaa na magari binafsi hasa yale mabovu na yaliyo chini ya kiwango.

Tunaweza kupunguza matumizi ya magari

                              www.do4five.co

Tuhamasishe upandwaji wa miti kila mahali panapostahili na kuzuia ukatwaji wa miti usikuwa na tija.Ni vyema kuyaboresha maeneo kama mashimo yaliachwa kwa shughuli mbali mbali kuwa misitu.

Tukumbuke kuwa, mabadiliko ya kuifanya dunia yetu kuwa sehemu nzuri ya kuishi yanaanza na mtu mmoja.

 

 

Na Henry Kazula.

Jielimishe Kwanza! Chukua hatua...

Alhamisi, 23 Mei 2013

MTAZAMO: Jinsi ya kupaza sauti ya mafanikio na jamii ikukubali...


Sauti na mafanikio yako katika kile unachotarajia kukifanya ili kujipatia kipato yanategemea muunganiko wa mambo muhimu manne(4); Kipaji chako, Shauku yako, dhamiri yako na kikubwa zaidi ni kuangalia uhitaji wa unachotaka kukifanya kwenye jamii.

Zig Ziglar aliwahi kusema, “ukitaka kufanikiwa na kupata ukitakacho, wasaidie wengine kwanza kupata wanachohitaji…”.

Jumatano, 22 Mei 2013

UCHUMI / BIASHARA:Tengeneza Pesa kupitia mitandao ya kijamii...

Picha:www.edudemic.com
Ukifuatilia kwa kina utagundua kuwa watu wengi wanapoteza muda na fursa njeti ya kutangaza shughuli au biashara wanazofanya. 

Unajua ni kwa jinsi gani ilivyo rahisi kwa sasa kukutana na watu wengi unaowafahamu na usiowafahamu kupitia mitandao ya kijamii? Hivyo basi, tumia fursa hii kutangaza biashara yako au kazi unazofanya kwa huo umati wa wanajamii. Zingatia maadili na sheria za nchi unapotangaza biashara yako...

Kizuri zaidi hapa, hakuna gharama kubwa ya kujitangaza...ni bure kabisa! Ikiwa unahitaji kutengeneza ukurasa ili uwekwe kwenye upande wa matangazo ndiyo utalipia gharama kidogo kwa mtandao wa kijamii husika.

Naomba nikuhakikishie kuwa kwa kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ni rahisi mno kuwasiliana na watu wengi kuliko kawaida.

Imekuwa ni mazoea mtu kuweka picha mbali mbali mfano akiwa anakula, na nyinginezo za kujionyesha ili watu wabonyeze kitufe cha "like". Je, unaingiza shilingi ngapi kwa watu kubonyeza kitufe cha "like"? au unalipwa shilingi ngapi kwa kubonyeza kitufe cha "like"? 

Kuna wengine kazi yao kubwa ni kubonyeza tu kitufe cha "like" hata kama kuna picha ya msiba au majonzi au kama kuna picha  ya tukio la maovu.

Nisieleweke vibaya, namaanisha ni vizuri pia kuangalia faida ya mitandao hii ya kijamii kwa upande mwingine tofauti...hatimaye kujiongezea kipato.

Haya tuachane na hilo, tufanye nini ili kutengeneza pesa kupitia facebook,twitter, na mingineyo?
  1. Wajulishe marafiki kuhusu biashara yako, weka picha ya bidhaa unazouza na mawasiliano.
  2. Tumia muda vizuri kwa kuhakikisha "unachat" na mtu bila kusahau kumueleza biashara yako.
  3. Tengeneza ukurasa unaoeleza biashara yako, ukiweza ilipie ili ikae upande wa matangazo kutegemeana na mtandao wa kijamii husika
  4. Kwa wale wanaotafuta kazi, weka sifa ulizo nazo watu wajue uwezo wako...kwa hakika utajikuta unaunganishwa kupata kazi.Usione aibu kujielezea kuwa huna kazi.
  5. Tumia mitandao ya kijamii kupata fursa za kubuni aina ya biashara au huduma kwa jamii.
Kila la heri.
Imetolewa na
Jielimishe Kwanza!

HABARI MUHIMU: Ziara ya Rais Obama nchini Tanzania,Afrika Kusini na Senegali...


Jarida maarufu la habari nchini Marekani-“Fox News” la tarehe 20 Mei 2013 limeripoti kuwa raisi wa Marekani-Barack Obama anataraji kuzitembelea nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Ziara hiyo muhimu itahusisha nchi tatu za Afrika; Afrika Kusini, Senegali na Tanzania.

Picha::www.letemps.blogs.com
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani “White House” inasema kuwa raisi Obama na mkewe Michelle Obama wataondoka Marekani tarehe 26 Juni 2013 kuelekea Senegali, Afrika kusini na mwisho Tanzania. 

Obama anatarajia kuonana na viongozi wakubwa wa nchi hizo, ikiwemo viongozi wa makampuni ya biashara, mashirika ya kijamii na jumuiya mbali mbali za vijana.

Utawala wa “White House” umeeleza kuwa ziara hii ya Obama ni chachu ya  mahusiano muhimu na yenye ukaribu  kati ya Marekani na nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
__________________________________________________________________

Sambamba na ujio huu mzito kwa Tanzania,Afrika Kusini na Senegali kumekuwa na manung'uniko mbali mbali hasa kwa nchi za jirani na Tanzania, eti kuwa -kwanini Tanzania? Ndugu msomaji naomba nawe ujiulize ni kwa nini? kwa nini si Kenya au Uganda au Rwanda au Burundi? 

SOMA ZAIDI:

Jumanne, 21 Mei 2013

TRAINING: MASTER SWAHILI LANGUAGE



AFYA YAKO NA MAZINGIRA:Je, unayajua madhara ya mifuko ya rambo kwa afya yako na mazingira?

Jumanne,21 Mei 2013

Kumekuwa na utaratibu uliozoeleka kwa watu wengi kubebea chakula mfano chips kwenye mifuko ya rambo, na mara tu wakiisha maliza uhitaji wao wa chakula huzitupa rambo hizo hovyo bila kujali madhara kwao na mazingira.

Utakubaliana na mimi kuwa mazingira yetu yamezungukwa na takataka nyingi hasa mifuko ya rambo.Kila mtu amechukulia ni sehemu ya matumizi ya kawaida tu kutumia mifuko hiyo ambayo inaelezwa kitaalamu kuwa haiozi na kwa lugha ya kigeni iliyozoeleka kuwa "Not-biodegradable". 

Yapo madhara mengi ya kiafya kwa kutumia vyakula vilivyohifadhiwa ndani ya mifuko hiyo pia kuzagaa kwa mifuko hiyo kwenye mazingira.Kuzagaa kwa mifuko ya rambo kumeendelea kuleta madhara kwa viumbe vya majini na nchi kavu.

KIUNDANI ZAIDI UNAWEZA KUPITIA MAKALA YANGU ILIYOANDIKWA KWA LUGHA YA KIINGEREZA KUPITIA: 

MAZINGIRA:Jukumu letu kuwatunza na kuwahifadhi viumbe hawa adimu...

  Jumanne, 21 Mei 2013


Photo: http://worldwildlife.org/species
Kuna viumbe ambao ni adimu sana, mfano faru,ni kutokana na hali yao ya kuzaliana; kuna mpishano mkubwa wa miaka ya kuzaliwa kati ya mmoja na mwingine.Pia huzaa idadi ndogo ya vizalia.Viumbe hawa adimu wanapaswa kutunzwa kama mboni ya jicho kwa mantiki kwamba wapo kwenye hatari kubwa ya kutoweka duniani.

Inafahamika kwamba viumbe vyote duniani huishi kwa kutegemeana na endapo kutatokea upungufu au kutokuwepo kwa kiumbe fulani, hupelekea kuharibika kwa mlishano ulio sahihi kwenye eneo husika viumbe vinapopatikana.

Ni jukumu letu kuwatunza viumbe hao adimu na ikiwezekana kuwazalisha katika maeneo mengi duniani kuzingatia na mazingira furahishi kwa viumbe hao.

Taarifa nyingine: 
http://www.slideshow.com/users/heka/extinction-of-species-690254261
 

http://mazingira-leat.blogspot.com/2010/10/vyura-wa-kihansi-thamani-ya-maliasili.html

Jumatatu, 20 Mei 2013

MALEZI: Zijue mbinu (12) za kumsaidia mtoto wako kuepukana na matumizi mabaya ya Televisheni na intaneti:

www.syracuse.com
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi wengi kuwa watoto wao hawabanduki kwenye televisheni na wengine kupenda kushinda kwenye intaneti wakiangalia picha chafu zinazowafanya wakue haraka kabla ya umri wao wa mabadiliko ya kibaiolojia.

Watoto wengi wanaamini na kuheshimu maagizo yatolewayo kutoka katika vipindi mbali mbali, hivyo kupingana vikali na maagizo/matakwa ya wazazi/walezi. 

Hapa utagundua kuwa muongozo wa tabia za watoto wetu unategemea na kuathiriwa sana na kupishana kwa itikadi mbili tofauti; yaani zile za kwenye vipindi visivyo na tija kwenye televisheni na zile za wazazi/walezi.

Tatizo hili limewapelekea watoto wengi kukosa maadili na kushuka kwa taaluma zao na kushindwa kuwa na muda wa kujipangia malengo yao ya baadaye, hivyo kutengeneza kizazi kisichojitambua, kisichokuwa na malengo wala muelekeo.Yaani ni kizazi cha bendera fuata upepo. 
www.mirror.co.uk
Pia kuna matatizo mbali mbali ya kiafya kwa mtoto yatokanayo na kukaa muda mrefu kwenye televisheni au intaneti, nayo ni;

  • Kuongezeka uzito isivyo kawaida
  • Maumivu ya macho kutokana na mionzi
  • Kuumwa kichwa
  • Ubongo kushindwa kuimarika hasa kwa watoto walio chini ya miaka 2
  • Kuwa kwenye hatari ya kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya...
Kutokana na utafiti nilioufanya kwa kushirikiana na tafiti nyingine, nimegundua mbinu zifuatazo ambazo wewe kama mzazi/mlezi ukizisimamia kikamilifu zitamsaidia mtoto wako, nawe kuishi maisha ya furaha pamoja na familia yako:

1.Mfanye mtoto wako kuwa msomaji wa vitabu, wewe ukiwa mfano

Mzazi/mlezi unatakiwa kusoma vitabu mbali mbali na pia kumsomea mtoto kitabu na kutoa simulizi mbalimbali kutoka kwenye vitabu.Mpatie majukumu ya kufanya kutoka katika vitabu alivyosoma; hasa kuandika taarifa fupi ihusuyo kitabu husika.

2.Mfanye mtoto aweze kuchagua vipindi vya kuangalia,wewe ukiwa mfano 

Inatakiwa ieleweke kuwa, si kila kinachoonekana kwenye Televisheni kinafaa kuangaliwa na kila mtu.Makampuni mengi huandaa vipindi kwa lengo la kufanya biashara na kwa kiasi kidogo kuelimisha umma.Mzazi/Mlezi unatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika suala hili na si kuwa mtu wa kuruhusu uozo wa aina yoyote ile.Anza kumkuza mtoto kwa maadili mema na atakulia katika njia hiyo.

3.Panga utaratibu unaoeleweka kwa kila mwanafamilia

Kuishi maisha yasiyo na mpangilio ni hatari kubwa. Ni vizuri kuwa na utaratibu mzuri wa kula, kusoma, na kulala.Ni dhahiri kuwa wazazi/walezi mna majukumu mengi, lakini yasiwafanye kuepuka na kuwa kisingizio cha kutotimiza wajibu wenu.

4.Toa zawadi kwa mtoto akipunguza muda wa kuangalia televisheni

Inaweza kuwa ni zawadi inayohusisha matembezi ya kawaida au kutembelea matamasha, pia unaweza kumpatia mtoto zawadi ya nguo, vitabu au CDs zenye mafunzo. Hii itamfanya mtoto kupata msukumo zaidi wa kupunguza muda wa kukaa kwenye televisheni.

5.Fanya utaratibu wa matembezi kwenye vivutio mbalimbali

6.Usiweke televisheni kwenye chumba cha watoto

7. Mjengee mtoto kuwa kujifunza kunawezekana kwa kuona hali halisi na si lazima televisheni 

Mzazi/Mlezi unaweza kutumia vitu asilia katika mazingira yanayotuzunguka kumssaidia mtoto kujifunza na si kutegemea afundishwe na Televisheni na intaneti.

8.Mweleze mtoto hasara za kutumia muda mwingi kwenye televisheni na intaneti

9.Mhusishe mtoto kwenye klabu za michezo na vikundi vya sanaa ili kukuza kipaji chake

10.Weka namba ya siri kwenye televisheni na kuiwasha pale inapohitajika

11.Hakikisha unakuwa na muda wa kujumuika na familia yako

12. Mpe mtoto majukumu ambayo atatakiwa kuwasilisha kwa wakati

Imeandaliwa na: Henry Kazula

Jielimishe Kwanza! 


Jumapili, 19 Mei 2013

MALEZI: Madhara (8) ya kumzuia mtoto wa umri (Miaka 3-12) kushiriki michezo na watoto wa rika lake...


Ijumaa, 3 Mei 2013
Wazazi wengi nchini na jamii nyingine wanapenda kuwaona watoto wao wakiwa kama wao
walivyokuwa enzi hizo.Kwa maana nyingine wanataka kuwaona watoto wao wakiwa kama nakala zao.
Watoto wa umri kati ya miaka 3-12(ni umri kabla ya kuanza shule na kuanza shule) huonyesha tabia za kutaka kufanya vitu wenyewe bila kuzuiliwa na mtu yeyote. Hupenda kujifunza lugha, na ishara mbalimbali kwa kasi isiyo ya kawaida. Hapa wazazi wengi huwachukulia watoto wao kuwa ni watundu na wasumbufu,la hasha! Ni umri wao kutaka kujifunza kuhusu mambo yanayowazunguka.

Kama mwanasaikolojia, Maria Montessori alivyoainisha kuhusu makuzi ya watoto, anasema kuwa watoto wa  rika hili hupenda kuwa na urafiki na watoto wa rika lao. Pia kuhusu kuwaruhusu watoto wafanye vitu wanavyoweza kufanya na si kulazimisha kuwasaidia.Alisema, "Never help a child with a task at which he feels he can succeed." Yaani “Usimsaidie mtoto kufanya kazi iliyo kwenye uwezo wake.”

Kiuhalisia makuzi ya watoto hutegemea sana mazingira, mfano mtoto aliyekulia mazingira ya shida na duni kiuchumi anatofautiana sana kiutendaji na yule aliyetokea mazingira ya raha na furaha na uchumi mzuri.Tofauti hii ambayo inahusisha saikolojia ya makuzi ya mtoto, ina uwezo mkubwa sana wa kushusha au kuongeza/kuimarisha utendaji wa mtoto afikiapo utu uzima.

Nitazungumzia tofauti za watoto katika mazingira hayo mawili katika makala nyingine.Leo napenda uungane nami katika kuyajua madhara (8) ya kumzuia mtoto wako kushiriki michezo ya kawaida na wenzake...

Mwanasaikolojia maarufu duniani Erick Erickson 1956 aliainisha hatua nane(8) za maendeleo ya makuzi ya binadamu kijamii na kihisia kuanzia kuzaliwa hadi utu uzima.Alisisitiza kuwa kila hatua ina vipingamizi vyake ni muhimu kupitia kila hatua na kuondoa vipingamizi hivyo kabla ya kwenda hatua nyingine. 

Nitapenda kujikita hasa kwenye makuzi ya watoto ambayo yana mchango mkubwa kwa utu uzima wa mtu.Nikizingatia hatua mbili za makuzi ya mtoto yaani hatua ya 2 na hatua ya 3 za maendeleo ya ukuaji wa mtoto kama alivyozielezea Erickson;

Katika hatua ya pili (2) umri wa mtoto kabla ya kuanza shule (chekechea), aliangalia mambo mawili yanayopingana yaani “Kujifunza mwenyewe Vs Aibu (miaka 3-4)”.Akimaanisha kuwa mtoto wa umri huu hupenda kufanya mambo mwenyewe na hujisikia aibu pale anapokatazwa kwa kuambiwa “Usi…” Mtoto aliyekuzwa vizuri hujisikia vizuri bila kuwa na aibu yoyote.

Pia katika hatua ya tatu (3) umri wa kuanza shule (baada ya chekechea), umri wa michezo, mtoto hupambana na vitu viwili yanayopingana yaani Kujianzishia kujifunza Vs Kujilaumu/Hatia.(miaka 4-12). Akimaanisha kuwa mtoto aliyekuzwa vizuri kwa kupewa uhuru wa kujifunza (1) hujiona fahari kuwa na wenzake,(2) hupenda kushirikiana na wenzake, (3) hupenda kuongoza pia kuongozwa.
Kwa upande mwingine, mtoto aliyekuzwa mazingira ya kubanwa hujihisi kuwa na hatia hivyo (1) huwa muoga (2) hujitenga na wenzake (3) anakuwa tegemezi sana kwa wazazi (4) anakuwa amekosa mbinu za michezo na uwezo wa ubunifu.
Nitayajumuisha madhara (8) ayapatayo mtoto wako kwa kukosa kushiriki michezo ya kitoto na wenzake kama ifuatavyo;
___________________

1.Mtoto kukosa uwezo wa kujiamini mbele ya hadhara.

Ukifuatilia michezo ya watoto kama mpira,kukimbizana, na mingine mingi utagundua kuwa watoto ni waongeaji na watendaji hasa wakiwa na watoto wa rika lao.Endapo mtoto wako atakosa fursa ya kukutana na wenzake, kwanza atakuwa na hofu-kwasababu hajawazoea, pili atajihisi mnyonge mbele ya wenzake.Hivyo kuanza kuijenga tabia ya kutokujiamini tangu utotoni.

2.Kukosa uwezo wa kuongoza
Kutokana na hofu aliyojingea tangu utotoni, ni dhahiri kuwa atakuwa hana mbinu za kuwasiliana kama kiongozi, pia atakuwa na aibu iliyopitiliza mbele ya watu anaotakiwa kuwaongoza.

3.Kuwa mtegemezi wa maamuzi mbali mbali kwa wazazi hata yaliyo kwenye uwezo wake
Tatizo hili ni kubwa, limepelekea vijana wengi kushindwa kuamua mambo yao wenyewe, eti “labla nimuulize baba na mama”, kazi lazima achaguliwe na wazazi/walezi.
Hili ni tatizo lililokuwa tangu utotoni, yaani kukosa uwezo wa kuamua kufanya hasa baada ya kuambiwa “Usi…” na kutopata nafasi ya kuona watoto wengine wakijaribu kufanya jambo fulani.

4.Mtoto hujitenga na jamii
Kwa kuwa mzazi au mlezi ulimtenga mtoto na jamii kwa kumfungia ndani wakati wote, na kumwachia mtoto wako awe na urafiki mkubwa na Televisheni na michezo yake pekee, usitegemee kuona mtoto wako akiwa mbali na jamii hasa afikapo ujana na hata utu uzima.

5.Kukosa uwezo na mbinu za kuwasiliana
Kama nilivyoeleza awali, watoto wa umri huu hupenda kujifunza lugha na ishara mbali mbali za mawasiliano wakiwa na watoto wa rika lao.Hivyo basi, kama utamfungia mtoto wakati wote asikutane na wenzake, tambua kuwa unamwandaa mtoto ambaye atakuwa hana uwezo mzuri kimawasiliano.Ujuzi huu ni muhimu sana katika shughuli mbali mbali za kijamii.

6. Kuwa na viungo dhaifu na kukosa uchangamfu wa mwili
Itafahamika kuwa uimara wa viungo vya mtoto haujengwi na vyakula pekee, bali mazoezi ya viungo hasa kwa michezo ya kitoto ya kukimbizana hapa na pale.Kisaikolojia, mtoto huathirika sana anapoona watoto wengine wakicheza kwa furaha wakati yeye anazuiliwa ama kwa kupigwa na kukaripiwa.Hii humfanya mtoto kunyongea na kukosa uchangamfu.

7.Humpelekea mtoto kujitengenezea tabia ya kutoroka ili atimize hisia zake 
Hapa ndipo utukutu na tabia mbaya zinapoanzia.Mtoto anaamua kujitengenezea mbinu ili aweze kushiriki kwenye michezo ya kitoto.Mtoto anapofikia hatua hii, wazazi wengi hulaumu sana kuwa watoto wa siku hizi hawatulii, wakiwa wamesahau kuwa wenyewe ndiyo chanzo cha kuwafanya watoto watoroke kwasababu ya ulinzi mkali nyumbani. Mtoto hawezi kutoroka nyumbani kama anapata upendo na kueleweshwa mema na mabaya kwa vitendo, pia kwa kumpa na kukubaliana utaratibu wa michezo.

8.Mtoto kukosa ubunifu wenye tija ya kupambana na changamoto za maisha
Ubunifu wa mtoto unachangiwa na kuwepo kwa ushirikiano wake na watoto wenzake.Ni hapo kipaji cha mtoto kinapojidhirisha. Kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, wazazi wengi wamewaachia watoto wao kutazama televisheni na komputa na si kwenda kucheza na watoto wengine.
Naomba nitoe rai yangu kwa wazazi wa karne hii ambao mnakumbana na changamoto mbali mbali za mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kiasi kwamba mnakuwa hamna muda wa kukaa na watoto, ila ni kutoa amri kuwa hairuhusiwi mtoto kutoka nje.

Ni vizuri kufuatilia kila hatua ya ukuaji wa mtoto na kuhakikisha yale mahitaji ya hatua husika yanafikiwa, kinyume na hapo tusishangae kuona watoto wetu wamekuwa vile tusivyotarajia.
Ungana na mkala yangu nyingine kuhusu "Sababu zinazoweza kumfanya mtoto wako kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya akiwa katika umri mdogo."

SOMA HII PIA KUMSAIDIA MTOTO WAKO KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA INTANETI NA RUNINGA http://jielimishekwanza.blogspot.com/2013/05/malezi-na-familia.html

Makala hii imeandikwa na Henry Kazula, ikiwa ni utafiti wake binafsi ukisaidiwa na nadharia kutoka tovuti zifuatazo:
  http://www.dailymontessori.com/montessori-theory/